Ndugu zangu,
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha muda huu kuwa na nguvu za kukaa katika kiti na kuweza kuandika haya machache kwenu. Nawashukuru sana Wanamabadiliko kwa salaam zenu nyingi za pole mara mliposikia ninaumwa na kulazwa hospitalini. Najua hamkuwa na taarifa kamili za kuumwa kwangu na kwa kweli suala la kuumwa ni suala la mtu binafsi (hata kwa mtu mwenye dhamana ya kiuongozi wa umma japo umma nao una haki ya kujua kinachomsibu kiongozi husika).
 Mwanzo
Nilianza kupatwa na maumivu ya kichwa usiku wa siku ya Ijumaa tarehe 20 jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili kutoka Jimboni tayari kwa kazi za Kamati za Bunge ambapo Kamati yangu ilikuwa imekwishaanza kazi wiki hiyo kwa kupitia mahesabu na utendaji wa Mamlaka za Maji nchini. Kama kawaida yangu niliona maumivu hayo makali kama ni sehemu tu ya uchovu wa ziara za Jimboni na safari za mara kwa mara nilizofanya kuinigilia ziara za Jimboni ikiwemo kuhudhuria Mdahalo wa Umeme na Mkutano wa Uwekezaji Kanda ya Ziwa Tanganyika. Hivyo nililala na nilipoamka kichwa kilikuwa kimepona na hivyo nikahudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma katika Ofisi ya Bunge mpaka saa saba mchana.

Siku ya Jumapili saa kumi na moja jioni nikiwa katika Hoteli ya Southernsun nilipatwa na homa kali ghafla. Nilikatisha mkutano niliokuwa nao na kuamua kurejea nyumbani, lakini nilishindwa kuendesha gari na hivyo kumwomba Dereva wa Mhe. Mhonga anifuate ili anisadie kunifikisha nyumbani. Nilipofika nyumbani kwangu Tabata, homa ilizidi kupanda na hivyo kuamua kwenda Hospitali mara moja. Nikapelekwa Agakhan Hospital na nikapata huduma. Nilipochukuliwa vipimo ilionekana sina malaria wala homa ya matumbo na pia hawakuweza kuona sababu ya homa ile namna ile (maana ilifikia degree 40). 
Walituliza homa, nikapewa Panadol na baadaye nikaruhusiwa kurudi nyumbani mnamo saa tano usiku. Nilipoamka siku ya Jumatatu nikaenda kazini kuongoza Kikao cha Kamati ya Bunge ambapo tulikuwa tunashughulikia Hesabu za Bodi ya Utalii na Benki ya Posta Tanzania. Nilipita Agakhan kupata majibu ya ziada na kuambiwa nipo sawa ila nipumzike nisifanye kazi kwa siku kadhaa na nitakuwa sawa.

Hali kubadilika
Siku ya Jumanne niliamka nikiwa salama, kichwa kikiuma kwa mbali lakini sio vya kutisha. Nikawajulisha wajumbe wenzangu wa kamati kuwa sitakwenda kazini na wao waendelee na kazi. Hata hivyo ilipofika saa sita kamili nilianza kutetemeka mwili mzima na homa kuwa kali sana huku kicha kikiniuma sana sana sana! Dada zangu wakamwita Driver na kunikimbiza Hospitali ya Agakhan. Wakarejea vipimo vilevile na matokeo yakawa yaleyale. Joto lilifika degree 39.8 Hivyo wakanipa dawa za kupoza homa na maumivu ya kichwa kwa drips na sindano kadhaa. Siku ya pili hospitalini nikafanya vipimo zaidi ikiwemo ultra sound na vyote kuonekana sina tatizo lolote. Niliendelea kuwepo Hospitali na kwa kweli hali ilikuwa inatia moyo sana kwani nilipata nguvu na hata kuweza kuzungumza, homa ilikuwa imepungua sana. Pamoja na kwamba Mganga Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Waziri wa Masuala ya Bunge na Daktari wangu binafsi kuwataka waangalie upya vipimo vya malaria, madaktari wa Agakhan waliwahakikishia viongozi hawa na Daktari wangu kwamba hawajaona Malaria na hivyo wanaendelea na uchunguzi wa 'a trigger' ya homa kali niliyokuwa napata.

