MGOMBEA wa CCM katika uchaguzi wa Jimbo la Uwakilishi Uzini Zanzibar, Mohammed Raza Daramsi ameibuka na ushindi wa asilimia 61 baada ya kupata kura 5,377.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Kati, Mussa Ali Jumma, alitangaza matokeo hayo jana jioni baada ya kumalizika kwa upigaji kura ulioanza jana asubuhi. Kwa mujibu wa matokeo hayo, Raza alifuatiwa kwa mbali na mgombea wa Chadema, Ali Mbarouk Mshimba aliyeshika nafasi ya pili baada ya kupata kura 281 sawa na asilimia 4 ya kura zote.

Mgombea wa CUF, Salma Hussen Zarali alimfuatia mgombea wa Chadema kwa karibu kwa kura 223 sawa na asilimia 3.8 ya kura zote. Wengine walioshiriki katika uchaguzi huo na kura zao katika mabano ni Yussuf Rashid Mshengawa ASP (8), Khamis Khatibu Vuai wa Tadea (14).

Uchaguzi huo umefanyika baada ya kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, Mussa Khamis Silima ambaye alifariki dunia mwaka jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kupata ajali ya gari huko Dodoma.

Mabadiliko Katiba ya CCM Wakati huo huo, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) imeridhia mabadiliko makubwa ya Katiba yake ya mwaka 1977 Toleo la mwaka 2010 na kanuni zake, ikiwemo kuongeza idadi ya wajumbe wa Halmashauri hiyo kutoka zaidi ya 200 hadi zaidi ya
300.

Pia katika marekebisho hayo kuanzia sasa viongozi wakuu wastaafu wa ngazi ya taifa
wataundiwa Baraza la Ushauri ndani ya chama hicho kwa ajili ya kutoa ushauri kwa chama hicho na Serikali inayoongozwa na CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema idadi hiyo ya wajumbe wa NEC imeongezeka kutokana na makundi mapya ya wajumbe yaliyobainishwa kwenye Katiba hiyo.

Aliyataja makundi hayo kuwa ni wajumbe wa NEC ngazi ya taifa ambao ni 20 kati yao 10 kutoka Tanzania Bara na 10 Tanzania Visiwani na wajumbe 10 wa kuteuliwa
na Mwenyekiti wa chama hicho.

Makundi mengine ni wajumbe wanaoingia kwa nafasi zao ambao ni Rais, Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Zanzibar ambao ni viongozi kutoka CCM. Wengine ni wajumbe wanaotoka kwenye vyombo vya uwakilishi ambao ni wabunge 10 na Wawakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar watano wa chama hicho.

Alisema kundi jingine ni wajumbe 221 wanaochaguliwa kutoka wilayani na watakaochaguliwa katika nafasi hizo ni viongozi wote wa kazi za muda wote kama vile wenyeviti wa wilaya, ili kuweka wazi zaidi wajibu wa wajumbe hao kuwa karibu na wanachama na kushughulikia shida zao.

“Hii yote bado ni utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, tulisema dhana hii itagusa maeneo mengi na eneo hili ni la kuhakikisha chama kinasogea karibu na wanachama,” alisema Nape. Alisema kupitia nafasi hizo za wilaya, wanachama watawakilishwa vizuri ingawa katika ngazi ya mikoa bado Mwenyekiti na Katibu wanabaki kuwa wajumbe wa NEC.

Kundi la mwisho kuwa ni la wajumbe wanaochaguliwa kutoka kwenye Jumuiya za chama; Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) nafasi 15, Tanzania Bara tisa Zanzibar sita, Umoja wa Vijana (UVCCM) 10, Tanzania Bara sita na Zanzibar wanne na Jumuiya ya Wazazi watano, bara watatu na Zanzibar wawili.

Kuhusu Baraza la Ushauri, Nape alisema viongozi wastaafu wakuu kama vile marais wastaafu na wenyeviti wa CCM taifa, marais wastaafu wa Zanzibar na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Taifa wastaafu watakuwa wajumbe wa Baraza la Ushauri.

“Baraza hili litakuwa na kazi ya kutoa ushauri kuhusu kazi zinazofanywa na CCM na Serikali zinazoongozwa na chama hicho katika jambo mahsusi,” alisema Nape. Alisema pia kikao hicho kimepitisha uamuzi kuwa viongozi hao wastaafu wawe na nafasi ya kualikwa ama wote au mwakilishi wao kuhudhuria vikao vya chama ngazi ya taifa.

Hadi tunakwenda mitamboni jana, bado mkutano huo ulikuwa ukiendelea kujadili ajenda nyingine ambazo zitaainishwa leo.(Chanzo: Habari Leo)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. sasa asiposhinda Raza ashinde nani mwingine? hivi kuna uwezekano wa tajiri kushindwa kesi kwenye nchi za kimasikini? na hapo hapo akiwa kakumbatiwa na serikali?

    mnapoteza hela za uchaguzi watu kama hao bila kufanya uchaguzi mngelikuwa mnakubaliana kuwapa tu

    ReplyDelete
  2. CUF wameanza kudorora

    ReplyDelete
  3. WATU WALIOANDIKISHWA = 8,743
    WATU WALIOPIGA KURA = 5,931
    TURNOUT = 67.84%
    KURA KWA RAZA = 5,377


    THEREFORE; SIO 61% BALI NI 91%! JIMBO HILI NI LA CCM BILA SHAKA..

    HONGERA MH. RAZA! KARIBU BUNGENI.

    NDUGU AF.

    ReplyDelete
  4. Kidumu chama cha mapinduzi...hivi kwa nini tusirudi kwenye mfumo wa chama kimoja?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...