Mpendwa Michuzi

Mimi ni mdau mkubwa wa blogu ya jamii na leo naomba nitumie fursa unayoitoa ya kuelimisha jamii juu ya mambo mbali mbali. Leo nahitaji ushauri na uzoefu juu ya jambo hili tete.

Mimi ni mzazi 'kijana', watoto wangu wa kuwazaa mwenyewe bado ni wadogo lakini kwa muda wa miaka isiyopungua mi-5 nimekuwa nikiishi na kumsomesha mtoto wa shemeji yangu, dada wa mke wangu. Hivi sasa yuko form 4 na anajiandaa kufanya mitihani muhimu ya kidato cha 4 ambayo huwa namwambia ita-define mwelekeo wa maisha yake kwa kiasi kikubwa sana. 

Mimi pamoja na mke wangu tumeshamshauri na kumsihi sana azingatie masomo na kwamba adui mkubwa sana ambaye anatakiwa kupambana nae ni kujiingiza kwenye mapenzi/ngono katika umri na kipindi hiki. 

Tumekuwa tukitumia kila mbinu mbalimbali kumwepusha na vishawishi ikiwemo kumwonya awaepuka vijana wa mtaani kwetu hasa wale wanaoonyesha dalili za kutaka kumtongoza, asiwe na marafiki wasio na maadili mema, kumfundisha neno la Mungu, kuhakikisha anakuwa nyumbani mapema kabla giza halijaingia, na pia kutomwacha peke yake nyumbani wakati wowote, kutomnunulia simu n.k. 

Anayoyafanya akiwa shule hatuyafahamu isipokuwa tunaamini anaendelea vizuri kwa sababu ni mara moja tu tuliona dalili ya kwenda ndivyo sivyo (alikuja na simu 'ya rafiki yake' nyumbani) na tukamwonya vikali na alionyesha kuelewa, akaomba msamaha na hatujaona tena tatizo hilo au yanayofanana na hayo.

Kwa bahati mbaya sana hivi karibuni majirani wametupa 'breaking news'. Wamemuona binti yetu huyu akitoka 'getto' kwa kijana mmoja mtata pale mtaani. Shahidi aliyeona hili anasema waliingia pale na bodaboda, wakakaa kwa muda, then wakatoka tena wote na ndipo alipoelekea nyumbani. Siku hiyo ilikuwa ni weekend na aliaga kwamba wanakwenda 'project' na wanafunzi wenzake.

Msaada ninaohitaji kutoka kwa wazazi wenzangu wazoefu (mimi na mwenzangu hatujawahi ku-deal na crisis kama hii) na washauri mbalimbali ni kwamba, nimsaidie vipi binti huyu kujiepusha na ngono katika umri huu, zaidi ya tulivyofanya? Hivi katika umri huu, ataepukaje mimba na UKIMWI? Wenzangu wanafanyaje? Huyu kijana wa mtaani nimchukulie hatua gani, nina hasira nae sana!? 

Ninauliza haya kwa sababu najua ni changamoto kwa wazazi wengi. Nimeshasoma case nyingi za mabinti kujiua kwa sababu 'walifokewa na wazazi wao walipogundua wanajihusisha kwenye mapenzi/ngonon na walipowalazimisha kuacha!'. Naogopa sana hili. 

Mke wangu amekasirika sana lakini nimemsihi asimshambulie binti mpaka tuwe wote na tujipe muda wa kutafakari na kuomba ushauri hatua za kuchukua. Natamani sana huyu mtoto asome kwa sababu hali ya wazazi wake ni duni sana, naona elimu ndio mkombozi pekee wa maisha yake.

Naomba kuelimishwa.

Mdau

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 28 mpaka sasa

  1. Poleni sana kwa majukumu mazito ambayo mnayapata. Ushauri wangu mimi kama mzazi ambaye nayo yameshanikuta matatizo kama hayo ni kwamba msichoke kumueleza umuhimu wa yeye kujielewa anatakiwa afanye nini. Kama mambo yakiharibika basi nyinyi kama wazazi mmejitahidi kadiri ya uwezo wenu naye akuelewa basi kosa litakuwa kwake nyinyi sehemu yenu imeshaisha.

    Kutokana na mfumo mzima wa sasa hakuna njia nyingine ya kumzuia mtoto kufanya mambo anayoyataka la msingi kumuomba mungu akusaidie awe msikivu kwenu. Kuhusu huyo kijana hata usiwe na hasira naye maana anaweza akakusababishia kutenda kosa la jinai hapo ndipo utakapoharibu maana hata hao watoto wako wadogo watakosa muelekeo wakati wewe upo jela.

    naomba mwenyezi mungu amfungue huyo shemeji yako awe msikivu kwenu.

