Ndugu zangu,

Unaweza kuwatawanya watu kwa mabomu , lakini kamwe, mabomu hayawezi kuitawanya mioyo ya watu yenye kutaka mabadiliko.

Habari kubwa usiku wa kuamkia leo ni anguko la CCM kule Arumeru Mashariki kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha Ubunge.

Tafsiri yangu;
Kuna wakati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alipata kutamka; " CCM haina hati miliki ya kutawala". Mkapa aliusema ukweli wake ambao kwa bahati mbaya hupata tabu kuusimamia. Na hakika, idadi ya Watanzania wenye kutaka mabadiliko inazidi kuongezeka. Na katika siasa za nchi hii ukiona wanawake watu wazima wanashiriki mikutano ya kampeni ya wapinzani, basi, ujue ni ishara ya mabadiliko yanayokuja.

Na ukweli mwingine ni huu; vijana wengi zaidi wamekuwa mstari wa mbele katika kutaka mabadiliko hayo. Kimsingi Arumeru Mashariki wamechagua mabadiliko. Na si kwamba Chadema ni chama bora na makini sana, la hasha, Watanzania wengi zaidi vijana wanaonyesha kuichukia CCM. Miongoni mwao ni Wana-CCM. Kiukweli, mvuto wa Chama Cha Mapinduzi kwa Watanzania na hususan vijana unazidi kupungua.

Na ajabu ya matokeo ya Arumeru?
Katika hali isiyo ya kawaida, kuna Wana- CCM waliyoyapokea kwa furaha matokeo ya chama chao kushindwa Arumeru. Tafsiri yake? Ni kushamiri, si tu kwa makundi ndani ya chama hicho, bali, hofu ya kutokea kwa mpasuko ndani ya chama hicho katika mbio za kuusaka Urais ifikapo mwaka 2015.

Kitakachotokea sasa ndani ya chama hicho ni ‘ Witch hunting’- kutafutana uchawi. Bila shaka, kuna maswali yatakayoulizwa. Moja kubwa ni hili; kimeshindwa chama au mgombea? Na msukumo wa swali hilo ni katika kumtafuta mchawi na kukitenganisha chama na mgombea katika ‘Anguko la Arumeru’. Huo utakuwa ni mwendelezo wa ‘ Vita vya Panzi’ ndani ya CCM. Lakini, katika siasa, kuna wanaoamini pia, kuwa wakati mwingine kuna lazima ya kuwepo kwa ‘ Vita vya Panzi’ ili kujitenganisha na kumbikumbi.

CCM ifanye nini?

Jibu; ifuate njia ya Dr Harrison Mwakyembe
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya Ipinda hivi majuzi Dr Mwakyembe alitoa kwa watu wake kauli ya ‘ Kichifu’ na iliyojaa hekima na busara. Alisema; “ Mimi sikubaliani na mtu yeyote anayesema kitu cha kwanza ni chama chako…. Hapana, mimi kitu cha kwanza kwangu siyo CCM , cha kwanza mimi ni Mtanzania, cha pili ndio tunaingia kwenye vyama. Mtu anayekimbilia chama kuwa cha kwanza hivi hicho chama kingetokea wapi kama siyo taifa?”. ( Dr Harrison Mwakyembe, Nipashe, Machi 31, 2012)

Na nilimwona na kumsikia Dr. Mwakyembe akiyasema hayo kwenye runinga. Umati ule uliomshangilia Dr Mwakyembe ulikuwa wa wananchi bila kujali itikadi zao. Kulikuwa na Wana -Chadema pia, na kiongozi wa Chadema alipewa kipaza sauti kuongea kumkaribisha ‘ Chifu Mwakyembe’ aliyerudi nyumbani na mtazamo mpya wa kizalendo.

Kuifuata njia ya Mwakyembe itawasaidia CCM kurudisha umaarufu wao. Maana, moja ya sababu za wananchi walio wengi kuichukia CCM ni hulka yake ya kuwabagua wapinzani na kuwaona ni watu wasiofaa kushiriki uongozi wa nchi.

WaTanzania wengi sasa wanatambua, kuwa si kweli wapinzani ni watu wabaya. Ni maadui. Kwamba watasababisha vita na vurugu. Wananchi wameona pia kazi njema inayofanywa na upinzani. Ghiliba hii ya CCM kuwachonganisha wapinzani kwa wananchi imepitwa na wakati. Badala yake, inachangia kupunguza kura za CCM.

Na CCM isipobadilika sasa, na Chadema ikabaki kama ilivyo sasa bila kusambaratika, basi, CCM itakuwa na wakati mgumu sana ifikapo 2015, maana, kuna ‘Jeshi kubwa’ la vijana linalojiandaa na kushiriki uchaguzi wa 2015. Jeshi hili linaundwa na vijana wengi wasio na ajira wala hakika ya maisha yao ya kesho. Wanaiona CCM kama sehemu ya matatizo yao. Wana kiu ya kumpata mkombozi.

