Ndugu zangu,
Msanii Remmy Ongala alipata kuimba;
" Ukiwa na roho mbaya,kweli tutakuogopa,
Ukiwa na roho mbaya, huko unakokwenda nako ni kubaya!"
Siku zote, mwanadamu usijaribu kufanikiwa maishani kwa kuwa mbaya kwa wengine. Ndio, kuna waliofanikiwa maishani kwa kuwa wabaya kwa wengine.
Siku zote, mwanadamu aliyefanikiwa kwa kuwatendea maovu wanadamu wenzake hawezi kuwa ni mtu mwenye furaha na amani maishani. Ataandamwa na jinamizi la maovu yake mpaka atakapoingia kaburini.
Je, mwanadamu huyo afanye nini?
Ajitazame mwenyewe. Aache kuendelea kuwatendea mabaya wengine katika kiu yake ya kukifikia ’ kilele cha mafanikio’- kama kweli kipo humu duniani! Hivyo basi, mwanadamu huyo atakuwa amejitambua. Na kwa vile naye ni mwanadamu, basi, hakuna mwanadamu asiyetenda makosa.
Dhambi kwa mwanadamu huyo itakuwa ni hulka yake ya kuendelea kuwakanyaga wanadamu wenzake katika juhudi za kuyafikia mafanikio yake. Misaada kwa yatima na masikini haitasaidia kuzifuta dhambi zake, maana, amezifanya na bado anaendelea kuzifanya.
Je, kwanini mwanadamu anakuwa ni mtenda maovu?
” Kwenda huko, utakufa kwa roho yako mbaya!”. Hiki kilikuwa ni kibwagizo katika moja ya matangazo ya kijamii redioni miaka ya karibuni.
Nilipata kumwuliza msanii Mrisho Mpoto swali la kifalsafa; ”Je, binadamu tunakufa kwa roho mbaya au roho chafu?”
Mpoto ananijibu: ” Kaka Maggid, naiona mantiki ya swali lako. Kama nitakunjua viganja vyangu na kuitema roho yangu kisha nikaiangalia... lakini fafanua kwanza fikra zako.”
Nikafafanua, kuwa binadamu hatukuumbwa kuwa wengine wana roho mbaya na wengine nzuri. Sote tumeumbwa na roho nzuri isipokuwa mazingira ndio yanayotufanya wengine tukawa na roho chafu na wengine roho safi. Ndio, roho nzuri tulizoumbwa nazo zinachafuka. Tunakuwa ni binadamu wenye roho chafu. Na hakika, Watanzania wengi tunakufa kutokana na roho chafu, zetu wenyewe au za wenzetu.
” Mh!” Anaguna Mrisho Mpoto. Ananiacha niendelee.
Maana, ni mtu mwenye roho chafu tu anayeweza kujaribu kuyazuia mabadiliko yatakayomsaidia mwanadamu mwenzake atoke mahali alipo na apige hatua itakayomsaidia maishani.
Ni mtu mwenye roho chafu tu atakayeweza kuhujumu mradi wa kuangamiza Malaria inayosababisha vifo vya maelfu ya watoto na watu wazima ili apate mafanikio binafsi.
Ndio, kuhujumu mradi wa kuzuia malaria ili apate fedha za kufanya mambo ya fahari au hata kununua uongozi wa kisiasa au kuendelea kubaki madarakani.
Kwa mwanadamu, ni heri ufe kwa kupambana na anayehujumu mradi wa kuangamiza malaria kuliko kufa kwa malaria inayotokana na mbu anayesababisha malaria.
Naam, You do not win by being bad. Utakwama njiani. Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
Ni kweli kabisa naungana na wewe kwa usemi huo, roho mbaya haijengi na malipo yake utajutia sio duniani tu hata akhera
ReplyDeleteNdugu Mjengwa,
ReplyDeleteSawa kabisa maneno yako ni kweli tupu sababu kubwa ni kuwa ktk idadi kubwa ya watu 'well wishers are few than bad wishers' yaani 'wakuombeao mema ni wachache zaidi kuliko wasiokutakia mema'.
Ndio maana wengi wetu wamekuwa na nia njema na mambo mengi lakini wamekuwa wakikwamishwa na watu wa namna hii.
Mara zote unapoleta wazo endelevu hutokea wakwamishaji hata kama huyo mkwamishaji iwe ana manufaa au hana manufaa yeyote na huo mpango ili mradi afikie lengo tu la kuifurahisha nafsi yake.
Mambo gani haya ya mianaume kushikana mikono? huu ndio ushoga au?
ReplyDeleteBi Aisha
Bi Aisha,
ReplyDeleteACha kuiga mambo ya ulaya,sisi wanaume waafrika kama ni marafiki wala hakuna noma kushikana mikono, ughaibuni ndo noma wanaume kushikana mikono, tusiige kila la mile na desturi za wazungu wajameni, naishi ughaibuni mwaka wa ishirini saa, na sioni tatizo lolote kwa wanaume marafiki wa kibongo kushikana mikono.
Asante sana kwa ujumbe wa maneno mazito kwani yamewalenga wahusika wote.Nchi yangu Tanzania yoyote mwenze sitisha maendeleo ya Umma ili apate mwenywewe basi Umma hauta sita kumng'oa kama sio leo basi kesho.Bora tufe kutetea haki zetu kuliko kufa kwa njia iliyosababishwa na wenye tamaa.Tutakung'oa tu muda si mrefu bora ubadilike kwani mtnzania ana huruma ya kusamehe endapo ukimtendea haki
ReplyDeleteBi Aisha Anonymous wa Wed Apr 04, 03:55:00 PM 2012
ReplyDeleteWewe kwa dalili za haraka utakuwa ni Mwislamu hata Dini zingine zinasisitiza Mshikamano na ndio dalili za kupeana mikono.
Hakuna ubaya kwa wanaume kupeana mikono isipokuwa kama utapeana mikono na mwanamke au binti usiye kuwa na uhalali naye ndio patakuwa na walakini na zaidi ya kupekecha mikono au vidole vya mwanamke au binti,,,ni dalili mbaya!.