Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar  
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiifungua Semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusiana na Masuala ya Sensa ya Watu na Makazu. Semina hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amewataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kuchukua jukumu la kuwaelimisha wananchi wao kuhusu kushiriki kikamilifu katika Sensa ya watu na makazi ambayo inatarajiwa kufanyika Agasti 26 mwaka huu.

Amesema kama Wajumbe hao watawaelimisha vyema wananchi katika Majimbo yao ni dhahiri kuwa maafisa sensa watakuwa na kazi rahisi ya kutekeleza majukumu yao siku hiyo ya sensa itakapofika.

Balozi Seif ameyasema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Semina kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu hali halisi ya maandalizi ya Sensa ya watu na makazi iliyofanyika leo Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Amesema lengo kuu la Sensa ya mwaka 2012 ni kuchangia katika uboreshaji wa maisha ya Watanzania kwa kutoa takwimu sahihi na zinazoendana na wakati kwa ajili ya kutunga sera,kupanga mipango ya maendeleo,uboreshaji wa huduma za jamii pamoja na ufuatiliaji na kutathmini utekelezaji wa programu mbalimbali zinazohusiana na maendeleo.

Balozi Seif amefahamisha kuwa Sensa ya mwaka huu itakuwa na umuhimu wa kipekee kulinganishwa na zilizopita kwavile itatoa viashiria vingi vitakavyotumika katika kutathmini programu muhimu za maendeleo kama vile MKUKUTA ,MKUZA,Dira za Maendeleo 2025 kwa Tanzania Bara na 2020 kwa Tanzania Zanzibar.

Viashiria vingine ni pamoja na kujua idadi ya watu kimakazi,ukubwa wa nguvu kazi,idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi, viwango vya uzazi,wastani wa kuishi kwa Mtanzania,idadi ya watu wanojua kusoma na kuandika na idadi ya watoto walioandikishwa Skuli mambo ambayo yataisaidia Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee amesisitiza haja ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuelewa vyema faida za Sensa ili wao waweze kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi wao pale ambapo wataenda kuwaelimisha.

Amesema ufahamu mzuri wa Wajumbe hao juu ya faida zinazopatikana kutokana na Sensa utachochea ari na hamasa kwa wajumbe hao kulifanya zoezi zima la Sensa kuwa ni wajibu kwao na jamii kwa ujumla.

Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Wajumbe hao amesema ni vyema pia ikaeleweka wazi kwamba Usiku wa Sensa utakuwa ni mmoja tu wa kuamkia Agasti 26 lakini zoezi la kuhesabiwa watu litachukua wiki moja.

Mzee amesema utaratibu wa Sensa ni kila Mtanzania anatakiwa ahesabiwe na kuchukuliwa maelezo yake pale alipoamkia siku ya Agasti 26 mwaka huu ambapo pia alitoa wito kwa watanzania kuifanya siku hiyo ni muhimu kwao na hivyo kushiriki kikamilifu.

Katika Semina hiyo ambayo ilishirikisha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Maafisa wa Sensa, wajumbe hao wa Baraza walipata fursa ya kuuliza maswali mbali mbali na kujibiwa

Sensa ya Watu na Makazi ambayo inatarajiwa kufanyika nchi nzima Agasti 26 mwaka huu inatarajiwa kugharimu Shl.Bilioni 141.5 hadi kukamilika kwake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...