Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen amepata ushindi wake wa kwanza ugenini tangu alipochukua timu hiyo kutoka kwa Mbrazil Marcio Maximo, Agosti mwaka jana baada ya leo kuifunga Chad mabao 2-1 katika mechi ya kwanza ya mchujo ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2014 nchini
Brazil.

Ikicheza kwa mara ya kwanza nchini Chad, Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufunga dakika ya kumi katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya hapa N'Djamena kupitia kwa winga Mrisho Ngasa.

Hata hivyo, mashabiki wa Chad walisubiri kwa dakika tano tu kabla ya kusherehekea bao baada ya kiungo Mahamat Labo kuisawazishia dakika ya 15. Labo anachezea klabu ya Laval ya Ufaransa alitumia vizuri makosa ya mabeki wa Tanzania waliochelewa kucheza mpira wa krosi.

Dakika kumi kabla ya mwamuzi Bunmi Ogunkolade kutoka Nigeria hajapuliza filimbi ya kuhitimisha pambano hilo lililohudhuriwa na takribani mashabiki 10,000, Nurdin Bakari aliyeingia badala ya Abdi Kassim aliifungia Stars bao la pili.

Mpira ulianzia kwa mshambuliaji wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Thomas Ulimwengu ambaye akiwa wingi ya kulia alifanikiwa kumtoka beki wa kushoto wa Chad kabla ya kutumbukiza krosi iliyomkuta mfungaji.

Stars na Chad zinakutana tena Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya marudiano ambayo matokeo yake ndiyo yataamua timu ipi kati ya hizo itakayoingia hatua ya makundi,kwenye kundi ambalo lina timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia.

Stars: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Idrisa Rajab, Aggrey Morris, Juma Nyoso, Shabani Nditi, Nizar Khalfan/Thomas Ulimwengu, Henry Joseph, Mbwana Samata/Mohamed Rajab, Abdi Kassim/Nurdin Bakari na Mrisho Ngassa.

Boniface Wambura
Media Officer
Tanzania Football Federation (TFF)
+23592159563
N'Djamena

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Ni mapema mno kuanza kuchekelea.

    ReplyDelete
  2. hii imenipa furaha sana leo kwavilesiku hizi siirahisi kufurahia chochote kila kona ni vikero vya hapa na pale

    ReplyDelete
  3. Wacheni kulewa sifa nyinyi ndiyo kwanza mechi ya kwanza mumewafunga kwa kigoli kimoja zaidi ndiyo munafurahia!

    Kazeni kamba vijana siyo kulala.

    ReplyDelete
  4. WEMBE NI ULE ULE ,HATA WAKIJA HAPA HIYO J5 YA 15 NOV, 2011 HAO CHAD WAPEWE KICHAPO PIA ndani na nje WARUDI KWAO.

    ReplyDelete
  5. Hongera stars..Komaeni na mazoezi kazi bado..FIFA nao wana matatizo..Timu zitachezaje ndani ya siku nne bwana pamoja na uchovu wa safari??Wambura una Uhakika ni tukifanikiwa kusonga mbele tunaingia kwenye Makundi?

    David V

    ReplyDelete
  6. Msije mkabweteka na hako kaushindi mkashindwa kusonga mbele.

    ReplyDelete
  7. Martin ChachaNovember 12, 2011

    Martin Chacha
    Duh, hongereni taifa stars, lakini kiukweli kazi ipo kwenye makundi maana hako katimu kachad ni kadogo mno kwenye mambo ya soka. Tutawamudu Ivory Coast au Moroco kwenye makundi? Poulsen andaa na vijana watakaotimika hata ukiwa haupo kama alivyokuwa anafanya Maximo usile faida tu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...