Meneja wa Bia ya Kilimanjaro,George Kavishe akizungumza mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani)  wakati wa uzinduzi wa mbio za Bendera ya Taifa ambazo ni sehemu ya Kampeni yake ya  ‘Jivunie uTanzania’ inayokwenda sambamba na maadhimisho ya sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.Kulia ni Mratibu wa Mbio hizo kutoka kampuni ya Alta Vista Events Ltd,Carol Ndossi
Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha nchini,Suleiman Nyambui akifafanua jambo wakati wakati wa uzinduzi wa  mbio za Bendera ya Taifa ambazo ni sehemu ya Kampeni yake ya  ‘Jivunie uTanzania’ inayokwenda sambamba na maadhimisho ya sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania,ambayo imeandaliwa na Kampuni ya Bia Tanzania kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Lager.Kulia ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro,George Kavishe.
Picha ya Pamoja na Baadhi ya wanariadha watakaoshiriki mbio za Bendera ya Taifa ambazo ni sehemu ya Kampeni yake ya  ‘Jivunie uTanzania’ inayokwenda sambamba na maadhimisho ya sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager leo imezindua rasmi mbio za Bendera ya Taifa ambazo ni sehemu ya Kampeni ya ‘Jivunie uTanzania’ inayokwenda sambamba na maadhimisho ya sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.

Uzinduzi huo umefanyika katika makao makuu ya TBL Jijini Dar es Salaam na kuwaleta pamoja baadhi ya wanariadha watakaoshiriki katika mbio hizo pamoja na viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania. Mbio hizo zinatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Wakati wa mbio hizo, wanariadha mbalimbali watakimbiza bendera ya taifa kutoka kanda tatu tofauti zikiwemo Kanda ya Kati, ya Ziwa na Pwani. Baadaye watakusanyika Jijini Moshi na kuipandisha bendera moja katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Kama alivyofanya Luteni Mstaafu Alex Nyirenda (mstaafu) alipoipandisha bendera ya taifa pamoja na mwenge wa uhuru katika kilele cha mlima huo miaka 50 iliyopita.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Chara cha Riadha Tanzania, Suleiman Nyambui alisema jumla ya wanariadha 90 watashiriki katika mbio hizo huku kila kanda ikiwa na wanariadha 30.

“Bendera zitakimbizwa kuanzia kanda nne kufuata rangi zake na maana halisi ya rangi hizo kwa Taifa, Kutoka kanda ya Ziwa, mbio zitaanzia Mwanza ambapo Bendera ya Njano kuwakilisha utajiri wa madini yetu, Kutoka kanda ya Kati, mbio zitaanzia Dodoma makao makuu ya Nchi ambapo bendera Nyesi inayowakilisha rangi yetu waafrika, na kanda ya Pwani bendera ya Bluu inayowakilisha Maji,mito na vijito, wataanzia Dar es Salaam,” alisema huku akiongeza kuwa Bendera ya Kijani inayowakilisha misitu na uoto wa asili itakayotokea Arusha.

Kwa mujibu wa Nyambui, wanariadha wote watakaoshiriki wako katika hali nzuri na wamepangwa vizuri kuhakikisha kuna uwiano mzuri kuepusha hali ya kuwa na wanariadha wenye majina peke yao katika kundi moja na wale wasio na majina pia peke yao.

Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Bw. George Kavishe, alisema matayarisho yote ya mbio hizo yamekamilika huku akiwapongeza wanariadha hao kwa uzalendo wao kwani kitendo hiki kina umuhimu wakati Tanzania inaadhimisha miaka 50 ya Uhuru.

Alisema Bia ya Kilimanjaro Ina furaha kuendesha Kampeni ya Jivunie uTanzania iliyozinduliwa Julai mwaka huu a baada ya hapo kumekuwa na matamasha mbalimbali Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro na Mwanza zote zikiwa na lengo la kuwakumbusha watanzania wajivunie mafaniko waliyoyapata katika miaka 50 ya Uhuru.

“Mbio hizi tunazozindua zitasaidia kuimarisha utaifa, utalii na michezo nchini,” alisema Bw. Kavishe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...