Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema iko tayari kushirikiana na Mfuko wa Taifa  wa Bima ya Afya (NHIF) katika uhamasishaji wa wananchi  kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote.

Akizungumzia umuhimu wa kujiuga na utaratibu wa bima za afya, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa alipotembea ofisi za NHIF, Dar es Salaam jana, alisema akiwa kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Ruangwa atahakikisha anakutana na makundi mbalimbali na kuyaeleza umuhimu wa kuwa ndani ya utaratibu wa CHF.

"Kwa kweli kazi mnayofanya ni kubwa katika kuboresha huduma za afya kwa wanachama wenu na kwa wananchi wa kawaida, nimefurahishwa sana na utaratibu wa kutambua kundi la waendesha piki piki na makundi mengine, hawa mtaji wao ni afya yao hivyo wakiwa na uhakika wa matibabu watafanya kazi zao za kujiingia vipato kila kukicha," alisema Majaliwa.

Akizungumzia hospitali ya Wilaya ya Ruangwa, alisema kuwa bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa vifaa tiba kama x-ray na vingine hali inayosababisha usumbufu kwa wagonjwa kwa kulazimika kwenda umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.Kutokana na hali hiyo, aliuomba Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuiangalia hospitali hiyo kwa jicho la pekee na kuipa kipaumbele katika fursa ya Mikopo ya Vifaa tiba na Ukarabati wa majengo ili iweze kuwa bora na kutoa huduma stahili kwa wananchi wa jimbo hilo.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa NHIF, Hamis Mdee, alisema kuwa, Mfuko umekuwa ukifanya mambo mbalimbali yanayolenga moja kwa moja kuboresha huduma za matibabu vituoni hivyo suala la fursa ya mikopo hiyo litafanyiwa kazi baada ya kupokea maombi kutoka Hopsitali hiyo.

"Sisi lengo letu ni kuona wanachama wetu wa NHIF, CHF na wananchi kwa ujumla popote walipo wanapata huduma bora hivyo nasi tutahakikisha tunalifanyia kazi baada ya kupokea maombi na uzuri wa mikopo hii inalipwa kwa makato ya madai ambayo wanachama wetu wametibiwa," alisema Mdee.

Wakati huo huo, sekondari za bweni mkoani pwani zimetakiwa kuwaandikisha wanafunzi wao katika mfuko wa afya ya jamii ili waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na mfuko huo.

Afisa anayeshughulikia huduma za mfuko kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF   Rehani Athumani ametoa wito huo alipokutana na wadau wa  wadau wa sekta ya elimu waliokutana mjini Kibaha kutathimini matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2011.

Rehani amesema, utaratibu wa kuwajumuisha wanafunzi umefanywa kuwa rahisi kwa sababu wanafunzi hao wanatakiwa kuchangia kati ya shilingi 1,000 mpaka 2,000 kwa mwaka hiyo kwa kuwawezesha kupata matibabu mwaka mzima.

Amesema utaratibu wa sasa wa kutoa fedha za tahadhari umekuwa na changamoto kadhaa ikiwemo kukosekana kwa uhakika wa huduma za matibabu kwa wanafunzi husika.

Naye mkuu wa mkoa huo Mwantum Mahiza amezitaka mamlaka za Halmashauri kutumia fursa ya fedha ya tele kuboresha huduma ikiwemo kuwasilisha madai ya kuomba fedha hizo NHIF mapema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...