    ReplyDelete
  2. Japokua mimi sio mzazi lakini naweza kukushauri kidogo ninavyoweza kufikiri...cha msingi muite tena huyo mtoto kaa naye chini wewe na mkeo halafu mzungumze nae kwa lugha ya kirafiki na mumueleze athari za kujiusisha na uhusiano katika umri mdogo na mumueleze ni jinsi gani akijihusisha na mapenzi katika kipindi hiki anaweza kupata matatizo and then jaribu kumueleza sasa ebu achana na mapenzi kwanza halafu maliza form 4 ukifaulu utayakuta hayo mambo yapo ila msimkaripie kwanza au kumfokea ni hayo tu........http://josephatlukaza.blogspot.com

    ReplyDelete
  3. Kaka, pongezi nyingi sana kwa kumlea mtoto asiye wako kwa juhudi zote hizo, tena kutoka moyoni!
    Mama ake mdogo amwite kirafiki, azungumze naye kirafiki madhara ya kungonoka ujanani, pia amwelimishe kutumia kondom. kwa sababu hata uchunge vipi, lazima watamla tu, kwa hiyo bora wamle ki-usalama.

    ReplyDelete
  4. Watoto wakifika age hiyo huna ujanja ni kumwomba Mungu tu awasaidie. Ila tafadhali musichoke hata kidogo kumpa maelekezo na kumweleza a b c za kushabikia matamanio ya mwili na kuwacha masomo. Mumueleze kinaga ubaga kwamba hata ukifanya nini jamii inamwona na mumpe mfano wa hilo tukio alipokwenda kwa huyo kijana. Mumpe live kwamba mimba na ukimwi siyo vitu vya mchezo ni vya kuharibu maisha na atakuja kujutia hapo mbele akikosa nafasi hii adhimu ya kuendelea na masomo yake sasa.

    TAFADHALI MUSICHOKE HATA KIDOGO KWANI HAPO HAKUNA UJANJA.

    ReplyDelete
  5. JAMBO LA KWANZA HUNA HAJA YA KUMCHUKIYA KIJANA WA KIUME MAANA YEYE KAMSEMESHA NA HUYO BINTI YENU KAKUMBALI MWENYE KWENDA GHETTO SASA UNAHASIRA NAE ZA NINI..?PILI MTOTO WA KIKE ANAPOPATA MDA WAKE NATHANI UNANIFAHAMUNIKISEMA MDA WAKE HUWA TAYARI SIO MTOTO TENA NI MWANAMKE MTOTO NI YULE WAKIKE AMBAYE HAPATI MDA UKIFIKIA MIEZI YAKE ILA KAMA ANA MDA WAKI IKIFIKIA MIEZI BASI HUYO SIO MTOTO NI MWANAMKE NA ASHAKUWA MKUBWA NA NDIO MAANA SASA ANATAKA MWANAMUME WENGI WENU MUNAPENDA KUYAFUMBIA MACHO MAMBO HAYA ILA BINTI AKIFIKIA UMRI WA KUWA NA MDA WAKE KILA MWENZI BASI HUWA TAYARI ANAWASHWAA NA DAWA NI KUKUNWA SASA UNAPOMKATAZA HAKUELEWI MAANA WEWE NA DADA YAKE KILA SIKU MUNAKUNANA VIPI YEYE ASIWE NA WAKUMKUNA..?LAMWISHO NI WEWE KUMULIZA UNATAKA KUSOMA AU UMEMPENDA YULE KIJANA TUKUOZESHE.LA KAMA NDIO BADO MUNATAKA ATI MPAKA AMALIZE MASOMO HAYA KUNA HATARI YA KUTIWA MIMBA KISHA HUYO KIJANA KUSEMA KUWA SIO YEYE ALIYE MTIA MIMBA MUTABAKI KUMLE YEYE NA MTOTO ALIYETUMBUKIZWA TUMBONI MWAKE.

    ReplyDelete
  6. Mimi sio mzazi, lakini unanikumbusha enzi za ujana wangu, nilipokuwa naishi na shangazi, na nilikuwa nipo high school vile vile! walikuwa ni geti kali sana, kila sehemu tunapelekwa kwa gari kutulinda na wanaume, but ukweli ni kwamba na ukali wote huo nilikuwa nikipata mwanya wa dakika tano namaliza yote!! nilichohitaji sio kufungiwa na kufanywa kama mtumwa, nilitaka mlezi anikalishe chini, anipo faida ya hasara zilizopo nje, then aniamini, aniachie uhuru, na kwa vile waliniamini, nisingetaka kuwaangusha, ningekuwa wazi na wao! funzo hapa, mtoto wa kike hafugiki, haswa umri huo! tumieni mbinu nyengine.

    ReplyDelete
  7. Pole sana mzazi, ukisikia ukubwa ndio huo umekuwa sasa na inabidi upambane na kashi kashi za uzazi. Mie mwenyewe na mume wangu tulikuwa na mitihani ya ulezi kama ya kwako, mbaya zaidi sisi watoto tuliokuwa tukiwalea wazazi wao walikuwa wanaona kila tunachokifanya kwa watoto wao kama tunawaonea.

    Inaonekana nyie mna mamlaka yote juu ya huyo binti kwa hiyo cha kufanya sasa hivi ni kukazania kwanza elimu yake kuwa haitetereki, na mumwambie wazi mkiwa wote wawili wewe na mkeo kuwa akifeli hiyo form four, hakuna cha private school, wala computer course sijui kozi ya kushona bali mtamrudisha kijijini kwa wazazi wake akakae huko kwani lengo la yeye kuwepo hapo kwenu ni elimu tu na si vinginevyo. Mimi na mume wangu tulitumia hiyo njia kwa binti aliyekuwa anausumbua ingawa tulipata malalamiko kutoka kwa wazee wake kuwa tunamsimanga lakini ilisaidia sana kwani hapo tayari alikuwa anarudia form two baada ya kufeli na kusoma alikuwa hataki. Ndani ya miezi mitatu tuliona mabadiliko makubwa. Hilo moja.