Hali kuwa Mbaya
Usiku wa siku ya Jumatano Hali ilikuwa mbaya sana. Joto lilipanda tena kufikia 40 na kichwa kuuma zaidi. Nilikuwa kama ninatwangwa kwenye kinu kwa kweli. Nilikuwa natetemeka sana. Ilikuwa taharuki kubwa sana katika chumba nilicholazwa. Wageni waliokuwa wamekuja kunijulia hali wakati hali inabadilika ilikuwa ni pamoja na Ndugu Murtaza Mangungu na Mohamad Chombo ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya POAC, walishauri mara moja nihamishwe Hospitali kupelekwa Muhimbili. Muda si mrefu kupita Waziri Lukuvi na Katibu wa Bunge walifika, wakaafiki na nikahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwa hali niliyokuwa nayo nikalazwa katika Chumba wanachokiita Mini-ICU. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mama Blandina Nyoni alikuwepo Hospitalini tayari.

Usiku huo huo nilifanyiwa vipimo upya. Full Blood picture pamoja na BS. Vile vile kufuatia malalamiko kuhusu maumivu ya kichwa ikaamuliwa kuwa nifanyiwe CT Scan usiku ule. Ikaonekana nina wadudu wa Malaria 150 na mara moja nikaanza matibabu. Namshukuru sana Daktari kijana Dkt. Juma Mfinanga kwa umahiri mkubwa aliouonyesha tangu nilipofika pale Mini ICU. Asubuhi ya siku ya pili nikapata majibu ya tatizo la maumivu ya kichwa. Nimekuwa nasumbuliwa na kichwa kwa miaka zaidi ya Kumi sasa na katika kipindi hicho mara nne nilipoteza fahamu na kuanguka (Mara ya kwanza mwaka 2000 nikiwa Jijini Mwanza nikielekea kwenye Mkutano wa Vijana wa National Youth Forum, Mara Pili Mjini Dodoma katika mkutano kama huo mwaka 2001 lakini ilikuwa usiku,Mara ya tatu Nikiwa chumbani, Hall II mara baada ya kutoka  Prep, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2002 na mara ya Nne Bungeni siku ya kupitisha Muswada wa Madini 2010 kufuatia wiki nzima ya Kamati na Mjadala wa Bunge(Ndugu Katulanda anakumbuka siku hii kwani yeye ndiye niliyemkamata njiani kunikimbiza Zahanati ya Bunge).

Tatizo lililogundulika ni SINUSITIS, ambayo tayari imekuwa sugu. Daktari Bingwa wa magonjwa haya Dkt. Kimaryo akanieleza kwa kirefu juu ya tatizo hili na kuniambia suluhisho ni 'surgery' na pale Hospitali ya Taifa hawafanyi hiyo operesheni. Akashauri niletwe India ambapo kuna Daktari mpasuaji wa ugonjwa huu. Nikakubali.

Baada ya kuwa Malaria imedhibitiwa kwa kufikia nusu ya 'dozi' nilopewa na wadudu kuonekana kutokomea, Ofisi ya Bunge ikaandaa safari. Nimefika India. Nimebakiza sindano mbili ili kumaliza 'dozi' hiyo na tayari nimefanyiwa taratibu zote kwa ajili ya 'surgery' hiyo.

Sijafa
Uvumi ulienezwa nimekufa. Kwa kupitia kwenu ndugu zangu WanaMabadiliko, napenda Watanzania wenzangu wajue mimi ni mzima wa Afya. Nimepata maradhi kama Binadamu mwingine yeyote anavyoweza kupata na namshukuru Mungu kwamba ninapata matibabu mazuri kabisa.

Shukrani
Nawashukuru sana Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili chini ya Prof, Mwafongo kwa juhudi kubwa walioonyesha katika kunihudumia.Naishukuru Ofisi ya Bunge kwa Kutimiza wajibu wao kwangu kama Mbunge,Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kwa kuonyesha upendo wa hali ya juu na watumishi wote wa Wizara ya Afya, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Slaa kwa ufuatiliaji wa karibu wa Afya ya Naibu wake, Wabunge wajumbe wa Kamati ya POAC, Dkt. Alex Kitumo,ndugu, jamaa na marafiki zangu wote.Nawapa pole wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa uvumilivu mkubwa hasa kufuatia uvumi mbalimbali ulioenezwa, pia Watanzania wengine kwa uzito huo huo.

