Kufuatia ajali ya Meli ya Mv. Spice Islanders, iliyotokea Jumamosi ya tarehe 10 Septemba 2011 katika pwani ya Nungwi Zanzibar, Ubalozi wa Tanzania London Uingereza, kwa majonzi makubwa unaungana na watanzania kutoa pole kwa wafiwa na majeruhi wa ajali hiyo.
Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, kuamuru siku tatu za maombolezi ya Taifa, Bendera ya Taifa katika ofisi za Ubalozi na katika makazi ya Balozi zimeshushwa nusu mlingoti kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 13 Septemba 2011.
Aidha Ubalozi utafungua kitabu cha rambirambi kuanzia tarehe 13 Septemba 2011 hadi tarehe 16 Septemba 2011 kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00 jioni. Jumamosi ya tarehe 17 Septemba 2011, Ubalozi utakuwa wazi kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana ili kutoa fursa kwa watanzania na watu wengineo ambao kwa sababu moja au nyingine watashindwa kufika Ubalozini siku za kazi kwa ajili ya kutoa salamu zao za rambi rambi.
Vilivile Balozi Peter.A.Kallaghe kwa niaba ya wafanyakazi wa Ubalozi na Watanzania waishio nchini Uingereza ametuma salamu za rambi rambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya M. Kikwete, na pia kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein kufuatia msiba huu mkubwa uliolipata Taifa letu.
Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.
Ubalozi wa Tanzania- London
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...