    Pili wewe na mkeo mwekeni chini mumuulize kuhusu hiyo siku alipokuwa kwa upole na utaratibu. Kisha muulizeni anataka nini kwenye maisha yake, kwani kama hataki kusoma hata mkimlazimishaje haitasaidia. Muulizeni kama anataka kusoma au anataka kuolewa na nyie mko tayari kukubaliana na matakwa yake. Kama anataka kusoma mpeni masharti ya kuishi hapo ndani ya nyumba yenu, na kama hataki kusoma basi njia ipo nyeupe mutamrudisha kijijini alipotoka ili mumchukue mtoto mwingine anayetaka kusoma muje mumuendeleze.

    Mwisho kama mnaona mna hasira kipindi hiki tulieni kwanza mpaka hasira ziishe ili muweze kucommunicate naye. Natumai kwa hayo mtakayomwambia yatamsaidia kumrudisha kwenye mstari kwani umri alionao ndio umri wenyewe huo wa kuhemukwa, mhimizeni kusubiri hayo mapenzi atayakuta mpaka yatamshinda. Na wala msithubutu kwenda kugombana na kijana wa watu you will make a situation worse, nyie kazaneni kutengeneza kwenu ila huyo kijana msg ataipata kupitia kwa huyo binti yenu ambaye alidhani anafanya siri. Na pia mhimizeni binti yenu kumuogopa Mungu zaidi na si kuwaogopa nyinyi kwani hata kama nyinyi hamuoni Mungu anamuona mpaka ndani ya nafsi yake.

    ReplyDelete
  8. Ushauri wangu kwako ni kujaribu kumkagua sehemu zake za siri (Yani sehemu nyeti ) Kila mara uangalie kama bado anachenza , chungwa au limao . Nafikiri itasaidia

    ReplyDelete
  9. Hawa watoto wa siku hizi bwana tamaa zinawaponza. Nafikiri kama anasimu mnyang'anye manake simu kwa kiasi kikubwa kinachangia Kufanya maovu . Alaf uwe na namba ya mwalimu wake umfuatilie kikamilifu ujue mda anaotoka shule na mda anaokwenda shule . Kukiwa na project kama hizo ww unawasiliana na mwalimu tu.

    ReplyDelete
  10. Tatizo liko kwenu nyinyi walezi, approach zenu za ulezi ni 'restrictive, oppressive' na mara nyingi zemethibitishwa they dont work. Kuhusu boyfriend au ngono, yeye ni binaadam na ni natural kuwa na hizo desires. Una option mbili

    Kukubali awe free kuwa na boyfriend na kumfundisha majukumu ya uhusiano pamoja kusoma na madhara yake.

    au

    Kuendelea kuwa mkali wakati hautobadilisha lolote zaidi ya nyinyi kufichwa anachofanya. This is far worse than above.

    Punguza ukali, elewa yeye ni binaadamu na acha kulea kama ulivyolelewa kiukalikali., unaamuaribu huyo kijana kisakolojia.

    Kubali ameshakuwa na anahitaji uhusiano as experience and part of learning and growing up.

    ReplyDelete
  11. Ndugu wala usijihangaishe na hasira si kwa bint wala kijana we kama mzazi mlezi mliisha muelimisha hasara na faida ya kujihusisha na mambo ya mapenzi na huyo ameonja asali saaan mkizidi atawatukana cha kufanya msubirini afanye mtihani kama atakuwa hajapewa ujauzito akimaliza tu hakikisheni karudi kwa wazazi wake hatakama ni duni kiasi gani na matokeo yakitoka mabaya ndio kabisaa fungeni pazia la msaada kwani usitegemee kwa kuwa wanao wadogo umsaidie huyo kwamba hata wakikua atawasaidia kuwaongoza vyema tabia yenyewe ndio hiyo loh tena aondoke kabisa kabla wanao hawajaua tabia yake.Akienda kwao akaona mazingira hayalipi na shule awe amechezea mwenyewe anyoe au asuke kwani tunaona wengi wanachezea nafasi mwisho wa siku wanaishia kuchukia kila mtu kwa uzembe wao wanaoufanya .

    ReplyDelete
  12. Kosa kubwa la kwanza mnalolifanya ni kumdhibiti mnooo kiasi siku akipata upenyo atakula mpaka mifupa. Mmuombe tu Mungu ampe busara na ni vizuri kumpa maadili na kumjulisha kuwa wengi hupata matatizo kwakuwa wanafanya vitu kabla akili hazija pevuka kufikia kiwango cha kuamua mambo sahihi. Mkianza kukasirika na haswa kama ni mzuri mnahatarisha hata maisha yenu kwa presha. Mwekeni awe huru kuwaambia kinachoendelea ili mjue mahali pa kumsaidia, mkikasirika atayafanya hayo kifichoni na mkijua itakuwa mmeshachelewa. Form 4 kesha kuwa mkubwa na anaweza kuwapiga chenga za kiteknolojia msiokote kitu. Kama wenzake wote wana simu kwanini yeye asiwe nayo? kwani wengine wote wenye simu wameharibika, la hasha siyo wote. Degelavita, Bergen, Norway.

