Msanii wa muziki na mtafiti wa masuala ya sanaa nchini,Innocent Nganyagwa maarufu kama Ras Ino akizungumza na wadau wa sanaa wakati akiwasilisha mada kuhusu Ubora wa Tungo Katika Kazi za Sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu katika Ukumbi wa BASATA.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti,Mafunzo na Habari,BASATA Bw.Godfrey Mungereza.
Mratibu wa Jukwaa la Sanaa Bw.Ruyembe Mulimba akichochea mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.Kulia kwake ni Ras Ino.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti,Mafunzo na Habari,BASATA Bw.Godfrey Mungereza akisisitiza jambo wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA.Kulia anayemsikiliza kwa makini ni Innocent Nganyagwa.
Mdau akichangia mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa linaloandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa ushirikiano na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni nchini (CAJAtz).

Na Mwandhishi Wetu

Wasambazaji wa kazi za sanaa nchini wametajwa kuwa chanzo cha kudidimia kwa vipaji vya wasanii nchini kutokana na kuendekeza faida katika kuuza kazi za wasanii pasipo kuzingatia maudhui na ubora wa kazi zao.

Hayo yamesemwa wiki hii na msanii pia mtafiti wa masuala ya sanaa nchini Innocent Nganyagwa wakati akizungumza na wadau wa sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu ndani ya Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Alisema kwamba,wasambazaji wa kazi za sanaa wamekuwa wakijikita kwenye kuwaahidi wasaniii fedha na magari ili watoe albam au kazi za sanaa bila kuzingatia ubora na maudhui hali ambayo imekuwa ikisababisha kazi hizo zikose ubora na maadili ndani yake.

“Zamani wakati sanaa ni ridhaa,kazi za sanaa zilikuwa na weledi na zenye tungo zilizotukuka ndani yake lakini siku hizi weledi umepotea,wasanii wakishaahidiwa gari na milioni tatu na wafanyabiashara basi atalipua kazi haraka ili iingie sokoni.Hapa tutapata tungo bora?” Alihoji Nganyagwa.

Aliongeza kwamba,uwepo wa nyimbo za taifa na uzalendo vilisaidia sana upatikanaji wa tungo za sanaa zilizotukuka na halisi tofauti na sasa ambapo wasanii wamekuwa ni wa kuiga kila kitu pasipo kuzingatia uhalisia wa mazingira kutokana msukumo wa fedha.

“Kadri siku zinavyosonga mbele,wasanii wamekuwa wakitanguliza fedha kuliko uhalisia na maisha ya jamii inayowazunguka.Fedha zimekuwa mbele uhalisia nyuma.Hili ombwe katika sanaa ndilo limekaribisha mamluki katika sanaa kwa sababu kilichoko mbele ni fedha na si tungo na ubora katika sanaa” Aliongeza Nganyagwa.

Mbali na wasambazaji,uhaba wa miundombinu kwa wasanii,kubadilishwa matumizi kwa kumbi mbalimbali za burudani na kukosekana kwa sheria na sera madhubuti ya sanaa vilitajwa kama moja ya sababu ya kukosekana kwa tungo bora na madhubuti kwa wasanii.

Alihitimisha kwa kutoa wito kwa wasanii kuzingatia weledi katika kazi za sanaa na kuhakikisha wanatafuta msaada huo kila inapobidi kwani wataalam wapo.Aliwataka kuacha kufanya kazi za sanaa kwa kusukumwa na fedha bila kuzingatia uhalisia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...