Nitawajulisha kwa lolote Mungu akipenda. Ninaendelea na matibabu na hali yangu ni nzuri
Ndugu yenu

Zitto
--
Kabwe Z. Zitto,MP- Kigoma North, Tanzania.
Chairman Parliamentary Public Investments Accounts Committee (POAC),
Deputy Secretary General CHADEMA and Deputy Leader of the Opposition,
Shadow Minister of Finance
Mobile:             +255756809535      
Blog: www.zittokabwe.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 27 mpaka sasa

  1. pole sana kaka ,Insh Allah utapata nafuu. by .mjuvi

    ReplyDelete
  2. Ndugu Zitto,

    Kwanza pole sana na maradhi yaliyokukuta, kwa rehma zake Allah, atakusaidia. AMin,

    Pili, binafsi sijawahi kusikia kufanyiwa operesheni kwa mtu aliyekua diagnosed with SINUSITIS, naomba usifanye maamuzi ya haraka haraka, mpaka upate background check ya hao madokta na je wamekua successfully vipi juu ya hili.

    Huku ulaya zipo dawa nyingi za kutuliza maumivu ya SINUSITIS, lakini jambo la kufurahisha zaidi, next time kama ukipata hilo tena au kwa wale wagonjwa wa haya maradhi.. TAFUNA CHEMBE MOJA YA KITUNGUU THAUMU...maumivu yanaondoka haraka sana...

    ReplyDelete
  3. florian rweyemamuOctober 30, 2011

    mwanamabadiliko huyu katika nyanja zote. siyo kisiasa tu bali pia katika mapokeo yetu waaafrika katika masuala ya afya. Siyo kawaida kwa siye waafrika mtu kuuuelezea umma kuhusu afya yake. Asante Zito. umeonyesha kupevuka kwa kiasi kikubwa. POLE.

    florian rweyemamu

    ReplyDelete
  4. Muhimbili oyee! Kule kwingine hata mimi huwa hawavioni vijidudu vya malaria ila nikienda hata dispensary za vichochoroni nashangaa wanaviona na ninapona baada ya kutumia dawa.

    Pole Zitto na tunakuombea afya njema! Kama vipi lianzishe huko huko maana quorum imetimia :-)

    ReplyDelete
  5. TUnashukuru Zitto kwa maelezo yako,kama siyo kushtuka na kuwa mtu wa watu,hakika ulikuwa unakufa.Maana Malaria peke yake ingekuondoa na huku ukiwa na imani uko Hospital kubwa na wamekosa wadudu.Na hivi ni mtu wa Kigoma,hapo Mashehe wangekusanyika na kuanza kupunga pepo kumbe unaumwa ugonjwa wa hospital.
    Tumejifunza mengi kwa mda mfupi kupitia maelezo yako na afya yako kwa ujumla.
    Mungu akutangulie kaka na mbunge wangu.
    Ni mimi Mzaliwa na mwanahi wa Kigoma Kasikazini.

    ReplyDelete
  6. We love you Zitto, tunakutegemea na tunakuamini. Tumekosa amani juu ya afya yako ila tumefarijika kwa maelezo yako mwenyewe. Mungu akusaidie upone haraka ili uendelee na majukumu yako ya kuipigania nchi yetu. Mdau Scandnavian

    ReplyDelete
  7. hizi hospitali majina hizi sina hamu pale trauma senta masaki bure kabisa nusu waniulie mtu, malaria imepanda hadi kichwani na homa kali wao wanadai ati ni uchovu na hapo hapo tumempima mgonjwa malaria kwa dola mia ati hamna kitu, eboo usiku wa manane nusu mgonjwa avute kimbiza tmj looo walikuta vijidudu vya kumwaga wakaanza kushusha homa kwanza yakafuataia madrip ya kufa mtu. hizi agakani sijui nini hamna kitu kabsaaaa THANK YOU DR KAPITENI WA TMJ YOU R THE BEST!!!!

    ReplyDelete
  8. wamekuroga hao , yatawashinda

    ReplyDelete
  9. Kuna kitu kinanishangaza mara nyingi hawa jamaa wa pale karibu na baharini na wenzao walio katikati ya mitaa ya indiragandhi huwa hawaoni vidudu vya malaria lakini ukienda hata vidispensary uchwara vya uchochoroni dakika chache tu tayari washanyaka vidudu kadhaa vya malaria je hawa jamaa wana tatizo gani? nakumbuka siku za nyuma kidogo tupoteze mtu kwa malaria walilala naye tu wodini wanazungula na kumtoboatoaboa mgonjwa na masindano lakini hawaoni malaria baada ya kumhamisha mgonjwa kumpeleka kwingine ilikuwa maajabu wadudu kibaaao na akasalimika. sasa sijuwi ni nini tu