Na wanafunzi hawa wa Shule za Kata wamegeuka kuwa ‘ agitators’ wazuri wa mabadiliko. Ikumbukwe, shule za kata ziko vijijini. Siku hizi hata waliokuwa wakiitwa ‘ wajinga’ wa vijijini wamepata walimu wa kuwafungua macho. Watoto wao wenyewe wanaosoma au waliomaliza shule za kata na kubaki vijijini kwa vile hata uwezo wa kujisomesha elimu ya juu hawana. Hawa hawana mapenzi na CCM.

Na katika vijana mia moja hii leo, utapata kazi kubwa kuwapata 20 wanaoipenda CCM. Huu ndio ukweli wa hali halisi. CCM ibadilike na kuwa chama cha kisasa kilicho tayari hata kuongoza nchi pamoja na wenzao wa upinzani. Yumkini jitihada za CCM kuangamiza upinzani zaweza kuwa na madhara makubwa endapo CCM itapata bahati mbaya ya kuondolewa madarakani 2015. Maana, anguko hilo laweza pia kumaanisha kifo cha chama hicho.

CCM haipaswi sasa kufikiria mikakati ya kuangamiza upinzani ili watawale daima. Dhana ya ’ CCM Daima’ ni ndoto iliyopitwa na wakati. Katika Tanzania ya sasa kuna wengi wenye kuombea kubaki hai na kushiriki kuzifuta ndoto kama hizo.

CCM ya sasa inapaswa kupanga mikakati ya kuendelea kuongoza dola huku ikishirikiana hata na wapinzani. Ingawa hata huo ni mtihani mgumu wenye kukihitaji chama hicho kuwa na watu makini zaidi badala ya waendekeza fitina na majungu.

Na hii ni tafsiri yangu.

Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 27 mpaka sasa

  1. ninakubaliana na tafsiri yako isipokuwa unaowaeleza wana pamba masikioni na wamevaa miwani ya mbao.And for sure time will tell,CCM will not survive in power beyond 2015.

    ReplyDelete
  2. wameweka pamba masikioni na wamevaa miwani ya mbao.They will understand when it is too late,2015 is the end of CCM

    ReplyDelete
  3. kimsingi mjengwa ameona mbali sana katika hili basi ankal nawe pia jitahid kuuelimsha umma pamoja na uongozi wa taifa letu, kuwa upinzani si uadui bali ni kioo cha kuangalia makosa ndani ya uongozi na kuondoa udikteta. naongezea kwa kusema kitendo cha wanavyuo vikuu kuwekewa masharti magumu likiwemo la vyuo vikuu kufungwa kipindi cha uchaguzi mkuu 2010 kuna kitu kibaya kimepandwa na matokeo yake tutayaona kwenye uchaguzi ujao.Nasikitika kwamba chama tawala kimekosa meno kwa kuwa na sera madhubuti zitakazoweza kuwashawishi wananchi wakarudisha imani ndani ya chama na serikali yake.issue za UFISADI wa EPA,RICHMOND, MIKATABA MIBOVU YA MALI ASILI ZA WATANZANI YENYE NANUFAA KWA MINORITY NA SI MAJORITY,KUUZWA KWA MBUGA YA LOLIONDO na mengine mengi vimefanya watu waichukie serikali pamoja na chama. matumizi ya nguvu na pesa haviweza leta mvuto kwa wananchi kamwe.

    ReplyDelete
  4. Kaka mimi nakubaliana na wewe. Ila si kwamba watu wanaichukia CCM, la hasha ila kinachochukiwa ni hiki kilichojitokeza siku hizi kuwa viongozi wa CCM walioko madarakani wanakosa na hawachukuliwi hatua yoyote. Hili ndio jambo linalowachukiza watanzania. Kila unapouliza unaambiwa pale hawezi kuchukiliwa hatua kwa sababu hizi na hizi. Ukishaona mmefikia hapo ujue hakuna serikali. Hata wazee hawadanganyiki tena na zile hoja za nchi ya amani. HATUDANGANYIKIII!

    ReplyDelete
  5. Umeichambua vyema hii makala yk bro! nakumbuka Mhe; Mkapa, wakati wa utawala wake alitumia, every resorces kuingusha CUF na Mhe Mrema, kokote alikokwenda, hivi sasa wale waliokuwa wakitishwa kuwa wapinzani ni watu wabaya ndy hao leo wanaoiona CCM ndy Adui namba Moja!

    ReplyDelete
  6. Mjengwa amesema kweli kabisa katika hili.