    ReplyDelete
  13. Kwanza nikupe pole na vilevile nikupe moyo kwamba hauko peke yako mwenye kukumban na tatizo la aina hiyo, tupo wengi.

    Pili nikuulize huyo binti ana umri gani? Nauliza hivi kwa sababu uzoefu nilio nao ni kwamba kuna umri ambao umepewa jina la "foolish age". Huu ni umri mbaya sana kama msichana ataanza mapenzi akiwa katika huo umri. Huu ni umri ambao msichana anakuwa katika kutamani kujaribu kila kitu kinachomfanye yeye atambulike kama binti. Umri huu unampa binti kiburi hasa pale anapotambua kwamba na yeye ameanza kukubalika kwenye jamii (Yaani anajisikia kuwa kumbe kuna watu wana draw attention kwake). Kwa sababu hiyo binti anakuwa hana rational judgement bali anasukumwa na kutekeleza yale yanayompa kuwa kama anavyojihisi. Kama ni wanaume atajitahidi kuwapa ili asirudi kule alikokuwa (yaani kipindi alichohisi hakuna anayemuona). Katika kipindi hiki, binti huyu anaharibu mipango yake yote ya maisha kwani akili yake inamtuma kufanya jambo amablo faida yake ni ya haraka (kwa tafsiri yake). Wengine huenda na ujinga huu hadi umri fulani wakajitambua kwamba waliharibu na kuamua kuanza upya na kuna wengine wanapotelea huko moja kwa moja. Sasa kama binti yako yupo katika umri huu, jitahidi kumsihi kwa lugha ya upole na kumpa matumaini ya baadae katika maisha yaka kama ataachana na mapenzi. Muelimishe kuwa mapenzi yapo tu atayakuata na atafanya hadi atayachoka lakini kwa sasa atilie mkazo maandalizi ya maisha yake.

    Sasa kama binti atafanikiwa kuvumilia akapiltiliza hiyo foolish age, kua uwezekano akajitambua na kuanza kufanya maamuzi ya kiutu uzima (rational judgement). Na huyu hata akiwa na mwanamume huhitaji kuhofia kwani anajua nini anachokifanya. Kama mzazi unaweza kumzuia tu kwa ajili ya kulinda heshima yake lakini ukweli ni kwamba anao uwezo wa kukutoroka akafanya na asiharibu maisha yake.

    ReplyDelete
  14. POLENI SANA. HATA MIMI NINA CHANGAMOTO KAMA HIYO KWA MTOTO WA MDOGO WANGU WA DARASA LA SABA. YAANI KAMA WALIVYOKUAMBIA WENGINE NI KUKAZA BUTI NIKIWA NA MAANA KWAMBA ENDELEENI KUMUOMBEA SIKU KWA SIKU NA FANYENI IBADA KAMA NINYI NI WAKRISTO AU WAISILAMU MUNGU ANASIKIA MAOMBI. MIMI IMAINE WAKWANGU NIMESHAMKANYA KWAMBA ASITOKE NJE YA GATE ANAPORUDI SHULE AOGE NA ALE KISHA APUMZIKE KIDOGO KISHA ALE NA KUSOMA LAKINI UTAMKUTA ANATOKA NJE GETINI. NIKAWA NANYEMELEA KISIRI SIRI NIKAMKUTA ANAONGEA NA MVULANA WA JIRANI. NIKAMKANYA KWA KUMPIGA NA KUMUINGIZA NDANI, SIKU NYINGINE NIKAMKUTA HIVYO HIVYO. SASA ANA KAMA MWEZI HIVI SIJAAMBIWA AMEONEKANA NJE YA GETI AKIONGEA LABDA WAMEBADILISHA SEHEMU SIJUI LAKINI NIKIMWAMBIA TUOMBE NA TUSOME NENO LA MUNGU WAKATI FULANI ANAKUBALI NA ANATII. SO WE NEED TO BE VERY STRONG KUENDELEA MUWASEMEA TU MUNGU NDIYE MLINZI WAO MKUBWA ENDELEENI KILA SIKU KUKEMEA KATIKA JINA LA YESU ATAMALIZA MASOMO YAKE SALAMA SALMINI NI SHETANI ANAWATIA VISHAWISHI TU SO TUMKEMEE KILA MARA NA KUSEMA NAO WATOTO WETU.
    JIPENI MOYO YAANI NI KAZI KUBWA SANA

    ReplyDelete
  15. Ninamiaka 45 sina mume wala mtoto. Nilipokuwa na umri huo wa huyo binti nilikuwa moto. Ningejua thamani ya mwiliwangu wakati ule nisingemruhusu mwanaume aniingilie. Siyo kuwa nilikuwa na matatizo ya uzazi lakini wanaume niliolala nao wakati mimi ninatafuta mtoto walitumia condoms. Sasa wao wanawatoto na familia mimi ninaishia kulia kwenyemto usiku.