    ReplyDelete
  10. Pole sana Kaka Zitto.upo hospitali moja na wagonjwa wengine viongozi wetu waliopelekwa huko?Kama ni ndiyo vipi hali zao?Tunaomba nao kama wanaweza kuandika watufahamishe hali zao.Mungu awasaidie mpone haraka

    David V

    ReplyDelete
  11. Mheshimiwa Zitto pole na nakutakia Mwenyezi Mungu akupe afueni. Asante sana kwa kutupa maelezo haya kwa kirefu kwani mimi nimejiuliza swali moja tuu hapa, sasa viongozi mnakimbizwa India kwa matibabu kwa sababu HOSPITALI KUU YA TAIFA YA NCHI haina uwezo wa kutoa SINUTISIS !!!!! Hii ni minor surgery ambayo binti yangu wa miaka 9 alifanyiwa alipokuwa na umti wa miaka 7 unusu tuu hapa na haikuchukua hata saa moja. Na kwa kweli kuumwa kichwa ilikuwa si moja ya dalili zake labda kwa kua yeye ni mtoto na hana stress za maisha sijui. Anyway SWALI langu la msingi ni JE KAMA hospitali kuu ya NCHi haina uwezo wa kufanya hata some of the minor surgeries sawa viongozi mna uwezo wa kupelekwa india ili kuokoa maisha yenu na kwa mwanamnchi wa kawaida ndio inakuwaje ??? ndio mnatuacha tufe si ndio ?? OMBI langu ni kwamba Mheshimiwa Mungu akujaalie upate Afueni na naomba ukaliangalie hili huko Bungeni ulifikishe kwani najua wewe ni mmoja wa wenye kuthubutu ! MAM

    ReplyDelete
  12. Get well soon Kamanda Zitto.

    Mmmh Aga Khan wamechemsha!

    ReplyDelete
  13. Tusiokuwa na uwezo na wadhifa tutapelekwa na nani India?

    ReplyDelete
  14. Mh. Zitto;
    Watu wengi wapenda amani walikuwa wamesikitishwa na hali yako ya ugonjwa. Tunashukuru umekuwa jasiri na kuuelezea umma kwa kirefu kuhusu unavyoendelea na matibabu.
    Bila shaka juhudi zinazoendelea zitaweza kutibu tatizo lako na kukurejeshea afya njema kabisa.
    Mungu awawezeshe madaktari huko India na kukuponyesha kabisa na tatizo hilo.
    Tunakutakia kupona haraka!!
    Kisarika

    ReplyDelete
  15. Hivi hata malaria na mafua siku hizi tunapeleka nje! Walalahoi tufe tu! Mungu ibariki nchi yetu!

    ReplyDelete
  16. Binafsi nimekuamini kuwa wewe ni mtu shupavu si wote wanao diriki kusema ukweli au kuuelezea umma juu ya miili yao, i love it, inaonekana ni jinsi gani utatuambia ukweli kuhusu nchi tukikuchagua kuwa rais wetu 2015. Vijidudu 150 kutokuonekana Aghakan ni maajabu kwani ni vingi. But we thank God and doctors for erything they done to get you back.
    Praise God and let us thank God together no matter who you are.

    ReplyDelete
  17. Pole rafiki Zito na inshaallah Allah atakupa afya njema ili uweze kuendeleza mapambano ya kuleta maendeleo.

    Pili napenda kuwapongeza sana madaktari wa muhimbili kwa kazi safi na kuonyesha uweledi. Na hili liwe fundisho kwa wengine kuwa na sisi tunaweza.

    Tatu sasa niwakati muafaka kwa kuwawezesha, kuwaamini na kuwapa fursa ya kutumia uweledi wao katika kutuhudumia naamaini tunaweza sana.

    Nne ninachukizwa sana na tabia ya viongozi kuingilia maamuzi ya wataalamu na hali ya viongozi wa juu kama katibu mkuu kwenda hospitali kwa sababu fulani anaumwa maana hii inaonyesha kuwa mifumo yetu haifanyi kazi au watendaji wanahitaji kusimamiwa kama nyapara hili nachukia sana sana tuamimini wataalamu wetu

    ReplyDelete
  18. Pona haraka ndugu yetu. Mchango wako unahitajika sana tukiingia Ikulu

    ReplyDelete
  19. Tusikimbilie kuwalaum agakhan, labda ni bahati mbaya, mie mwaka jana nililazwa pale na waligundua tatizo kubwa nililokuwa nalo la uvimbe kati ya uti wa mgongo na koromeo kama sijakosea kiswahili (trauma between spinal cod and throat) na niwao walishauri nipelekwe muhimbili kitengo cha Moi ambao ndio walinifanyia upasuaji (Thanks to Prof Kahamba). Agakhan siwabaya kihivyo wanamazuri yao pia.

