Na Zitto Kabwe (MB)


Mwalimu Azaveli Lwaitama ni mwalimu na mlezi wangu nje ya darasa. Alipokuwa Katibu wa Umoja wa WanaTaaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mimi nilikuwa Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Idara ya Uchumi. Nilikuwa nashinda kwenye Ofisi ya UDASA tukijadiliana kuhusu Umajumui wa Afrika (Pan Africanism), Ujamaa na harakati za kulinda haki za watu.
Ilikuwa ni nadra kwa Mwanafunzi wa Uchumi kuwa karibu na mwalimu wa Lugha na mnadharia mkubwa. Wanafunzi wa Uchumi tulikuwa tunajidai na kujivuna. Tulikuwa tunajiona bora sana maana darasa letu halikuwa linazidi watu 40 na kwa kweli wote hawamalizi. Darasa langu tulimaliza wanafunzi 25 tu kati ya 40 tulioanza. Mwalimu Lwaitama ni mpenzi mkubwa wa Muungano kama nilivyo mimi. Tumeapa kuulinda kwa namna yeyote ile. Yeye alikuwa mhafidhina sana akitaka muungano wa muundo huu aliouacha Mwalimu Nyerere. Mimi nataka kuulinda kwa kuufanyia marekebisho makubwa sana ya kimuundo. Hatukuwa tunakubaliana.

Wiki iliyopita Mwalimu Lwaitama kaandika kuhusu muundo wa Muungano katika makala zake za kila wiki katika Gazeti la kimombo la The Citizen. Amebadili msimamo. Ameona sasa muundo wa Muungano ulivyo sio endelevu. Ametoa mapendekezo niliyoyatoa siku za nyuma katika mazungumzo yetu ingawa yeye bado anayasema kwa shingo upande. Lwaitama sasa anataka Serikali mbili zilizonyumbuliwa. Anapendekeza Waziri Mkuu wa Muungano mwenye nguvu za za kitendaji. Nampongeza kwa kuboresha mawazo yake.

Hata hivyo bado Mwalimu wangu na Watanzania wengi wamejikita katika mjadala wa Serikali ngapi. Idadi ya Serikali inaonekana kama ndio dawa ya kero za Muungano. Ni kweli WaZanzibari wanataka uhuru zaidi na wengine hawataki kabisa Muungano. Unawalalia. Unawanyima uhuru wa kuamua baadhi ya mambo yao na japo halisemwi unawanyima wanasiasa wa Zanzibar mamlaka ya masuala mengine ambayo yangewafanya wajilimbikie madaraka.

Huku bara napo kuna watu, tena wanaongezeka kwa kasi kweli kweli, wakitaka Tanganyika yao. Tena wengi vijana. Demografia zetu zinaonyesha kwamba Watanganyika waliozaliwa Tanganyika ni takribani asilimia 12 tu ya Watanzania. Asilimia 70 ya Watanzania wamezaliwa wakati Muungano umeshasherehekea miaka 15 ya kuzaliwa kwake. Lakini wanataka Tanganyika yao. Wamechoshwa na kelele za WaZanzabari. Hawawataki WaZanzibari kujaa kwenye Bunge la Muungano wakati wapo kiduchu sana. Wanasiasa nao, japo hawasemi waziwazi wanataka wawe na mamlaka zaidi bila kulazimika kushauriana na wanasiasa wa Zanzibar. Linapokuja suala la wagombea Urais ndio kabisa wanakereka kutafuta mgombea mwenza kutoka Zanzibar. Wachambuzi wa historia za kisiasa siku wakiamua kufanya tafiti watachoka na roho zao watakapoona aina za wagombea wenza ambao wagombea Urais huteua, hasa kutoka sisi vyama vya upinzani.

Kiimsingi idadi ya wapinga muungano inazidi kuongezeka siku hata siku. Ukiwauliza kwa nini hawataki muungano wanasema aah, basi tu. Kama ni Mzanzibari atasema Tanganyika wanatutawala. Kama ni Mtanganyika atasema Wazanzibari wamezidi kelele, tunataka Tanganyika yetu. Sisi ‘Unionists’ nao hatuna majibu ya kuridhisha sana na kukonga nyoyo. Isipokuwa tu, Muungano huu ni wa iana yake Afrika na Duniani. Ni alama pekee ya kuonyesha Mwafrika kupinga mipaka ya kikoloni. Sasa hili haliwaingii kichwani ‘secessionists’ hatuna la kuwasaidia. Lakini ni lazima tuurekebishe Muungano huu. Ulivyo sasa utavunjika tu. Kuulinda muungano ni kuufanyia marekebisho makubwa. Mwalimu Lwaitama kaliona hilo. Pendekezo lake liboreshwe sasa. Sio rahisi sana.

