JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA
KUMILIKI KISHERIA WANYAMAPORI AU MASALIA YA WANYAMAPORI
Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa taarifa kuwa mtu yeyote haruhusiwi kumiliki nyara za serikali, yaani mnyamapori au kipande chochote cha mnyamapori, bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori. Hii inatokana na Kifungu cha 86(1) na (2) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura Na. 283 ya mwaka 2009 ambacho kinapiga marufuku kumiliki nyara kinyume cha sheria.
Kwa mfano, mtu yeyote haruhusiwi kumiliki, chui, simba, punda milia, fisi, au mnyama yeyote kwa sababu yoyote ile bila kibali kinachotolewa kisheria.
Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura Na. 283 inatoa tafsiri ya nyara za serikali kuwa ni mnyamapori aliye hai au aliyekufa ikiwa ni pamoja na masalia yake. Masalia hayo ni kwa mfano pembe, mifupa, ngozi, kucha, kwato, nyama, nywele, manyoya, mayai, au sehemu yoyote ya mnyamapori au nyara zilizotengenezwa.
Wizara inawataka watu wote wanaomiliki nyara bila vibali watoe taarifa na maelezo kuhusu namna walivyopata nyara hizo kwenye Ofisi za Idara za Wanyamapori za: Wilaya,Mkoa, Mapori ya Akiba au Kikosi dhidi ya Ujangili. Baada ya uhakiki taarifa hizo zitawasilishwa Idara ya Wanyamapori Makao Makuu ili uamuzi sahihi ufanyike kuhusu kuhalalisha umiliki huo au vinginevyo.
Kutokana na Kifungu cha 87(1) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura ya 283 Wizara inamtaka mtu yeyote atakayeona nyara za serikali zikimilikiwa na mtu asiyehusika, au asiyekuwa na kibali, kutoa taarifa kwa kwenye ofisi za Maliasili, Wanyamapori au Polisi.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na:-
Mkurugenzi,
Idara ya Wanyamapori
S. L. P 9372
Dar es Salaam
{MWISHO}
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
7 Aprili 2012
Sungura naruhusiwa kumiliki? au na yeye mpaka kibali?
ReplyDeletena hao wanyama mnauza nje ya nchi kila siku inakuwaje??
ReplyDeleteje waweza kutofautisha mfupa wa swala na mbuzi? au mtafanya DNA test
ReplyDeleteKucha na Pembe za wanyama! - Duh! - Naona Serikali imeanza kuwaandama Waganga wa Kienyeji pamoja na Wachawi! - maana wao ndio huwa wanatumia kucha na mapembe kwenye shughuli zao
ReplyDelete