Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akiwa pamoja na msaidizi wake, Naibu Katibu Mkuu Asha-Rose Migiro na Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Balozi Csaba Korosi akizungumza na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa hawapo pichani. katika mazungumzo hayo yaliyofanyika siku ya jumatano, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alieleza masuala mbalimbali yakiwamo ya hali tete za kisiasa nchini Syria, Mali, Guinea Bisau, mapigano kati ya Sudan ya Kusini na Sudan, maandalizi ya mkutano wa kimataifa wa maendeleo endelevu na mazingira maarufu kama RIO+20 unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao huo Rio de Janairo, Brazil. Na ziara za kikazi alizofanya nchini India na Myanmar.
Na Mwandishi Maalum,New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amelaani vikali shambulio la mlipuko uliotokea siku ya jumatano katika kizuizi karibu na mji wa Dar’a kusini mwa Syria, muda mfupi baada ya msafara wa waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa kupita.
Akizungumza na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amesema tukio hilo linatakiwa kulaaniwa na jumuia yote ya kimataifa na ni kielelezo cha dhahiri kwamba hali nchi Syria inazidi kuwa mbaya.
“ Ninalaani kwa nguvu zangu zote tukio hili, ni tukio ambalo halikubaliki, linatakiwa kulaaniwa vikali na jumuia yote ya kimataifa. Hiki ni kielelezo cha wazi cha namna gani waangalizi wetu wa amani wanavyokabiliwa na mtihani mkubwa, lakini pia ni kielelezo cha hali halisi ya kile kinachowasibu wananchi wa Syria kila siku”. Akasema Katibu Mkuu.
“ Nimeongea na Meja Jenerali Robert Mood, mkuu wa Misheni ya Usimamizi wa Amani ya Umoja wa Mataifa nchini humo ( UNSMIS) amenipa taarifa kamili ya nini kilichotokea. Hakuna aliyejeruhiwa kufuatia mlipuko huo au uharibifu kwa magari ya Umoja wa Mataifa ingawa kulikuwa na majeruhi kwa upande wa askari kumi wa Syria waliokuwa wakisindikiza msafara huo” akafafanua Ban Ki Moon
Katika mazungumzo hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Asha-Rose Migiro, Katibu Mkuu ameelezea kwamba kuendelea kutokea kwa milipuko hiyo anapata wasiwasi mkubwa wa uwezekano wa kutokea kwa vita kamili ya wenyewe kwa wenyewe nchi humo ikiwa pande mbili zinazohusika hazitaweka silaha zao chini, kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo ya amani.
Akawasihi sana mabalozi hao kuunga mkono juhudi za mjumbe maalum Bw. Koff Annan za kujaribu kurejesha amani nchi Syria na vile vile kuunga mkono upelekekaji wa waangalizi wa amani 300.
Aidha akatumia mazungumzo hayo kuzishukuru nchi 38 ambazo zimekubali kutoa wanajeshi wa kwenda kuangalia amani nchi humo.
“ Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa nchi 38 ambazo zimeonyesha nia ya kutoa watu wao kwenda kusaidia kuangalia amani nchini Syria, natambua uzito wa jukumu hili na hatari inayowakabiri ni kazi kubwa lakini ni lazima tufanya hivyo kwaajili ya watu wa Syria” akaongeza Ban Ki Moon.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi zilizoombwa kuchangia waangalizi hao wa amani na tayari imeshaonyesha nia ya kutekeleza ombi hilo.
Akizungumzia hali ya kisiasa katika Bara la Afrika, Ban Ki Moon, ameelezea kusikitishwa kwake na hali ya mambo ilivyo katika nchi za Guinnea Bisau, Mali na kati ya Sudan na Sudan ya Kusini.
Kuhusu mgogoro wa nchi za Sudan na Sudan ya Kusini, Ban Ki Moon amezitaka pande hizo mbili kusitisha mapigano na vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani na kurejea katika mkataba wa makubaliano ya amani. Na kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kuzisaidia pande hizo mbili.
Kwa upande wa Guinea Bisau, Mkuu huyo wa UM ameeleza masikitiko yake ya kuwapo kwa taarifa za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kuwaonya wale wote wanaohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu kwamba watawajibishwa.
Akahimiza kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba na kwamba amemuagiza mwakilishi wake kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Africa, ECOWAS na Muungano wa nchi zinazozungumza Kireno katika kutatua mgogoro unaoendelea nchini humo.
Na huko Mali, Katibu Mkuu anasema Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na AU, ECOWAS na wadau wengine ili nchi hiyo ambayo nusu ya eneo lake limetwaliwa na wapiganaji wanaotaka kujitenga irejee katika hali ya amani na kuwa nchi moja.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu ametangaza kuundwa kwa jopo la watu mashuhuri ambalo litafanya marejeo ya masuala yote yahusuyo maendeleo endelevu na hususani utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia baada ya 2015 na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.
Jopo hilo litakalokuwa na wajumbe kati ya 20 na 25 litaongozwa na wenyeviti wenza watatu ambao ni Marais Susilo Bambang Yudhoyono wa Indonesia,Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na Bw. David Cameron, Waziri Mkuu waUingereza
Akizungumzia kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa kuhusu maendeleo endelevu na mazingira maarufu kama RIO+20 unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao huko Rio de Jenairo nchini Brazil. Katibu Mkuu amewahimiza wakuu wa nchi na serikali kuhudhuria mkutano huo muhimu na ameelezea kuridhishwa kwake na mwitiko wa wakuu wa nchi na serikali.
Hata hivyo amewataka wadau wote wanaoshiriki katika kuandaa kabrasha maalum la mkutano huo kuonyesha utashi wa kisiasa na kukamilisha majadiliano hayo ambayo yameongezewa muda wa wiki moja zaidi.
Kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya wadau wakuu, nchi za Ulaya kwa upande mmoja na kundi la nchi 77 na China kwa upande mmoja, kuhusu masuala gani muhimu yanayotakiwa kuingizwa katika kabrasha hilo kwa kuzingatia vipaumbele vya makundi hayo. Vuta ni kuvute hiyo imefanya majadiliano hayo kuwa magumu na kutokamilika kwa wakati na hivyo . kupunguza kasi ya ukamilishaji wake ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa wa kabrasha hilo ambalo lina kurasa zaidi ya 200.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...