    ReplyDelete
  20. Yes, you can do surgery to clean and drain the sinuses, especially in patients whose symptoms fail to go away after 3 months, despite medical treatment, or in patients who have more than two or three episodes of acute sinusitis each year.

    Also, most fungal sinus infections require surgery.

    Feel better mpiganaji!

    ReplyDelete
  21. Kwa kweli inatisha kuwa na hospitali ambazo ni useless. Agakhan pamoja na kuwa ni very expensive hospital lakini huduma zake ni questionable. Mtu ana vijidudu 150 na bado hawaoni kitu??? Can they explain this?? Inakuwaje? Pole mheshimiwa wetu.

    ReplyDelete
  22. Angekuwa mtu wa kawaida tayari angekuwa ameshafariki. Sasa mtu malaria ipoo kibao halafu vipimo vinaonyesha hakuna?? Yaani hii hospitali ni ya kufungiwa kabisa. Afadhali umetoa maelezo mheshiwa manake watu wangeanza ohh sumu mara kapigwa kipapai.

    ReplyDelete
  23. MUNGU YU MWEMA

    ReplyDelete
  24. Bwana Mungu apewe sifa kwa kuendelea kumpa afya njema Mhe. MP Zitto Kabwe. Tunakuombea sana Mhe. kwani wewe ni mkombozi wa watu waliokwishaonewa sana, kudhalilishwa sana na kupuuzwa sana ndani ya nchi yao wenyewe.

    Ninaamini, kama unavyoamini wewe Mhe. kuwa ni ugonjwa wa kawaida na si vinginevyo. Ila endapo kuna mkono wa mtu, WASHINDWE KWA JINA LA YESU!

    ReplyDelete
  25. Kazi kwenu mnaokimbilia Aghakhan watu wengi sana wameshalalamika kuhusu hiyo hospitali hawako vizuri kabisa kwa upande wa malaria ugonjwa ambao ndio unaoongeza kwa kuua kuliko hata ukimwi. It's about time Aghakhan you do something about it.

    Kaka Zito nakupa pole na upone haraka pia usiwe mwoga kucheki afya yako mara kwa mara hasa kujua chanzo cha hiyo sinus.

    ReplyDelete
  26. Pole Mheshimiwa, ukipona ni vyema ukafuatilia kwanini Agha Khan hawakiona malaria naamini watu wegni wameshakufa Agha khan kwa tatizo kama lako la malaria kutoonekana na ni tatizo la muda mrefu kwa hiyo hospitali ni wauaji hao wanagharama kubwa lakini hamna kitu nafikiri wakati muhafaka kwa serikali kuingilia kati suala malaria ktk hospital ya agha khan kwani mimi ni muhanga nimempoteza mtu muhimu sana katika maisha yangu hapo Agha Khan tulimpeleka homa ilikuwa inapanda na walikuwa hawaoni malaria ghafla hali ilibadilika kupelekwa ICU saa tisa mchana wakati tuanafikira kumpeleka muhimbili kesho yake asubuhi akafariki.

    ReplyDelete
  27. Jumatatu ya tarehe 24/10/2011 nilipandwa na homa kali sana usiku wa manane nikakimbizwa Aga Khan! Usiku ule ule wakanipa kitanda na kuchukua vipimo vyote huku wakinipa dawa za kushusha homa.

    Asubuhi yake homa ikiwa imeshuka walinambia kuwa vipimo vinaonesha sina malaria wala tatizo lingine lolote. mchan nikatoka na kurudi home homa yote ikiwa imeshuka ila nikiwa bado na uchovu.


    Alhamis nikiwa ofisini hali yangu tena ikabadilika, nikawa natetemeka sana, joto likapanda. Nikapelekwa kwenye dispensary ya ofisi yetu, kunipima wakanikua na Malaria wadudu 40. Wakashusha joto, na kunipa dozi ya malaria.

    Bado sielewi Aga Khan walishindwa vipi kugundua wadudu wengi kiasi hicho. Ni vizuri management ya hospitali hii ikaangalia vizuri vipimo vyao ili kulinda reputation.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...