    Watu wote wanaichukia CCM sana. Watu pekee wanayoipenda ni wenye Mikakati binafsi ya kifisadi.

    Sioi hana kosa lolote. CCM ndiyo Inayochukiwa na imemsababishia kuukosa ubunge

    ReplyDelete
  7. Hilo ni anguko la ccm,

    wajitathimini wapi wanakosea wapi wanaende vizuri. Watu wamechoshwa na kauli za mapambano wanapamba na nani!! wakati sisi tumewapa ridhaa watuletee maendeleo!!!

    ReplyDelete
  8. Bwana mjengwa umesema ukweli mtupu. Umefanya uchambuzi nmzuri sana ambao pia unaweza kuwasaidia ccm kama watauchukulia positive. Ni lazima ccm wajue kuwa watanzania wa leo si wa kuburuzwa na kudanganywa tena!

    ReplyDelete
  9. AHSANTE NDUGU MDAU MAGGID MJENGWA!

    Kwa kweli taarifa ya anguko la CCM imeniuma saaana hasa ukizingatia Tafsiri anayotoa ndugu yetu Mjengwa hapa kwa ufupi:

    1.Kuacha dhana ya kuua Upinzani na badala yake kufanya Siasa za Ushindani.

    2.Ni kweli kabisa kuwa CDM imeshinda isipokuwa ina mapungufu mengi ingawa imebebwa na ile dhana ya watu ile tu kutaka mabadiliko.

    3.Uzalendo KWANZA!,,,Ni muhimu kuzingatia uzalendo zaidi kuliko kutetea Itikadi !

    Uwezekano wa CCM kutawala daima upo endapo mabadiliko ya dhati yatafanyika sio 'kuvua gamba' kinadharia wakati kiuhalisia Chama kingali na Koo za Kifalme na Tawala za Kiukoo !

    ReplyDelete
  10. Mjengwa nakubaliana na wewe, tulikuwa tukifundishwa kuwa ili tuendee tunahitaji vitu vitatu, watu, siasa safi na uongozi bora. Now hakuna kiongozi wa ccm au serikali mwenye uwezo wakutamka kauli mbiu hii. Wananchi sio kama wanaichukia ccm moja kwa moja bali matendo ya viongozi wa ccm ndiyo vinapelekea wanachi kuanza kuichukia ccm.

    Kwa mfano, wananchi wanajua kiongozi fulani amekosea,badala ya kuchukuliwa hatua utasikia tupo kwenye mchakato, uchunguzi unaendelea n.k lakini wanachi hata wasio na hatia huadhibiwa.

    Viongozi wa serikali ambao wanatokana na ccm, wamefanya nchi ni mali yao na familia zao. Kiongozi gani aliyesaini mikataba mibovu leo yupo jela? Kamati ya Mrema imegundua ubadhilifu wa fedha za halmashauri, viongozi wapi waliochkuliwa hatua mpaka sasa?

    Kibanga Msese

    ReplyDelete
  11. Huyo mzee uliyempiga picha hachagui sera anachagua chama. Wanachama wengi wa CCM, CHADEMA na CUF wanachagua chama kwanza sera au kiongozi baadae!!

    ReplyDelete
  12. Majjid nakubaliana nawe na uliyosema,kweli wakati umefika kwa chama tawala na vyama vyote vya kisiasa kuuacha SIASA ZA CHUKI kama tulivyoshuhudia ARUMERU.Matusi,kejeli na UONGO wa viongozi ndiyo kampeni ilivyokuwa Arumeru,ambapo suala la kutatua matatizo ya wananchi halikutiliwa maanani.Kwahiyo kuanguka kwa CCM Arumeru wakulaumiwa ni viongozi wa CCM waliopanda jukwaani na kuongea UPUUZI na UONGO ambao wananchi wamechoka nao kwa miaka mingi.

    ReplyDelete
  13. CCM wanapaswa kuufuata ushauri huu uliotolewa hapa haraka sana, wanahitaji kufanya U -turn haraka ya jinsi wanavyoendesha mambo yao, wasipofuata ushauri huu wa bure, ifikapo 2015 wasimlaumu mtu kwa lolote litakalotokea. Shida ni kwamba hawatafuata ushauri huu

    ReplyDelete
  14. SIKIO LA KUFA HASIKII DAWA!

    ReplyDelete
  15. HONGERENO CHADEMA KWA USHINDI, TATIZO LA CCM HAWANA UTAMADUNI WA KUSIKILIZA USHAURI, WANAPASWA KUTUMIKIA UMMA NA SIO MASLAHI BINAFSI, KILICHOWAANGUSGA ARUMERU NI MASLAHI BINAFSI

    ReplyDelete
  16. Na bado, yote tisa, kumi 2012

    ReplyDelete
  17. CCM bila kuvua gamba(kiukweli) CHADEMA itawatesa CCM kila siku - and this is just an alarm for CCM

    ReplyDelete
  18. Kudos to chadema and a wake up call for CCM

    ReplyDelete
  19. Zama za Siasa za umwamba na mabavu zimeisha !

