Ndugu zangu,
TANGU ‘Enzi za Mwalimu’, kukiwa na jambo kubwa kitaifa, basi, Mwalimu aliliongea kupitia kwa “ Wazee Wa Dar Es Salaam”. Na mahali haswa wanapokutana ‘Wazee wa Jiji’ kumsikiliza ‘ Mkuu Wa Kaya’ ni pale Upanga kwenye Ukumbi wa Diamond.
Jambo hilo lililoasisiwa na Mwalimu sasa limekuwa ni utamaduni wa kisiasa. Mathalan, ni pale Upanga Diamond Jubilee ndipo Mwalimu alipotangaza vita dhidi ya Idi Amin kupitia Wazee Wa Dar Es Salaam . Nilipokuwa mtoto pale Ilala, nilitamani sana nikue nije kuwa mtu mzima, kisha niwe mmoja wa ‘ Wazee wa Dar Es Salaam’ ! Ndoto yangu hiyo imefutika! Naam, nimepoteza sifa ya kuwa ‘ Mzee wa Dar Es Salaam’!
Ndio, sifa ya kwanza ya kuwa ‘ Mzee wa Dar Es Salaam’ ni lazima uwe na zaidi ya miaka 50, uwe mkazi wa Dar Es Salaam kwa miaka isiyopungua 20 mfululizo! Hilo halijaandikwa popote lakini ‘ Wazee’ wenyewe wa jiji wanauzingatia utaratibu huo.
Siku za karibuni kuna “Kijana wa Dar es Salaam” kaninong’oneza kuwa wako mbioni kuwashawishi wazee wa jiji waongeze sifa za kuwa mzee wa Darisalama. Kwamba ili uwe Mzee wa Dar Es Salaam ni sharti, ama uwe umezaliwa na kukulia Dar, au umezaliwa nje ya Dar lakini ujana wako wote umeishi Dar. Hivyo basi, unapoteza sifa ya kuwa Mzee wa Dar es Salaam kama umekuja Dar ukubwani! Marekebisho hayo ya taratibu na sifa yakifanyika, huenda hata mie nitakuwa na sifa ya kuwa Mzee wa Dar es Salaam.
Na Wazee wa Dar Es Salaam wana Mwenyekiti wao. Kwa kawaida siku ya ‘ shughuli’ ya wazee, huvalia kanzu, kibagharashea na kizibau. Ndiye huyu ambaye huwa wa kwanza kumpokea ‘ Mkuu wa Kaya’ anapoingia ukumbini kuwahutubia wazee.
Ni kwa namna gani basi Mwenyekiti wa Wazee wa Dar Es Salaam anachaguliwa?
Jibu: Hilo ni swali la kizushi na usithubutu kuliuliza mbele ya ‘ Wazee wa Dar es Salaam’- watakutoa mbio kwa bakora! Lakini lililo dhahiri ni kuwa, Wazee Wa Dar Es Salaam hawajawahi kuwa na Mwenyekiti mwanamke. Hata Bi. Titi Mohammed hakupata kufikiriwa. Heshima ya kumpa barabara kuitwa kwa jina lake ilitosha, na amshukuru Julius, wanasema Wazee ‘ orijino’ wa Dar Es Salaam.
Ndio, Mkuu yeyote wa Kaya katika nchi hii atashauriwa aongee mbele ya Wazee wa Dar Es Salaam kama ana kubwa analotaka liwafike wananchi. Ni mara moja katika miaka ya karibuni nimemsikia Rais wa nchi akilihutubia taifa kupitia Wazee wa Mkoa wa Dodoma.
Inasemekana jambo hilo liliwashtua baadhi ya Wazee wa wa Dar Es Salaam. Na kuna siku nilitembea kwa miguu mitaa ya Kariakoo Kusini; Livingstone, Mahiwa, Swahili na mingineyo. Hatimaye nikafika kwenye kijiwe cha chai na kahawa pale Mtaa wa Lumumba. Nilianzisha mjadala juu ya Wazee wa Dar Es Salaam. Na hapo nikayasikia manung’uniko.