Sasa tufanyeje? Serikali moja itaimeza Zanzibar. Serikali Tatu ni gharama kuendesha na Serikali mbili zimeimeza Tanganyika na watu wanataka Tanganyika yao na zinainyima uhuru Zanzibar na watu wanataka wawe huru zaidi. Mfumo wa Serikali ngapi na kadhalika ni moja ya mikakati ya wanasiasa katika kusaka vyeo. Sisemi sio halali kujadili lakini kiukweli mfumo gani wa Muungano hautaongeza fungu la dagaa kwa mwananchi wa Kagongo au sinia la ubwabwa kwa mwananchi wa Mkanyageni. Waingereza wana msemo ‘unataka kula keki yako na kubaki nayo’, basi tuwe na Serikali zote.

Nimeanza na Mwalimu Azaveli Lwaitama. Naboresha hoja yake kwa kurudia niliyowahi kuyasema huko nyuma kuhusu muundo wa Muungano. Tuwe na Dola Moja tu. Ndio, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wala sio Shirikisho la Tanzania (kwanza litatuondoa kwenye kiti chetu kule Umoja wa Mataifa maana kwa jina letu sisi tunakaa katikati ya Uingereza na Marekani. Katikakati ya mabwana wakubwa, labda ndio maana wanatupa misaada sana, unajuaje?). Tuwe na Rais mmoja tu mwenye mamlaka kamili ya Asasi za Dola – Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Uhamiaji, Sera za Fedha na jukumu la jumla la kusimamia ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Achaguliwe na Watanzania wote wa pande zote mbili za Muungano kwa kupata zaidi ya nusu ya kura za pande zote za Muungano. Tuachane na mambo ya Mgombea Mwenza. Tumejaribu tumeona hana maana zaidi ya kutembea na mikasi tu.

Zanzibar iwe na Waziri Mkuu mtendaji kwa masuala yote ambayo sio ya Muungano. Tanganyika iwe na Waziri Mkuu mtendaji kwa masuala yote ambayo sio ya Muungano. Hawa watateuliwa na Rais wa Muungano kutoka chama chenye Wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi Tanganyika na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Wote watakuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa utaratibu kwamba iwapo Rais anatoka Zanzibar, basi Waziri Mkuu wa Tanganyika atakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Pili wa Rais. Kule kule kwenye misingi haswa ya Muungano. Hawa wataongoza Mabaraza yao ya Mawaziri na watakuwa na nguvu ya kuteua na kufukuza Mawaziri wanavyotaka. Hawatakuwa Wabunge katika Bunge la Muungano.

Bunge la Muungano litakuwa dogo lenye Wajumbe wasiozidi 101 pamoja na Rais wa Bunge la Muungano. Wabunge wa Muungano watatoka kwenye mikoa (au Majimbo kama sera ya Majimbo itakubalika). Kwa utaratibu wa sasa kila mkoa utachagua wabunge 2 mmoja mwanamke mmoja mwanaume kwenda Bunge la Muungano. Wajumbe wa Ziada watatokana na uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata kwenye kura za Rais wa Muungano. Idadi hii yaweza kupunguzwa na hata kuwa na Wabunge 51 tu akiwemo Rais wa Bunge la Muungano ambapo kwa mikoa ya sasa kila mkoa utachagua Mbunge 1 na wengine watokane na uwiano. Rais wa masuala ya Muungano atakuwa Mkuu wa Shughuli za Serikali katika Bunge la Muungano na Rais kwa mwaka mara moja atahutubia Baraza la Taifa (Wabunge wa Bunge la Muungano na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka kila upande wa Muungano). Wazungu wanaita hotuba hii ‘State of the Union’ na wengine huita ‘Queen’s Speech’.

