Meneja Masoko na Uhusiano wa benki hiyo Linda Chiza akionyesha Kadi ya Faida kwa Wadau wa Diaspora (hawapo pichani) alipokuwa akiwasilisha mikakati ya benki ndani ya Diaspora katika mkutano wa tatu wa uratibu wa Wadau wa Diaspora uliofanyika mkoani Arusha mwishoni mwa wiki ambapo benki hiyo imedhamiria kuwaunganisha wadau husika na huduma za kibenki kupitia kadi hiyo kote duniani.Kushoto ni mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Ms Bertha Semu na katikati ni Mwezeshaji wa mkutano huo Cristentius Magori.
Na Mwandishi Wetu, Arusha
BENKI ya Exim Tanzania imedhamiria kuwaunganisha Wadau wa Diaspora kupitia kadi yao ya ATM ya Faida kwa lengo la kurahisisha mahitaji ya kibenki katika shughuli mbalimbali za maendeleo zinazolengwa kufanya chini ya Diaspora.
Pamoja na mkakati huo, benki hiyo ipo katika tathimini za mwisho kuandaa huduma mpya ya kibenki itakayokidhi mahitaji ya jumla ya wadau ndani ya Diaspora.
Meneja Masoko na Uhusiano wa benki hiyo, Linda Chiza aliyasema hayo katika mkutano wa tatu wa uratibu wa Wadau wa Diaspora uliofanyika mjini hapa mwishoni mwa wiki.
Chiza alisema benki yao imeamua kuingia na kuchangia nguvu zake ndani ya Diaspora katika kutambua kazi na umuhimu wa malengo yake na kwamba benki itahakikisha inakuwa mdau mkuu wa kuunganisha nguvu za wadau husika katika kuleta maendeleo ndani ya Tanzania.
“Hatua zetu za mwanzo kabisa katika Diaspora ni kuhakikisha tunawaunganisha wadau wote na benki yetu kupitia kadi yetu ya Faida ambayo inamwezesha mhusika kupata huduma za kibenki popote duniani lakini pia tumekuwa tukifanya tathimini ya kina kuona jinsi ya kuandaa huduma mpya kulingana na mahitaji ya Diaspora”, alisema Chiza.
Alisema mwaka jana chini ya Diaspora wameweza kuajiri watanzania tisa (9) wanaoishi Afrika Kusini na kwamba tayari wamefanya usaili kwa Watanzania wengine 35 wanaoishi London, Uingereza yote hayo yakilenga kushawishi kurudisha nguvu ya kimaendeleo ndani ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Huduma za Kibenki wa benki hiyo, Ramakrishana Rao alisema benki hiyo inawekeza nguvu nyingi kufika katika maeneo yasiyo na huduma za kibenki ndani na nje ya Tanzania hatua ambayo itasaidia kwa namna moja nyingine kufikiwa kwa malengo ya Diaspora.
Alisema tayari benki hiyo inatoa huduma zake nchini Comoro na Djibouti ambapo pia wana mipango ya kufika Kusini mwa Sudan kwa lengo la kurahisha mahitaji ya kibenki na kuwezesha nguvu ya watanzania waishio katika maeneo hayo kurudi nyumbani kwa njia ya kuwekeza na nyinginezo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, John Haule aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wake Bernard Membe aliwataka watanzania kuitumia vizuri Diaspora kwani nchi nyingine ndani ya Afrika Mashariki zimeweza kufaidika kwa kiasi kikubwa na mpango huo.
Alisema Tanzania imekuwa haifaidiki ipasavyo na watu wake wanaoishi nje hatua ambayo inaisukuma Serikali sasa kuona haja ya kuwekeza nguvu nyingi kuhakikisha Wadau wa Diaspora wanachangia maendeleo ya nchi.
Alisema nchi za Marekani na Uingereza tayari zina mitandao madhubuti ya kuwaunganisha watanzania wanaosihi huko na kwamba sasa ni jukumu la wizara yake kuhakikisha watanzania wanaoishi katika maeneo mengine nao wanaungana na kuchangia maendeleo ya nchi yao.
Huo ni mkutano wa tatu wa uratibu wa Wadau wa Diaspora uliojumuisha wadau kutoka nchi za Burundi,Kenya,Rwanda, Uganda na Tanzania kama wenyeji uliofanyika kwa siku mbili ikitanguliwa na ile iliyofanyika Januari na Juni mwaka jana.
kwakweli ninakubali sana kwamba ni lazima tusaidie nyumbani. sasa hili jambo la dual citizenship litafanyika lini. mbona maneno yamekuwa mengi na ya kurudia rudia kila siku. watanzania wengi wana sita kujiandikisha ubalozini kwasababu hawajui hili jambo la dual citizenship ni la kweli au vipi. wakenya wamepata dual citizenship bila ya serikali yao kuwauliza kujiandikisha ubalozini kwao. nimekaa na wakenya miaka mingi sana lakini hawaja wahi kuambiwa warudishe passports zao ili zibadilishwe kwasababu ya security reasons hizi au zile, lakini watanzania wamesha fanya hivyo sijui mara ngapi. kama ni juu ya wakimbizi wakenya wamekuwa na wakimbizi na wahamiaji haramu chungu nzima toka wapate uhuru. bureaucracies zimezidi tanzania.
ReplyDelete