Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Lawrence Gama akifungua rasmi Mkutano wa Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) wa Mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika jana katika ukumbi wa Uhuru Hotel.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Hamis Mdee akitoa maelezo ya Utangulizi juu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii wakati wa Mkutano wa wadau wa NHIF na CHF mjini Moshi.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali Mama Mwanaidi Mtanda akiongea wakati wa Mkutano wa Wadau wa NHIF na CHF Mjini Moshi.
Mkuu wa Wilaya ya Same Bw. Marwa kama mdau mmojawapo wa NHIF, akichangia mawazo juu ya kuboresha huduma za CHF katika Halmashauri za Kilimanjaro katika Mkutano wa Wadau wa NHIF uliofanyika Mjini Moshi.
Wadau mbalimbali wa NHIF na CHF wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwakilishwa katika Mkutano wa wadau wa Mifuko hiyo mjini Moshi. Mkutano huo ulijumuisha wadau wapatao 280 kutoka wilaya zote za mkoa huo ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa na majadiliano yalifanyika juu ya majukumu mbalimbali ya wadau wa NHIF na CHF na jinsi ya kuboresha huduma hizo.
Katika muendelezo wa utaratibu wa kukutana na wadau wake Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) jana umefanya Mkutano wa Wadau wake wa Mkoa wa Kilimanjaro. Mkutano huo ambao ulijumuisha wadau wapatao 280 kutoka Halmashauri zote za Mkoa huo ulifunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Lawrence Gama.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Bw. Gama aliipongeza NHIF kwa utaratibu wanaoufanya wa kukutana na wadau wake mikoa yote ili kuweza kupata mrejesho kutoka kwa wadau juu ya huduma za Mifuko ya NHIF na CHF na kujadili na wadau hao jinsi ya kuboresha huduma hizo ikiwa ni pamoja na kubainisha majukumu ya kila mdau katika kufanikisha hayo.
Ukitoa hotuba yake Bw. Gama aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ambayo imeweza kuwahimiza wananchi wake katika suala zima la afya zao na asilimia 90 wa wananchi wa Rombo wamejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa alibainisha kwamba kimkoa bado wananchi hawajahamasika vya kutosha na bado jitihada za makusudi zinatakiwa. “ Kama Rombo wameweza, kwa nini Halmashauri nyingine zishindwe, nataka niwahimize Viongozi wa Halmashauri nyingine wajifunze kutoka kwa Halmashauri zilizofanikiwa kama Rombo na Kahama ili nao waweze kufanikisha suala hili”
Kuhusiana na malipo ya Serikali kwa huduma za afya kwa Halmashauri (Tele kwa Tele), Mkuu wa Mkoa alionyesha masikitiko yake kwamba kumekuwa na kusuasua kwa uwasilishaji wa maombi ya Tele kwa Tele na Halmashauri za Wilaya za mkoa huo na imepelekea kuambulia malipo ya asilimia 9 tu ya Shilingi 3.5 bilioni ambazo Serikali ililipa kwa Halmashauri nchini kati ya Desemba 2009 na Juni 2011. Aliwahimiza Viongozi wa Halmashauri kufahamu kuwa jinsi wanavyohimiza watu kujiunga na CHF ndivyo wanavyoweza kupata fedha za tele kwa tele kutoka serkalini kwa wingi zaidi na kuwa na uwezo wa kuboresha huduma za matibabu katika halmashauri zao na hasa huduma za dawa. Alisema katika asilimia 9 zilizolipwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro, asilimia 79 ilikwenda Halmashauri ya Rombo kwa kuwa wamekuwa wakifanya vizuri.
Pamoja na hayo Mh. Gama aliwaagiza Wakaguzi wote wa Halmashauri kukagua mapato na matumizi ya fedha zote za Afya ikiwa ni pamoja na zinazokusanywa kutoka kwa wanachama wa CHF, malipo ya NHIF na fedha za Tele kwa Tele na taarifa kufikishwa kwake kwa wakati.
Kwa upande wake Meneja MSD Kanda wa Kilimanjaro ikijibu hoja zilizotolewa na wadau kuhusu suala la Uhaba wa Dawa katika vituo vya afya alieleza kuwa dawa imekuwa ni tatizo kwa nchi nzima lakini alihimiza kujifunza kutoka halmashauri ambazo zinafanya vema katika suala la dawa kuwa wao badala ya kusubiri fedha za Serikali kwa ajili ya mgao wa dawa wamekuwa wakitumia fedha zinazokusanywa kwa ajili ya afya katika halmashauri zao kununua dawa MSD na endapo kuna upungufu MSD wamekuwa wakinunua kutoka vyanzo vingine binafsi ili kukidhi uhitaji huo katika Halmashauri zao.
Akifunga rasmi Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Siha Bi. Anna Nyamubi kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo aliwataka wadau wa Mfuko kutumia nafasi zao kuhimiza wananchi kujiunga na Mifuko ya Afya ya Jamii ili waweze kufaidika na huduma za matibabu katika Halmashauri zao. Wakifikia mwisho wadau walikubaliana juu ya maazimio mbalimbali ya kuboresha huduma za Afya katika Mkoa huo na kila mdau akijua majukumu yake.
Is this Laurence or Leonidas Gama...!?!
ReplyDeleteEddy
Vancouver