WAUZAJI TIKETI YANGA v AZAM

Mmoja wa wauzaji tiketi kwenye mechi ya Azam na Yanga iliyochezwa Septemba 18 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Seleman Masoud aliripoti kupotelewa kitabu kimoja cha tiketi mara baada ya ugawaji wa vitabu hivyo kwa wauzaji kufanyika asubuhi ya siku ya mchezo kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Tiketi kutoka kwenye kitabu hicho ziliuzwa kwa mashabiki ambao walikamatwa. Walitakiwa kuonesha mahali ambapo wameuziwa tiketi hizo ambapo walionesha kwa muuzaji mwingine Salum Abdallah. Abdallah pia alikuwa mmoja wa wauzaji tiketi katika mechi hiyo.

Wauzaji wote wawili walikamatwa na TFF na tukio kuripotiwa Kituo cha Polisi Chang’ombe. Tukio hilo lilifunguliwa jalada namba CHA/IR/6257/2011 ambapo watuhumiwa wameshachukuliwa maelezo yao. Kitabu kilichoibwa kilikuwa na tiketi 100 zenye thamani ya sh. 300,000. Thamani ya kila tiketi ni sh. 3,000.

POULSEN KUTAJA TIMU SEPT 26

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen anatarajia Septemba 26 mwaka kutaja wachezaji watakaoingia kambini kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Oktoba 9 mwaka huu jijini Casablanca.

Timu inatarajia kuingia kambini Septemba 28 mwaka huu, na inatarajia kuondoka Oktoba 6 mwaka huu kwenda Casablanca. Mechi hiyo ni ya mwisho hatua ya makundi kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Equatoria Guinea na Gabon.

Poulsen ambaye pia ni Mkufunzi wa Makocha wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) yuko nchini Gambia ambapo anaendesha kozi ya wakufunzi na anatarajia kurejea nchini Septemba 24 mwaka huu.


LIGI DARAJA LA KWANZA

Ligi Daraja la Kwanza inayoshirikisha timu 18 inatarajia kuanza mwezi ujao. Kamati ya Mashindano inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Ramadhan Nassib inatarajia kukutana Septemba 24 mwaka huu kuangalia mambo mbalimbali ya ligi hiyo.

Moja ya mambo ambayo kamati hiyo itafanya ni kupitisha tarehe ya kuanza ligi hiyo pamoja na vituo.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. TFF ifutiliwe mbali, hakuna maendeleo yoyote inayoleta zaidi ya vioja na aibu kwa taifa. Itapendeza kama mtu atafanya tathmini ya kina ya nini ambacho TFF wamefanya tokea kuanzishwa kwake ukilinganisha na nini ambacho walipaswa wawe wameshafanya. I'm ashamed of you. Pia nitafurahi kama taarifa za ukaguzi wa hesabu zenu zikiwekwa hadharani (japo ni suala dogo katika kukatishwa kwangu tamaa na TFF).

    Mzalendo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...