Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego akisisitiza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya Baraza hilo ambapo mada ya wiki hii ilihusu Sanaa ya Unenguaji na Maleba katika Muziki. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Juma Ubao na Mtendaji wa Binti Leo, Betty Kazimbaya.
Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Bw. Ubao akieleza athari za kuwepo kwa unenguaji usiyozingatia maadili kwenye muziki wa dansi wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Mtendaji kutoka asasi ya Sanaa za Majukwaani ya Binti Leo Bi. Betty Kazimbaya akiongea na Wadau wa Sanaa kuhusu Umuhimu wa Maleba Kwa Wasanii wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa.Kulia ni Mratibu wa Jukwaa hilo, Godfrey Lebejo.
Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mjadala.

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Sanaa la Taifa (BASATA) limeeleza kukerwa na hali ya uvunjifu wa maadili katika sanaa hususan unenguaji na kutaka hali hiyo sasa ifike mwisho.

Akizungumza katika Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bw. Ghonche Materego alisema kuwa, ni lazima kuwe na mabadiliko dhidi ya uvunjifu maadili kwenye sekta ya Sanaa vinginevyo hatua zitaanza kuchukuliwa.

“Haya si mambo yanayofurahisha, ni lazima jamii ioneshe ushirikiano kwa kupambana na udhalilishaji wa aina hii, kuna mambo yasiyopaswa kufanyika hadharani na yanabaki kuwa ya ndani tu kwenye night club na Casino na si vinginevyo” alisistiza Materego.

Aliongeza kuwa, haivumiliki kwa maonesho hayo ya sehemu maalum za ndani kuanza kufanywa hadharani kwani ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi na ni udhalilishaji wa sekta ya Sanaa hivyo aliwataka Wasanii kujipanga kupiga vita hali hii.

“Mabadiliko lazima yafanywe. Vyama, mashirikisho na mitandao ya Wasanii vianze mara moja kuangalia maadili kwenye maeneo yao. Hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya watakaoendelea kuvunja maadili kwenye Sanaa” alizidi kusisitiza Materego.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) Juma Ubao alisema kuwa, kinachofanyika sasa kwenye unenguaji si muziki wa dansi bali ni aina fulani ya matukio ambayo ni maalum kwa ajili ya night club na kasino.

“Unenguaji wa uchi usihusishwe hata kidodo na muziki wa dansi. Haya yanayofanyika sasa ni kuuchafua muziki huu. Ni lazima tuelewe haya si ya kuvumilia kwenye muziki wetu” alisisitiza Ubao.

Alizidi kueleza kuwa, huko nyuma wanenguaji walivaa kwa heshima na kufanya maonesho yaliyovutia watu wa rika zote lakini kwa sasa hali ni tofauti kutokana na kuwepo kwa vikundi vinavyovaa uchi na kuanza kunengua hadharani.

Kwa upande wake, Mtendaji kutoka asasi ya Binti Leo inayojishughulisha na Sanaa za majukwani Bi. Betty Kazimbaya alisema kuwa, kinachofanyika sasa ni kudhalilisha Sanaa na ukiukwaji wa maadili kupitia maleba (mavazi ya Wasanii) hivyo kutaka hatua zichukuliwe.

“Kazi kubwa ya maleba (mavazi ya wasanii) ni kusitiri mwili, inakuaje kuwe na vikundi havitumii mavazi haya kwa kazi hiyo? Alihoji Kazimbaya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Hongera Basata:

    Ilikuwa ni fedheha sana ukitaka kuazama Vipindi vya Luninga kama utakaa na mtu wa aibu kwako kama Mkwe au Watoto.

    Wadau wa Marumba walizidi kutukatikia na kutukalia kihasara hasara utadhani wao hawana watu wa kuwaonea aibu wanaowaona.

    Hili zoezi linatakiwa liwekewe utaratibu wa kuendelea!

