Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kuomboleza kifo cha Mwakilishi wa Jimbo la Bububu (CCM) Mheshimiwa Salum Amour Mtondoo.
Hayati Mtondoo alizikwa kijijini kwao Bumbwini, Mkoa wa Kaskazini Unguja jana, Ijumaa, Machi 16, 2012, baada ya kufariki dunia juzi kwa matatizo ya shinikizo la damu, malaria na sukari.
Katika salamu zake kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea kwa mshtuko na masikitiko habari za kifo cha Mheshimiwa Mtondoo ambaye alikuwa Mwakilishi wa Wananchi wa Bububu katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi.
Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko habari za kifo cha Mheshimiwa Mtondoo. Siyo tu alikuwa mwanachama hodari wa chama chetu, lakini pia katika kipindi chake cha uwakilishi amefanya kazi nzuri na ya kukumbukwa ya kutetea ipasavyo maslahi ya wananchi wa jimbo lake kwa uadilifu na moyo mkubwa wa kujituma,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
Kupitia kwako Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa Wawakilishi wote kwa kuondokewa na wenzao, kwa wananchi wa Bububu kwa kumpoteza mwakilishi wao hodari na kwa wana-CCM wa jimbo hilo kwa kifo cha mwanachama mwenzetu.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Aidha, naomba uniwasilishie salamu zangu kwa wanafamilia wote wa Mheshimiwa Mtondoo kwa kupotelewa na mhimili mkuu wa familia. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Aidha, nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amen.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
17 Machi, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...