Kikundi cha Utamaduni kutoka Cameroon kilitumbuiza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika ukumbu mkuu wa mikutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
wanautamaduni kutoka nchi Cameroon ambao walipamba siku ya kimataifa ya kumbukumbu ya biadhara ya utumwa na utumwa wakiigiza namna biashara hiyo ilivyokuwa ikifanyika kwa kuwakamata watu wakiwamo wanawake na kuwapiga mnada mbele ya wafanyabiashara haramu wa biashara hiyo. inakadiliwa kwamba zaidi wa Waafrika milioni 28 waliadhirika na biashara hiyo pamoja na ukatili wa hali ya juu waliofanyiwa kwa vile tu ya rangi yao. katika maadhimisho hayo jumuia ya kimataifa imekumbushwa kwamba ingawa biashara hiyo imekomeshwa zaidi ya miaka 200 iliyopita lakini madonda ya utumwa na athari zake bado zingalipo hadi sasa kwa mtu mweusi kuendelea unyanyaswa , kukandamizwa na kubaguliwa kwasababu tu ya rangi yake.
Bango linalobeba ujumbe wa maadhimi ya siku ya kimataifa ya biashara ya utumwa na utumwa uliofanyika kupitia bahari ya Atlantik. maadhimisho hayo hufanyika kila Marchi 25 safari hii yalifanyika siku ya jumatatu ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro ambaye pamoja na mambo mengine amesisitiza jumuia ya kimataifa kuwa macho na ongezeko la aina mpya ya utumwa na ubaguzi wa rangi.
Na Mwandishi Maalum - New York
Ikiwa ni zaidi ya miaka 200 imepita tangu biashara ya utumwa na utumwa ulipokomeshwa. Jumuiya ya Kimataifa, imetakiwa kuwa macho dhidi ongezeko kubwa la aina mpya ya utumwa unaojikita katika misingi ya ubaguzi wa rangi, biashara haramu ya binadamu, utumwa wa madeni, unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia, ndoa za utotoni na utumiaji wa watoto katika vita.
Tahadhari hiyo imetolewa siku ya jumatatu wiki hii na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha- Rose Migoro wakati Umoja wa Mataifa ulipoadhimisha siku ya kimataifa ya ukomeshaji wa biashara ya utumwa na utumwa, maadhimisho ambayo hufanyika Marchi 25 ya kila mwaka.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni “kuwaenzi mashujaa , wapinzani na waathirika wa biashara ya utumwa”. Pamoja hotuba maadhimisho hayo yalipambwa na kikundi cha utamaduni kutoka nchini Cameroon
Migiro amesema, licha ya kwamba kumekuwapo na sheria mpya na mbinu mpya na bora za kukabiliana na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Hata hivyo anasema. “ Ni lazima tukubali kwamba kunaongezeko la vitendo vinavyoashiria wazi kuwapo kwa ubaguzi kwa misingi ya rangi katika maeneo mengi duniani”
Na kuongeza kwamba kauli zinazoashiria ubaguzi wa rangi zimekuwa zikiongezeka kupitia majukwaa ya kisiasa, katika baadhi ya vyombo vya sheria, mashirika na katika matumizi ya teknolojia za kisasa za mawasiliano ambapo vyombo hivyo vimekuwa vikitumika kueneza dhana hasi ya kwamba rangi moja ni bora dhidi ya rangi nyingine.
Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa kila mtu anao wajibu wa pamoja wa kuwa macho juu ya ongezeko la vitendo hivyo vya ubaguzi wa rangi na aina mpya ya utumwa.
Akabainisha kwamba maadhimisho hayo licha ya kuwakumbuka mamilioni ya waafrika walioathiriwa na janga la kutisha la biashara ya utumwa na utumwa. Maadhimisho hayo ni lazima pia yatumike kama sehemu kujifunza sababu na matokeo ya biashara ya utumwa, ukandamizaji na ubaguzi wa rangi. ubaguzi ambao uliifanya rangi moja ya binadamu kujiona kuwa ni bora zaidi dhidi ya rangi nyingine.
Akamaliza kwa kusema “ kwa kupitia siku hii basi sote tuonyeshe dhamira ya kukabiliana na kupambana na ubaguzi wa rangi na kujenga jamii bora kwa kuzingatia usawa , haki na mshikamano”.
Pamoja na Naibu Katibu Mkuu kuzungumza katika maadhimisho hayo, Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Bw. Nassir Abdulaziz Al-Nasser naye alizungumza ambapo kama ilivyo kuwa kwa Naibu Katibu Mkuu, alisisitiza haja na umuhimu wa Jumuia ya Kimataifa kuunganisha nguvu dhidi ya aina mpya ya utumwa.
Akasema jumuia ya kimataifa inapashwa kujifunza kutoka yale yaliyojitokeza katika biashara ya utumwa na utumwa na kuhakikisha matukio yale ya kutisha yalioathiri na kuudhalilisha utu na hadhi ya Mwafrika hayajirudi kwa namna moja ama nyingine au katika mfumo wowote ule.
Akabainisha kwamba mwaka 2007 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitenga Marchi 25 ya kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya kuwakumbuka wa Wafrika zaidi ya milioni 28 walioathirika na janga kubwa la biashara ya utumwa na utumwa kupitia bahari ya Atlantik.
Aidha Bw. Al- Nasser amezikumbusha nchi wanachama ambazo hazijachangia mfuko wa ujenzi wa mnara wa kudumu wa kumbukumbu ya utumwa kufanya hivyo.
Mbali ya Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wazungumzaji wengine katika maadhimisho hayo walikuwa ni Balozi Chitsaka Chipaziwa wa Zimbabwe aliyezungumza kwa niaba ya nchi za Afrika, Balozi Jane Chigiyai wa Micronesia aliyezungumza kwa niaba ya nchi za Asia na Pacific, Balozi Petrika Jorgji wa Albania aliyezumgumza kwa niaba ya nchi za Ulaya Mashariki na Balozi Dessima Williams ambaye alizungumza kwa niabya ya nchi za America ya Latini na Visiwa vya Caribbean.
Wengine waliozungumza ni Balozi Daniele Bodini wa San Marino aliyezungumza kwa niaba ya nchi za Ulaya Magharibi na nchi nyingine, na Balozi Rosemary DiCarlo aliyezungumza kwa niaba ya Marekani. Wakati Dkt. Rick kittles ambaye ni Mkurugenzi wa African Ancestry,Inc yeye alitoa mada kuhusu historia ya utumwa na madhira yake kwa mtu mweusi na matumizi ya vinasaba katika kuwasaidia wamarekani wenye asili ya Afrika kutambua asili ya kule walikotoka.
Maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya biashara ya utumwa na utumwa yanafanyika kwa juma zima yakihusiaha pia, midahalo ya wanafunzi, asasi zisizo za kiserikali, maonyesho ya sanaa mbalimbali zinazohusiana na utumwa, filamu makala mbalimbali pamoja na vyakula vya asili ya Afrika.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...