    ReplyDelete
  16. Poleni sana wazazi vijana kwa situation ngumu kama hiyo inayowakumba pili hongereni sana kwa kuwa na moyo wa kutaka kusaidia jamii , esp kuokoa maisha ya huyo binti. hii story yenu imenikumbusha mbali sana enzi zangu zileee nipo form 4, i used to do the same ila sasa mimi ni mwanaume sikuwa binti, mama yangu huwa si muongeaji sana ila siku akifunguka huwa hafichi kitu, she used to give me blank points hadi naogopa,,,,,,,nikapata demu ambaye mom yangu alimpenda sana akawa anakuja home tunachill nasindikiza kwao ila, what she told her ni kwamba angalieni usije ukapata mimba, na alimdirect kwa dada yangu mmoja hivi ili ampe shule on how to solve tatizo hilo ili yasimkute hayo, kwa kweli alifanikiwa kwa asilimai kama 80 hivi, maana tulikuwa poa kabisa na i can say i felt love that tym, tulikuwa tunasoma shule tofauti za boarding so kukutana kwetu esp kimwili haikuwa sana. USHAURI; ongeeni na huyo binti yenu kiunagaubaga juu y amtazamo wote wa maisha yake na umuhimu wa shule in general , jaribuni kuwa karibu nae zaidi na muwe kama marafiki kwake to the extent akiwa na chochote akilini anaweza kuwa free kuwaeleza, pili mchunguzeni huyo kijana ana muelekeo gani wa maisha au ndio wale vijana waharibifu tuu? maana enzi zangu i was doing good at school to the extent that nikawa napendwa kwa akina yule binti coz i raised her performance sana at school. kama kijana ni mwanafunzi pia muelezeni athari ambazo anaweza kuzipata kwa kufanya hivyo, na muwasisitizie kama kweli wanapendana wapeane muda shule iishe kwanza though kuwa marafiki inaruhusiwa msimbane sana , huyo binti mtampa hamu ya kutaka kutoroka kifungo hicho.mwisho salini sana mungu ndio kila kitu hata mfanye nn, yeye tuu ndio anaweza kum keep safe huyo binti. SUMMARY; zingatieni, UWAZI, UPOLE na REAL SITUATION . msema ukweeeefe.

    ReplyDelete
  17. Kwanza Poleni.Mimi nilipata mimba wakati niko nyumbani nangoja matokeo ya form four.Wakati huo mamangu alikua amekufa kwakweli sikua na rafiki zaidi ya boyfriend ambae atlest he helped me wakati wa kile kipindi
    Now,before mama hajafa no matter what a man would say to me,it would not change msimamo wangu.Wazazi wangu walikua wanaongea na sisi very friendly kutuambia mapenzi yapo lakini yana mda.Na kwa upande wa masuala ya umri ni ngumu mtoto kukuelewa wakati hayo ni mahitaji ya mwili na akili pia.
    Ushauri wangu ni kwamba mwiteni,mjulisheni kwamba mnajua alienda geto akatoka mda gani,that way atahisis kila akiwa mishen mtajua then atapunguza spidi na mda utaenda.Kuna wakati tunahisi kwamba watoto wanajua kilakitu,kumbe hapana.Mimi nilijua mimba inaingiaje baada ya kupata.Na mimi nimekulia Dar,nimeattend semina nyingi tu za peer(amref)but they all not that open .Tuwe wawazi kabisa ndio angalau tatizo litapungua

    ReplyDelete
  18. andikeni kwa ufupi wadau,kwani mnatunga kitabu?

    ReplyDelete
  19. mi naona nikumuita mtoto na kumuuliza kama antaka kusoma au anataka mume kwasababu mnaweza kumlazimisha mtoto kusoma kumbe mwenyewe anataka kuolewa so itakuwa ni ngum na kuumiza vichwa vyenui kwa sababu kama kumueleza mmeshamueleza ila hasikii na kama hataki mume anataka kusoma basi hayo mambo mmueleze zaid ayaelewe. na mumuambie kama haina haja kuumizana vichwa na kama kuna siri yoyote awaeleze au kama kuna kitu anachukia pia aseme pengine kumfungia sana mtoto ndio imesababisha hayo au kuna kitu anachukia na kwa vile nyie ni wazazi walezi na anajua kama nyie ndio manemprovide everything usikute anogopa. mengine watu wameshakueleza uamuzi uko kwenu

    ReplyDelete
  20. Pole kwa kazi ya kulea, maisha ya kitanzania ni kusaidiana jamaa wa koo moja. Tatizo lipo kwa watoto wengi wa kulelewa na walezi pia. Hapo umetaja kuwa umemnyang'anya simu au hutaki awe na simu ya mkononi. Hiyo pekee tayari imeshatoa mwanya wa mtoto kuona hapendwi na familia inayomlea. Akienda shule anaona wenziwe wengi wana simu. Pengine akizungumza nao wanamwambia wapenzi wao ndio waliowanunulia. Sasa naye akiwa nyumbani anaona dada yake naye unamwangalia na hata kulea na yeye. Sasa wasichana wengi wanaona akishakuwa mkubwa tu na mzuri wa sura atapata bwana wa kumpatia mahitaji yake yote. Hii inawafanya wasichana wengi wasiwe wasikifu hususan wanapofika miaka ya kukua. Pia hizi TV zimejaa michezo ya mapenzi, watoto wanajifunza tangu wadogo kuwa mpenzi ndie atakayempa kila kitu. Siku hizi hata madume nao wameingia kwenye mchezo huu wanatafuta majimama au wazungu. Kwa ufupi badilisha strategy zako za kulea ukifikiria zaidi unayemlea ameshakuwa na wahitaji yake na malengo yake ni tafauti na wengine.