    ReplyDelete
  2. Wadau mimi nataka kujielemisha tu,hivi "kuvaa uchi" ndo nini katika kiswahili!

    Wasanii waelezwe kitu gani wasivae au wasionyeshe kwenye muziki majukwaani vinginevyo watu wengi watakuwa hawaendi na watoto.

    Kwani kunengua vizuri lazima uonyeshe sehemu za siri.Mbona kuna mavazi aina nyingi yanayompendeza mnenguaji!

    ReplyDelete
  3. Ahhh hii sasa basi!

    Unakuta Msanii wa Muziki wa Dansi ama Mchezaji wa Mziki (Mnenguaji) akiwa Jukwaani 'anakatika' na 'kusasambua' kwa madaha na kujiamini kabisa utafikiri hana wanaomwita yeye Mzazi, utadhani yeye mwenyewe kama hana Wazazi, kama vile hana Wakwe, kama hana Mashemeji na Mawifi na watu wa karibu wa kuwaonea aibu.

    Ndio Muziki hatukatai ni kazi kama kazi zingine ila kwa Mtaji huu inatia kinyaa !

    ReplyDelete
  4. Mimi sioni kama kunasababu yoyote kwa BASATA kuingilia ulimwengu wa VIJANA, swala la wanenguaji kukaa UCHI sisi vijana wa sasa ndio tunapenda so TUACHIENI ULIMWENGU WETU JAMANI!!

    ReplyDelete
  5. Kanga moko ,laki si pesa ,njoo uone kanga inavyovaliwa ............

    ReplyDelete
  6. Mdau mbona unatujumuisha vijana wa sasa sote?Mimi pia nikijana wa sasa na sipendi hizo tabia.
    Kitu kimoja tu mimi naona BASATA wanajichanganya,nijuavyo mm muziki unaenda mkono kwa mkono na zinaa na ulevi pia.Hivyo basi kutaka mabadiliko ktk mavazi tu bado hamtakua mumetatua bali na ulevi na mazingira ya ngono pia yawe marufuku.Km hilo mtalikubali moja kwa moja na mziki pia utatoweka jambo ambalo mm ndio ningefurahi kuliona.Vinginevyo mnachotaka BASATA hakiwezekani,chumvi itabaki kuwa chumvi na haitakua sukari kwa kujaribu kuipunguza ukali wake.

    ReplyDelete
  7. NAONA MMEKOSA KAZI! KWELI KATIKA MAMBO YA MUHIMU YOTE MMEONA LA UNENGUAJI TU? JITAHIDINI NCHI IPATE MAENDELEO KWA WATU WALIO MASIKINI KULIKO KUONGELEA MAMBO YASIYO NA MSINGI! UTAMADUNI WA MWAFRIKA NI NGOMA NA KUKATA VIUNO. WANAUME WANAFICHA UUME TU! NA WANAWAKE WANAACHIA MAZIWA WAZI NA KUFICHA UKE WAKE! HIYO NDIO ILIKUWA MILA YETU TOKA ZAMANI NYIE MNAOJIDAI MMESOMA NDIO MNAOHARIBU MILA ZETU! MMASAI MNAMVALISHA NGUO ZA KISASA! MMAKONDE MNAMKATAZA ASIWEKE NDONYA WALA KUCHANJA CHALE ZAKE NA ILE NDIO HATA WAZUNGU WALIIGA NA KUITA TATOO! HAPO NYUMBANI MNASEMA TATOO NI UHUNI! KUMBE NDIO MILA ZETU HIZO MLIZOPIGA MARUFUKU! LETENI MASHINE ZA KUSAIDIA WAGONJWA WA FIGO WAPATE MATIBABU YA DAYALISISI, ILI WAISHI MAISHA MAREFU ZAIDI KULIKO KUONGEA UPUUZI HUO! ONGEENI KUHUSU WASANII WANAVYOKOSA HUDUMA MUHIMU NA HAKI ZAO KULIKO HAYO MLIYOSEMA.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...