Ndio, baadhi ya Wazee wa Dar Es Salaam wanaamini kuwa Ilala ndio Dar Es Salaam. Na kwamba ni Wazee wa Ilala ndio waliompokea Julius Nyerere alipoingia mjini. Wanahoji; Iweje Wazee wa ‘ mashambani’ Kinondoni na Temeke nao waitwe Wazee Wa Dar Es Salaam? Swali linabaki; Wazee Wa Dar Es Salaam ni akina nani?
Maggid Mjengwa,
Iringa,
0788 111 765



Wazee wa Dar es Salaam wako katika makundi matatu (1) Wenyeji wa asili wa Dar, k.m. marehemu Thabit Wadau (baba yake mkubwa Dr R Dau), Kitwana Kondo, marehemu mzee Mohamed wa Kariakoo (baba yake Halima Kibadeni), marehemu Abdul Baki, n.k. (2) Walowezi wa vizazi vya tatu, nne na tano (ukoo wa kina Sykes, Paul Rupia, marehemu Hamisi Akida na wengineo). (3) Wahamiaji waliokulia Dar na kutoa mchango ulioonekana katika jamii. Hawa ndio wazee wa Dar.
ReplyDeleteKwa kawaida wanaohudhuria mikutano hii ni wazee wastaafu wa chama tawala kuanzia ngazi za chini wakati ule wa nyumba kumi. Ingawa haitangazwi ila utaratibu ndio huo na ndio maana kazi yao huwa ni kushangilia na kupongeza kwa ushabiki wa kisiasa kwa lolote wanaloambiwa bila kujali kama wanachoambiwa ni ukweli. Hata uratibu wa mikutano hiyo hufanywa na wazee wa chama hiki ikiwa ni pamoja na kutayarisha mavazi.
ReplyDeleteNdugu Mjengwa mi nachoweza sema kama maoni yangu ni kwamba, kwa mtazamo wa Mwl na nyakati zake, ilikuwa ni jambo la busara, tena la kiungwana kuwaita wazee na kuwaeleza jambo muhimu la kitaifa. Kwa sababu Mwl. aliamini wazee ni kundi muhimu sana katika jamii hasa katika kutoa ushawishi na nasaha zitakazo wasihi vijana na makundi mengine yafuate ushawishi wao. Na kwa wakati huo, wazee waliheshimika sana. Kwa kuwa Mwl. alipokelewa na wazee wa Dar, akaishi nao vizuri, akakubaliana nao mambo mengi ya kisisasa, wakasaidiana, mpaka wakaanzicha TAA, baadae TANU, hatimaye Uhuru, kwake yeye Mwl. wazee wa Dar es Salaam walikuwa kundi muhimu sana kwake katika kutatua mambo ya nchi hii, aliwaomba wamsaidie katika kuwashawishi vijana kufanya kazi nk.
ReplyDeleteLakini sasa ninavyodhani, tunapoongele wazee wa Dar es Salaam, ni kundi fulani tu la watu wenye umri mkumbwa ambao wengi wao ni wanachama au washabiki wa CCM wanaotumiwa sana kwa masuala ya propoganda za kisiasa.Heshima yao na uzito wa majukumu waliyokuwa wakipewa hapo unaporomoka!!! Kwa mfano hivi sasa serikali ina mgogoro na madaktari, badala ya serikali kutafuta muafaka utasikia inakimbilia kuwahutubia wazee wa Dar es Salaam. Katika mantiki hiyo ya kupoteza umuhimu ndo maana wao kwa wao wanaanza kubaguana, kuwa sisi wa Ilala ndio wazee wa Dar es Salaam na wao wa shamba (Temeke, Kinondoni na Mabwe pande ukitaka) sio wazee wa Dar es Salaam.Raisi akizungumza na wazee wa Dodoma au Mbeya au Songea, utawasikia hao wazee wa Dar es Salaam wakilalama, kwa nini amefanya hivyo!!! wanalalama kwa sababu fikra zao zinawatuma kudhani wao wana-privilege kuliko wazee wengine nchi hii, wanadhani wao wako karibu sana na rais kwa kukaa Ilala. Huko ni kukwepa majukumu na kutojua nafasi yao katika jamii, na shida hii inaletwa na composition yao. Sio wazee wa Dar es Salaam ila ni wazee wa CCM. Mtazamo huo uko sawasawa na wa serikali ambao si sahihi, kuwa kukitokea jambo azima ikafanye siasa kupitia kwa wazee. Katika mabadiliko ya kijamii tuliyopitia toka enzi za Mwl. hadi sasa, sidhani kama nafasi na majukumu ya wazee vinaheshimiwa kama ilivyokuwa enzi hizo.
