Mwenyekiti wa bodi ya benki ya Exim Tanzania Yogesh Manek (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mambo mbalimbali ya kimaendeleo ya benki hiyo likiwemo suala la uwezeshaji katika mikopo walipokutana na Wakurugenzi wote wa bodi na Mameneja wa matawi yote nchini Dar es Salaam hivi karibuni kutathimini utatendaji wa benki hiyo.Kushoto ni Meneja Mkuu wa benki hiyo Dinesh Arora na katikati ni Meneja Masoko na Uhusiano Linda Chiza.
======== ========= =========
BENKI ya Exim Tanzania imetoa mikopo ya thamani ya zaidi ya sh. bilioni 10/- (USD milioni 8) kwa Wajasiriamali Wanawake kupitia mpango wake wa uwezeshaji wa WEF. Kutokana na hatua hiyo, benki ya Dunia imeipongeza benki hiyo katika Jarida lake linaloelezea mambo mbalimbali ya maendeleo lililotoka mwezi huu.
Jumla ya Wanawake Wajasiriamali 214 wamewezeshwa katika mikoa mbalimbali nchini kupitia mpango wa WEF wa benki hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu ya Ujasiriamali jumla ya wanawake 1344 nchini.
Akizungumzia hatua hiyo ndani ya Exim, Meneja wa mpango wa WEF, Felister Simba alisema umekuwa na maendeleo makubwa tangu kuanzishwa kwake na kwamba mpango huo na mingine ya uwezeshaji ndani ya benki hiyo ni mkombozi wa maisha ya wanawake nchini.
Alisema wanawake katika mikoa 15 nchini tayari wamepatiwa elimu kuhusu uwezeshaji na kwamba elimu hiyo sasa inawapa ujasiri wa kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo wakiwezesha na mikopo ya benki hiyo. “Kwa kweli tunapiga hatua na mpaka sasa tumeweza kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 10/- kwa wanawake wajasiriamali nchini, hatua ambayo ni ya kujivunia kibenki na nchi kwa ujumla”,
“Mpango wetu wa WEF, Akaunti ya Tumaini kwa pamoja na uwezeshaji wa benki ya dunia kupitia mipango yao mbalimbali ya uwezeshaji ikiwemo IFC na GBA maalumu kwa wanawake tumeweza kupiga hatua kubwa kwa kuwapa ujasiri wa kuthubutu wanawake nchini,” alisema Simba.
Alifafanua kuwa tafiti mbalimbali zilizofanywa na benki ya dunia zilionyesha kuwa kati ya 43% ya wanawake waliokuwa wakiendesha biashara ndogondogo nchini hadi kufikia mwaka 2006 ni 5% pekee waliokuwa na akaunti za benki.
Alisema hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa sasa na Wanawake wajasiriamali Tanzania kwa namna moja au nyingine imechangiwa na msukumo mkubwa wa mipango ya uwezeshaji ya benki hiyo ambayo sasa inatoa huduma katika mikoa mingi nchini. “Kabla ya kuhudhuria mafunzo wa uwezeshaji wa benki ya Exim chini mpango wao wa WEF yaliyofanyika Arusha mwishoni mwa mwaka 2007 nilikuwa nafanya biashara ndogo ndogo ambapo sikudhani kama ningeweza kuinuka katika kipindi kifupi”,
“Baada ya kupata mafunzo ambayo yalinijengea ujasiri wa kupanua biashara yangu, sikusita nikachukua mkopo Exim na sasa namiliki kiwanda kidogo cha usindikaji na nimeajiri watu wasiopungua 200”, anasema Monica Gaimo wa Arusha.
Benki hiyo ambayo hivi sasa ina matawi takriban 21 kote nchini, ni benki ya kwanza ya kitanzania kufungua matawi nje ya mipaka ya nchi, ambapo hadi sasa ina matawi kwenye nchi za Djibout na Comoro, huku mipango ya kufungua matawi katika nchi ya Zambia, ikiwa kwenye hatua za mwisho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...