    Hivi sasa ni Siasa za Sera na Uenezi Halisi sio wa Kimipango mipango na Kiusanii.

    Yamefanyika makosa makubwa sana kufanyika mizengwe hadi kuachwa kwa SARAKIKYA !

    ReplyDelete
  20. DUA ya mtu mzima hairudi bila majibu !

    ReplyDelete
  21. Ndugu Mjengwa ahsante sana !

    Imekuwa ni vizuri sana makala hii makini inatoka katika Fikra zako wewe ambaye tunakuelewa ni Kada Mzuri sana wa Chama Tawala.

    Kwa kweli nimeipenda aina yako ya Msimamo wa Kisiasa zaidi kwa kuukubali uhalisia wa mambo na mustakabali wa yaliyojiri hasa Arumeru Mashariki.

    Kwa kweli ni wachache sana miongoni mwa Makada wa vyama ambao wanaweza kuukubali ukweli wa mambo kama ulivyo tuchambulia ktk Makala yako adhiimu.

    Ahsante saana !

    ReplyDelete
  22. CCM kumbukeni kila kitu kina mwanzo na mwisho lleo hii yko wpi gadafi ylo wpi sadam hitlana wengine wengi ambao walijifanya wao ndo mihungu watu ivi ni kweli viongozi wa CCM hawajui kuwa wananchi wanatabika kwa ajira maji umeme hospital bara bara mbovu na wao ndo wakwanza kujirimbikidhia mali watu wamechoka na maisha ni magumu sna kiukweli mwaka 2015 watakuwa na kazi ngumu sna mana sijui watamsimamisha nani mana wote wanadosali ninauwakika hakuna tena mtz mwenye himani na ccm pamoja na viongozi wao

    ReplyDelete
  23. Mwakyembe anaposema yeye ni Mtanzania kwanza, halafu ndio chama. Ilo wazo wengi tumekuwa tukilipigania sana kwenye katiba mpya, wagombea wa kujitegemea. Hapo waTanzania wanachagua viongozi wao wenyewe na wala si chama. Tatizo lipo sasa unapoona chama kinamufukuza mmbunge na wanataka afukuzwe ubunge wakati yeye ni kiongozi wa waTanzania na si chamapekee.

    ReplyDelete
  24. HONGERA MABADILIKO! BINAFSI SIIPENDI CHADEMA ILA NAPENDA KUONA HALI ILIOKO SASA INABADILIKA. NA KWA KUWA CHADEMA NDIYO IMEHUSIKA BASI ACHA NISEME HONGERA CHADEMA NA NASARI. BINAFSI NAFURAHI SANA KUONA MTU ALIEPIGIWA KAMPENI NA MIONGONI MWA VINARA WAWILI WA UFISADI NCHINI AMSHINDWA!

    NIMEFURAHHI SANA

    ReplyDelete
  25. 52.4% ya waliojiandikisha hawakupiga kura yaani kati ya watu 127453 ni 66785 hawakupiga kura ni suala la aibu sana kusema Tanzania kuna TUME YA UCHAGUZI. Kwa mjinga kamamimi nashawishika kusema kwamba kwa kiasi kikubwa hao waliosemwa na tume kwamba hawajajitokeza ni mkakati maalum lio na lengo la kupunguza tofauti kubwa ya kura kati ya Sioi na Josh lengo ni kuficha aibu walioipata vinginevyo sioni sababu ya walio kwenye tume hii kuendelea kuwapo kwenye nyadhifa zao huku wakionesha dhahiri kushindwa majukumu yao. Haiingii akilini watu asilimia 47.6 tu ndio wajitokeze mimi sikubaliani na hili. Japo nakubaliana na ushindi wa CDM. Hongereni wana Arumeru japo uhuni ulitaka kuwanyima haki yenu

    ReplyDelete
  26. MIMI CCM WA NGUVU BW SIOI NA WANA CCM WENZANGU TUMEPATA ASILILIMIA 42 YA KURA TUNAKUBALIKA!! TUJIPANGE VIZURI 2015 SI MBALI CCM OYEE, SIOI OYEE!

    ReplyDelete
  27. dalili ya mvua ni mawingu...na chelea chelea utakuta mwana si wako..CCM ndio hivyo tena bye bye 2015 ndio mwisho wao tumeona imetokea Zmbia,Malawi nk so haitakua ajabu kutokea bongo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...