Ila ambalo kwangu naona pia ni sifa ya kuwa Mzee Wa dar es salaam lazima pia uwe mwana TANU au wa sasa CCM! maajabu na mara nyingi wana vaa ukijani?...Itakuwaje baada ya 2015?
ReplyDeleteAcha owongo. Hizo sifa za uzee wa Dar kakupa nani? Au ni mwngo mwenzio anataka utuzoeshe uwongo? Kama umedanganywa wewe usituzoeshe uwongo. Acha kabisa. Andika kitu cha ukweli, hisia zako sio muhimu kwa jambo kama hili. utatupotosha. TENGANISHA UKWELI NA MAWAZO YAKO.
ReplyDeletewazee wa Dar ndio walioleta uhuru
ReplyDeleteHakuna lolote anaogopa asirogwe
ReplyDeletewazee wa Dar ndo waliopigania uhuru na ndio kundi lenye nguvu na busara ktk kutatua mambo meng ya msingi katika nchi na kwa taarifa tu ni hao hao wazee wa Dar ndio waliomkaribisha JKN Mzizima ili kuendleza harakati za uhuru wa Tanganyika na hakuna la ajabu la kushangaza,Kwan ikulu,bandari kuu,kiwanja kikuu cha ndege hata reli na ubungo temino vyote vipo Dar!na hata Simba na Yanga ni za Dar,tena ukiondoa temino ya UB vingne vyote vhpo Ilala ya mzizima na majemadari wao toka enzi za kina Tewa,Sykes,Dosa mpaka leo kina Id Simba,Alhaj Mbilili,Kawambwa n.k bado kundi hlo lina nguvu hata ya kuweka mtawala wa nchi.Japo lina harufu ya CCM
ReplyDeleteHakuna cha maana chochote kuwa mzee wa Dar hiyo ni moja ya ujinga mwalimu alitumia hiyo kutengeneza njia yake kisiasa.. Kinachotakiwa kuwa na wazee wa Nchi watakao weza kuikemea serikali.
ReplyDeleteRasVin,
Medical Instute Heidelberg DE,,
Kama wazee ndio waliomkaribisha Mwl na kuwa nae katika harakati za chama na uhuru hadi kupata uhuru. Hapa jibu liko wazi kuwa wazee wa Dar es salaam ni wachama tawala.
ReplyDeleteSioni kwanini hao wazee wa Dar waheshimiwe. Kwa lipi hasa? Kwa sababu ya kukaa Dar? Nasikia wanakuwaga wa kwanza kujisifu kuwa wao ndiyo walioanzisha Mzizima....vipi hao watangulizi wa kijerumani, kiarabu, waingereza na wahindi? mbona hamkuwaweka katika kundi la wazee wa Dar. Kwa taarifa yenu hao hawana nguvu yoyote ya kumweka Rais zaidi ya kujipa cheap popularity...kwamba enzi zile..enzi zile tulifanya hivi au hivi. Ni muhimu wakafikiria mambo ya maana yanayoendana na karne ya 24 kuliko kujipa umaarufu usio na maana. Ni kweli wakiitwa kama ilivyotokea jana/leo watakachofanya ni ushabiki usio na maana.
ReplyDeleteNdugu zangu kama ulipata bahati ya kuona ile video ya hotuba ya Mwalimu iliyoeleza jinsi alivyopelekwa Bagamoyo na wakafanya maombi makubwa pamoja na kufunga ili upatikane uhuru Mwl alisema alipelekwa na wazee wa DSM. Ndiyo wazee waliopambana hadi uhuru ukapatikana. Mambo ya Chama tuweke pembeni.
ReplyDelete