JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO MKUU WA MWAKA WA SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII UTAKAOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA GLONENCY, MOROGORO MANISPAA: KUANZIA TAREHE 19- 21 DESEMBA, 2011

Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto itaendesha Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii kuanzia tarehe 19 hadi 21 Desemba, 2011 utaokaofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Glonency, Manispaa ya Morogoro.

Mkutano Mkuu wa kisekta hufanyika kwa madhumuni ya kutathimini mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka huu; kuainisha changamoto pamoja na kuweka mikakati ya baadaye ya kuboresha utekelezaji wa shughuli za sekta. Aidha, Mkutano mkuu wa mwaka utawawezesha wadau wa sekta ya maendelo ya jamii kukutana pamoja na kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa majukumu yao ili kujenga uwezo na kuboresha utendaji katika ngazi zote yaani Halmashauri, Seketarieti za Mikoa na Wizara.

Kwa kuwa Mkutano huu unafanyika sanjari na maadhimisho ya miaka hamsini (50) ya uhuru wa Tanzania Bara ni wazi kuwa watendaji wataweza kufanya rejea kuhusu mafanikio yaliyopatikana kutokana na utendaji mzuri wa wataalamu wa sekta ya maendeleo ya jamii na kutafakari jinsi gani tutasonga mbele katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali na kuboresha utendaji wa sekta kwa ujumla.

Washiriki wa Mkutano huu ni watumishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na vile vya Maendeleo ya Wananchi, Washauri wa Maendeleo ya Jamii katika Sekretarieti za Mikoa, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri zote za Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya. Aidha, kutakuwa na wawakilishi kutoka Wizara mbalimbali na wawakilishi kutoka katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Wizara imekuwa ikiaandaa mikutano ya kisekta kwa kuwa na kaulimbiu mahsusi kulingana na vipaumbele vya maendeleo kwa wakati huo. Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka 2011 ni “Tatizo la Watoto Wanaoishi katika Mazingira Hatarishi: kwa pamoja Tuwajibike” Kaulimbiu hii inahamasisha wadau wote kutambua kuwa tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi linazidi kuongezeka kwa kasi kubwa nchini; na ni wajibu wa kila mdau hasa familia, kuhakikisha kuwa hatua madhubuti zinachukuliwa kukabiliana na tatizo hili ambalo linaathiri jamii na maendeleo ya nchi yetu. Matarajio ya Wizara ni kupata mapendekezo ambayo yatawezesha kuwapa watoto wote wa Tanzania haki zao za msingi ambazo ni haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushirikishwa na kutobaguliwa.

Katika mkutano huu mada mbalimbali zitatolewa kwa kuzingatia kaulimbiu iliyotajwa hapo juu. Mada hizo ni mosi, Mchango wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii katika kuleta maendeleo na kupunguza tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi; pili, Ukatili dhidi ya Watoto; tatu, Nafasi ya Wanawake na Wanaume katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii na nne, Uzoefu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kushughulikia Watoto wanaoishi katika ajira za hatari na yatima.

Aidha, Wajumbe wa Mkutano huo wanatarajia kuandaa maazimio ambayo yatalenga kuimarisha nafasi ya Sekta ya maendeleo ya jamii katika kudhibiti tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwemo watoto wanaoishi mitaani, wanaotumikishwa katika ajira hatarishi na yatima.

Mkutano utafunguliwa tarehe 20 Desemba, 2011 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mheshimiwa Sofia M. Simba (Mb), na kufungwa tarehe 21/12/2011 na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu (Mb),

Anna T. Maembe
KAIMU KATIBU MKUU
16/12/2011

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...