    ReplyDelete
  21. Pole kwa yote, mimi sina mengi ya kusema bali kukushauri kuwa hakuna binadamu duniyani mwenye akili yake timamu ambae anaweza kuchungikika. Mwanadamu anaweza kuchungika kwa asilimia mia kwa mia labda kama ana ubovu kidogo wa aliki au kimwili... lakini kama yuko sawa na ana hisia kama mwanadamu mwingine kuchungika sio rahisi.

    mimi napata mshangazo sanaa unaposema kwamba mnambania mtoto wenu mpaka simu ya mkononi. Nyie hamuoni kwamba ndio kwanza mnamuweka kwenye vishawishi na tamaa kama marifiki zake wanakuwa walitumia hizo simu.

    Pili, kumchunga nyumbani muda wote na kuhakikisha kuwa anabaki nyumbani na mtu.

    hizo hatua zote mnazo zichukua hazimjengi mtoto wenu na wala hamumuonyeshi kwamba mna "trust" kwake. Binti anaefikia umri huo anajiona kama mtu mzima japokua ni mtoto... na nyie manchopaswa kumfundisha ni masuala yote ya kidunia kama mtu mzima na madhara yake.... yeye mwenyewe atatumia akili yake aliopewa na mungu na kuchambua na kuyakataa... muelezeni kuwa wanaume wapo.... na atakuja kupata mwanaume baadae, ataolewa na kupata wototo na kuwa na familia, lakini muelezeni ukweli mkimpa mifano mbali mbali ya watu mbali mbali.... nyie wenyewe mpaka kuja kuowana utakuta mlipitia vishawishi vingi ambapo pengine vingewa 'cost' maisha yenu kama msinge chukua umakini wowote. Hamna binadamu ambaye anapenda kuharibu maisha yeke.... tatizo ni kwamba watu wanaharibu maisha yao japokuwa wanaelimishwa ni kwasababu wanafikiri kwamba kile kizuri wanacho elimishwa sio ukweli bali ni ndoto za alinacha.... kwahiyo kama ukizungumza na binti huyo kama mtu mzima mwenzenu na kumuambia ukweli wa mambo kwamba dunia unavyo iona kwa macho sio ndivyo ilivyo ... dunia pamoja na wanadamu wake kwa mtazamo mmoja wamejaa "deceiving factors" nyingi na sio kila kitu ukionacho ndivyo kilivyo.

    mpe ukweli wa mambo na wala sio uwongo au kumficha.

    Mwisho, ni kwamba huyo binti anapaswa kuwa rafiki yenu... kwanza umesmema nyie ni wazazi vijana... kahiyo msijifanye kama wazee sana kwasababu mnawatoto... ambao pia ni wadogo sana.... mpeni "trust" huyo binti, na kumuonesha mapenzi yenu kama wazazi... na kama ana shukurani na pia akili yake salama, sijui kama atawaficha kama akimpenda mtu barabarani au nini... atawaambia ukweli na nyie mtamuelimisha.

    ni vibaya sana mtoto akiwa anafanya vitu akificha kwasababu anaweza kufanya vitu vibaya zaidi kwasababu kwanza hajui anafanya nini, pili hajapata uzoefu wowote na hamna mtu aliemwambia. Ukiwa wazi na mtoto wala hana tamaaa... tamaa inakuja pale ambapo anaaambia hiki ni kibaya wakati anaona dunia nzima wanafanya hicho kitu.. iweje yeye asifanye?

    Kumfungia mtoto na kumfichia simu au nini yote hayo hayasaidiii... ni kwanza unamfundisha mtoto tabia ya uwoga amabyo ni mbaya zaidi.. huyo mtoto anaweza akakuwa bila "confidence" yoyote kwasababu amezoea kuficha vitu.

    Badilisheni "style" ya malezi na muwekeni mtoto huru.

    ReplyDelete
  22. kaka poleni,mimi ninae mtoto wa kike lakini bado mdogo,kutokana na uzoefu wa kuona watu wengine wanao patikana na tatizo kama hili na nawengi wao wamefail kurekebisha na mwisho wake wanapata hasara, kwamtazamo wangu haya ni maumbile hauwezi kuyazuhiya kwa vyovyote vile, la msingi ni kumkazanie azingatie masoma ili asiweze kufail vyote,mueleze kuwa ameshakuwa mkubwa,(usimuonee haya),je jamaa anampenda?vilevile huyo jamaa anamfaa, hatakama akiwa na maisha yake je anafaa kuwa mpezi wake!!kama hafai mwambie atafute ambae atamfaa katika maisha yake, na mwenye mawazo kama yake ya shule, mkaribishe jamaa nyumbani,mfahamiene, ili mjomba wako awe free asiwe anatoroka pia mpangie mashariti kwe kuona na jamaa baada yakumaliza kazi zote za shule, ukijaribu hilo nazani litakufaa, kwani sio kila wakati ni wakati wa mapenzi ikiwa wakiwa free,kumbuka wewe mwenyewe ulipo kuwa na umri huo.

