Msondo Ngoma
Sikinde Ngoma ya Ukae.

Na Mwandishi Wetu

Ikiwa imebaki wiki moja kabla ya pambano baina ya bendi mbili zenye upizani mkubwa nchini, Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra (Wana Sikinde), tayari bendi hizo zimeamua kupiga kambi kujiaanda na pambano hilo litalofanyika siku ya Krismasi kwenye viwanja vya TCC Club Chang’ombe, Temeke.

Habari za uhakika zilizopatikana jijini Dar es Salaam zimebainisha kuwa bendi ya Msondo Ngoma imeweka kambi yao jijini Mwanza wakati wapinzani wao, Sikinde, wenyewe 'wamejificha' jijini Dar es Salaam kujiaandaa na pambano hilo linalofanyika chini ya udhamini wa kinywaji cha Konyagi.

Meneja wa bendi ya Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti, jana alithibitisha habari za bendi yake 'kuhamia' jijini Mwanza akisema kuwa wameamua kujichimbia mbali ili kujiandaa vyema na pamabano hilo ambalo hufanyika kwa nadra.

“Litakuwa ni pambano kubwa mno na muhimu kwetu" alisema Kibiriti na kuongeza; "inatulazimu tujiandae vyema ili tusije tukaangusha wapenzi wetu. Tumeamua kwenda Mwanza kwa sababu ni sehemu tulivu ya kujiandaa. Tukirudi Dar es Salaam kazi itakuwa moja tu, kuwashinda watani wetu.”

Naye afisa mipango wa Sikinde Hamisi Mirambo alisema wao watabaki jijini Dar es Salaam na kufafanua; “sisi hatuendi mbali, tutajificha hapa hapa jijini kutayarisha nyimbo zetu mpya ambazo tutazitumia kuwaangamiza wapinzani wetu,” alisema Mirambo.

Mpambano huo utakaoanza saa nane mchana hadi usiku, umeandaliwa na kampuni za Bob Entertainment na Keen Arts na kudhaminiwa na kinywaji cha Konyagi chini ya uratibu wa Joseph Kapinga aliyetamba kuwa pambano hilo litakuwa la 'funga mwaka'.

Kapinga amesema mbali ya kutoa burudani kwa wapenzi wa bendi hizo mbili, pambano hilo pia litaamua ni ipi bendi bora ya mwaka 2011 kati ya bendi hizo mbili.

Ili kuondoa hisia za hujuma, hasa kwenye upangiliaji wa milio ya vyombo, kila bendi itatumia jukwaa lake kwa kupiga kwa muda wa saa moja kabla ya nyingine kupanda jukwani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. hatumwi mtoto dukani siku hiyo....SULUHU VS JINAMIZI LA TALAKA...itakua hapatoshi... Msondo mwisho wa maneno

    ReplyDelete
  2. Hivi mshindi wa pamvano la msondo ngoma na sikinde hupatikana vipi na kwa vigezo gani? Au ndiyo kila mashabiki wanaenda nyumbani wakisema "sisi tumeshinda"?

    ReplyDelete
  3. Janja ya kutafuta pesa tu, utashindanishaje bendi mbili zilizo kwenye hadhi tofauti kwa sasa, moja inapiga muziki vichochoroni kwa kiingilio cha bia wakati nyingine inapiga kwenye kumbi zinazoeleweka. Msiwajaze ujinga sikinde wasaidieni kimawazo kujikwamua maana kitendo cha wao kupiga vichochoroni kinatoa kinaashiria kuelekea kuzimu. Anayebisha aende pentagon pub mivinjeni Kilwa road kila ijumaa.

    ReplyDelete
  4. Mtoto hajawahi kumshinda baba!!!

    ReplyDelete
  5. Katika Ushindani viwango hushuka na katika Umri aliye mkubwa mkubwa umri ukienda anatakiwa awe na busara zaidi,,,kwa vile ingawa ilikuwa ni mazoea Mkubwa kumpiga mdogo mara kwa mara inaweza tokea Mdogo akamtwanga Mkubwa tena kwa Knock Out!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...