Na Hadija Chumu – MAELEZO,Dar es Salaam
KAMPUNI ya Vision Investment inatarajia kuandaa maonesho ya siku tatu ya wadau na wafanyabiashara wa zana za magari na huduma shirikishi yatakayoanza tarehe 7 hadi 9 Oktoba, mwaka huu katika viwanja vya Kijitonyama jijini Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mratibu wa maonesho hayo Ally Nchahaga amesema maonesho hayo yatawanufaisha wafanyabiashara, wadau na watumiaji wa magari kwa kuwa watapata fursa ya kujitangaza kitaifa na kimataifa.
“Maonesho haya ya zana za magari yatawasaidia wafanyabiashara kutangaza bidhaa zao katika masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi”, amefafanua Nchahaga.
Mbali na kujitangaza, pia wafanyabiashara hao watapata fursa ya kukutana, kubadilishana mawazo na ujuzi katika sekta nzima ya magari.
Nchahaga amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ili kujifunza masuala mbalimbali yanayohusiana na zana za magari pamoja na suala zima la usafirishaji na huduma zake shirikishi.
Maonesho haya ya zana za magari ni ya nne tangu kuanzishwa kwake na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ulinzi katika uendeshaji gari ni ufunguo wa usalama barabarani”.
Kiswahili pia kinatupa taabu jamani. Sio "Maonesho ya zana ya magari" bali ni "Maonesho ya zana za magari"...
ReplyDeleteMdau Seattle, WA.