    ReplyDelete
  23. mabinti wana vichwa vibovu hawaelewi unafanya hivyo kwa faida ya nani,mwache kama umefanya part yako, akamilishe yake naye kwa kutiwa hasara, mara nyingine tunakua hatupendi lakini kuna watu wengi hawataki kujifunza kwa makosa ya wengine, watu hawa hujifunza kwa makosa yao wenyewe, usihofu jali yako sasa maana kila mtu ana zigo lake. kuongea imetosha.

    ReplyDelete
  24. watu wengine hawaendi kwa upole hata kidogo ,kuna watu upole unawarekebisha na kuna watu mpaka uwe harsh ndio aelewe msome huyo kicheche then sisemi uwe mpole, do what you got to do! hata kwa kuchapa. mabinti ni crazy hata wenyewe wanajijua, mmoja hapo juu anasema alikua napelekwa na gari kila sehemu lkn alikua akipata dk tano anatoroka, mpuuzi sana sasa hizo dakika tano za ujinga wako zimekupa faida gani? yani pamoja na kuwa walikua wanakulinda kwa faida yako mpaka sasa hivi umekua mtu mzima bado unaona ni ujanja ulichokifanya, mi nadhan kama ungeeelimisha wanaotoroka kuwa wazazi wanafanya hivo kwa kukulinda ili badae upate maisha yako mazuri na sio kukuchukia, kwa hiyo uwafundishe kuwa ulifanya hivo kwasbb ulikua huna akili, teenagers ni watu tofauti kwa wale mnaowachukulia kama watu wazima mnawaharibu. wadau mnaniboa sa zingine.

    ReplyDelete
  25. Pole sana mdau. Mimi ni baba wa watoto 3 wa kike ambao wote wamevuka miaka 16.Na mara nyingi nimekuwa karibu sana na kuwa rafiki yao wa karibu mno zaidi ya kuwa mzazi/baba yao.Nimetumia mbinu hii ili iwe rahisi sana kushare nao mambo mbalimbali ya kielimu na kuwafanya wasiniogope bali wanione ni baba mwenye upendo kwao na ninayehitaji kuona maendeleo yao mema.

    Njia hii imenirahisishia uongea nao very frankly bila kuogopa hata kutaja mambo mengine kwa maneno yake makali, njia hii imefanya niwe nashauriana nao, na kwa sababu mimi ni msomi huwa najiingiza kabisa hata kukagua kazi zao za shule/chuo na kuanza kuwafundisha mambo mengi ambayo najua waalimu wao hawawafundishi hasa kulingana na jinsi ninavyowatathimini.Ninanawajribu kuwaeleza na kuwataja wanawake wengi ambao wamefanikiwa, na hata wengine ambao wanawajua na waliwajua kabla ya kufika hapo walipo na kuwapa matumaini makubwa jinsi ambavyo Mungu amewapangia katika maisha kama hawataharibu maisha yao kwa kukimbilia mambo ya kuchezea miili yao.

    Kusema ukweli sijapata nafasi ya kuwafungia,kwa sababu najua nimewapa elimu ya kutosha, na ni juu yao kujichunga.Ninachoweza kukuambia ndugu mleta maada ni kwamba upendo uwe mkubwa zaidi katika maelekezi yenu yote.Msimfanye huyo mtoto sawa na watoto wenu wadogo.Mfanye rafiki yenu mkubwa zaidi ya kujisikia kuwa mnamsomesha au mnampa hiki na kile.Mkiwa karibu sana naye bila kumpa masimango mtafaulu kumfanya ajisikie na aone fahari ya malezi yenu kuliko kumtenga mbali na hasira na maelekezo ya kumkemea.Jinamizi la mapenzi likiingia litamchota zaidi kwa sababu siku akipata mwanya atafanya mapenzi hadi achubuke.Ni vema kumpa uhuru wa kiasi ule unaomfanya ajisikie kuwa na yeye ni binadamu mwenye haki fulani katika maisha na maamuzi yake fulani.

    wazazi/walezi ni waongozaji tu na wala hatuwezi kutibu maugonjwa ya uhuni kwa ukali au kwa kiboko,bali tunaweza kutumia njia ya mahusiano mazuri na watoto wetu.hata akifanya mapenzi lakini anakuwa anajua kuchukua tahadhari nyingi kwa uangalifu mno kuliko ule wa kumsinikiza na gate huo ni mbaya maana atakapopata mwanya atasahau kuchukua tahadhali yoyote na uangalifu wowote zaidi ya kutamani kukidhi haja yake kwa muda mfupi ule.Muombee sana mungu amlinde.

