Na Hamad Hija-Maelezo Zanzibar.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Shamsi Vuai Nahodha ameitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)kuusimamia mradi wa Maji ili wananchi wa maeneo ya Nungwi waweze kufaidika
Amesema kuwa mradi huo ni muhimu sana kwa wananchi hao kwani utasaidia sana kupata maji ya uhakika na salama jambo ambalo litasaidia katika kutunza afya kwa wananchi.
Nahodha ameyasema hayo huko Tazari Mkoa wa Kaskazini Unguja alipokuwa akizindua Mradi wa Maji katika eneo hilo ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kuwa katika kuyaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 ni lazima yaenziwe kwa vitendo kama hivyo vya kuleta maendeleo kwa wananchi na siyo kwa maneno.
Aidha amewataka wananchi wa eneo hilo kutoa ushirikiano kwa ZAWA ili malengo yaliyopangwa katika utekelezaji wa mradi huo yaweze kutimia.
Amesema endapo ZAWA watausimamia vyema mradi huo kwa kushirikiana na wananchi hao ni dhahiri kwamba wananchi watafaidika sana na kuondokana na kadhia ya muda mrefu inayowasumbua.
Mradi huo ambao unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh. 500Millioni utakuwa wa miezi nane,lakini amesema atafurahishwa zaidi ikiwa Mradi huo utamalizika kabla ya miezi hiyo.
Waziri Nahodha amewataka Wananchi wa eneo hilo kujituma kama rasli mali watu ili mradi huo uweze kufanikiwa kwa haraka na Wananchi hao waweze kufaidika kwa Mradi huo wa Maji uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa.
Mradi huo ambao ulianza Augosti 2011 unatarajiwa kumalizika mwaka 2012 ambapo jumla ya Wananchi Elfu kumi na moja wa Vijiji vya Kilimani, Tazari na Kigunda,watafaidika na mradi huo
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ndio unaofadhili Mradi huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...