    ReplyDelete
  26. Mimi ningekushauri mumwite huyo binti muendelee kumuelimisha madhara ya kufanya mapenzi. Cha zaidi huyo dada yake aongee naye pembeni kuhusu safe days, Amuelimishe umuhimu wa kutumia condom kwamba inasaidia kuzuia mimba na magonjwa pia. Ampatie links na vitabu kama evidence. Awe mkweli kuhusu mimba inaingia vipi na jinsi inavyobadilisha maisha ya mtu for good.

    Hii ni kwa sababu ili ajue mwenyewe kwamba anapoamua kulala na boyfriend basi either atapata mimba siku hiyo au la. Na asiwe na excuse ya kusema hakujua from the get go.
    Akhsante, Mama H.

    ReplyDelete
  27. KULEA NI KAZI KUBWA NI JUKUMU LA KUKABILIANA NALO.KWANZA WASICHANA HAWA WANATAKIWA KUANGALIWA KWAMAMBO MENGI.
    1-JARIBU KUANGALIA MARAFIKI ALIONAO INAWEZEKANA NI VISHAWISHI KUTOKA KWA MARAFIKI.
    2-JARIBU KUKATAZA WASIANGALIE CINEMA ZISIZO NA ADABU KWA SABABU CINEMA NI KIVUTIO KIKUBWA NA KISHAWISHI CHA MAMBO MENGI.NA UWATAFUTIE MICHEZO YENYE KUFUNZA.KAMA UTAGUNDUA MICHEZO YETU YA BONGO KWAKWELI HAZINA ADABU HATA KIDOGO KUWA MAKINI KWA HILO.
    3-TAFUTENI MUDA KILA WIKI KWA AJILI YA KIFAMILIA KWA KUTEMBELEA NDUGU NA JAMAA NA IWE SIKU YA KWENDA KUTEMBEA SEHEMU NZURI SIO IWE LAZIMA YA KULIPIA MNAWEZA HATA MKAJICHUKULIA CHAKULA CHENU KAMA NI BEACH.AMA KAMA MNALO SHAMBA PIA NI JAMBO LA KUJIFUNZA MENGI.
    4-INABIDI VILEVILE KUWA MKWELI KTK MASUALA YA KIMAPENZI ILI KUMUELEZA MADHARA YA BAADAE.PIA JARIBU KUMSHAWISHI YAKUWA VIJANA HAO NI WAHARIBIFU NA HAWATAKI MAENDELEO YAKE.UNAWEZA UKAMTAFUTIA MIFANO MINGI HATA KTK MOVIE AMBAZO ZINAELEZA MAISHA KAMA YAKE.
    5-JARIBU KUMSAIDIA KTK KUTAFUTA KITU AMBACHO ANAKIFIKIRIA KUKIFANYA KTK FUTURE YAKE.NA VILEVILE MJARIBU KUMUEKEA HESHIMA YAKE KWA KUONGEA NAE KWA SAUTI YA CHINI KULIKO KUM-BWATUKIA KWASABABU NI KITU KINAWEZA KUMSUMBUA KTK BRAIN YAKE NA KUSABABISHA KUTOKUWA NA CHOICE NZURI YA KIMAISHA NA BAADAE AKAANGUKIA KTK MAKUNDI MABAYA KAMA ILIVO SASA.
    6-BILA YA KUMSAHAU MWENYEZIMUNGU NA KUMUELEKEZA MAMBO YALIYOKATAZWA KTK DINI ILI AINGIWE NA UOGA KWA KUMUOGOPA MWENYEZI MUNGU.

    ReplyDelete
  28. Nimefurahi na majibu mengi yaliyotoloewa na wadau leo. Great advice! Hasa kwenye mambo ya kuongea na binti kama binadamu/mtu mzima mwenye akili ya kufahamu zuri na baya, na si kama mnyama. Mambo ya geti kali au kuchungwa yamepitwa na wakati! Hata mbuzi akikata kama na akaona geti wazi si atatoroka, au? Sasa inabidi muongee na huyu binti kwa upole, ongeeni kuhusu hatari za ngono e.g. mimba, UKIMWI, na kama mnaona aibu mpeni hata vitabu vya kusoma. She is maturing and she is not a child anymore. Wanaosema omba mungu, mungu ameshawapa akili wote (wewe, mkeo, binti). Tumieni akili kusuluhisha hili tatizo, na pia kumbukeni nyie mlivokuwa na umri wake.

    And for Anyonymous 6:50pm: Kumbuka kwamba ingawa umezaa mtoto haimaanishi kwamba wanaishi maisha yao kwa ajili yako. They are individuals with their own urges, wants, desires, goals, and brains. Sio kila kitu wanachokifanya ni kwa ajili yako. It sounds like you have had a negative experience with the females in your life..but maybe it is because of your negative attitude towards them. All sexes are equal. Talk to your children and mold them into the fine adults they are destined to be!

    From experience, kama binti anataka kuongea na mvulana au vice versa, atapata njia. Ask me! Hata sisi tulikuwa hatuna simu za mkononi , but you make it happen. My mama gave me 'the talk' so I could never do anything stupid because I KNEW what could happen if I ever got pregnant. Knowledge is key. Knowledge gives you the power to make the best decisions.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...