Mkuu wa nchi mmoja, Dola moja ya Jamhuri ya Muungano. Serikali mbili na kila upande una Serikali yake yenye mamlaka kamili ya maisha ya watu wao ya kila siku. Haya, tatu pamoja na Serikali ndogo ya Muungano. Lakini tutakuwa tumepata kila kitu labda. Wenye kutaka Uhuru mpaka Zanzibar watapata. Wenye kutaka Tanganyika watapata na wenye kutaka Muungano kama Dola yenye nguvu watapata.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 33 mpaka sasa

  1. Hoja ni nzuri sana, kwani itairudisha Tanganyika. Ila Hoja hii haijaangalia upande wa Zanizbar, hayo yote aliyoyapedekeza Zitto kwa sasa takriban yote yapo, baraza la wawakilishi, mkuu wa nchi mtedaji,na kutowa makamo wa Raisi. Jee kilio chao ni kipi? au ndio unataka tuamini kwamba hawana hoja ya msingi ya kutaka mabadiliko zaidi, ni kelele tu. Hapana wazanzibari wanajuwa wanachokitaka, hawana haja sana ya Muundo huo kwani madai yao bado hayajatekelezeka hapo. na wanachodai wao sio siri kila siku wanakisema.
    Ila kama na upande wa pili nao wanaona ipo haja ya kuwa na Tanganyika yao, nao wawe wazi wasibubiri Wazanzibari waseme ndio wajifanye nawo kana kwamaba wanaimani sana na muugnano kumbe wanumia pia.

    Hii hoja ni njema zaidi kwa mtu alitengaza nia ya Kuutaka urasi, kwani itampa mamlaka zaidi, si kwa wazanzibari, kwao haijatatua tazizo, endelea kufikiri. Wao msimamo wao unatokana na hoja na uzoefu wa miaka 50. Nadhani hawana haja tena ya Queen speeches.

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 26, 2012

    Wazo zuri sana sasa kwa nini tusifanye kama Canada au Marekani ambapo provinces au states zinachagua Premier na Magavana... yaani kufanya federation. Zanzibar waendelee walivyo ila badala ya kuchagua Raisi wachague waziri mkuu na Bara pia wachague waziri Mkuu hawa wapigiwe kura. Hawa wataunda serikali zao na kuendesha mambo yao na kufuatana na katiba zao. Mwisho ufanywe uchaguzi wa Raisi wa Muungano ambaye ndiyo atakuwa Mkuu wa nchi kufuatana na katiba ya Muungano. Kwamba katika katiba yajulikane yapi ni mambo ya Muungano na yapi ya serikali ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Tukisema kwamba hatuwezi kufanya hivi kwa sababu ya gharama tutakuwa tunajidanganya bure na matatizo ya Muungano hayataisha. Waswahili wanasema maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga. Maadamu tuliamua Muungano na tumeukubali basi na gharama zake tuzikubali lakini in a long run kila mtu atawajibika na maendeleo yatapatikana.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 26, 2012

    Kwa kweli Zitto umechambuwa kadiri ya uwezo wako ila unarudia makosa yale yale waliyoyafanya nyerere na Karume, Kwa nini munahubiri democracy lakini muna-turn blind kwenye implementation? Kwa nini hamtowi pendekezo la kuwa wananchi wote wa pande zote mbili za muungano waulizwe kama wanataka muungano au la na kama wanautaka ni muungano wa aina gani? hapo ndio mutakuwa mumeutendea haki umma wa Watanzania.
    Na haya makosa pia yamefanywa na marais wa East Africa mimi ni mtanzania sijaulizwa hata siku moja maoni yangu kuhusu jumuia hii jee kwa nini hatuigi mifano ya jumuia zilizofanikiwa ikiwemo EU ambapo wananchi wanashirikishwa mfano Waengereza wamekataa Pound kuingia kwenye Euro na hakuna aliepiga kelele kuwa wamevunja EU. Wacheni usanii, mukiendelea kutuamulia basi muungano utakufa kifo cha kawaida kabisa na then EAC itakufa the same siku ambapo atakuja rais wa kati ya big three nation awe na tofauti na mwenzake kama vile alivotofautiana nyerere na kenyata EAC ikavunjika

    ReplyDelete
  4. Naona imekaa vizuri, ingawa tunahitaji kuijadili zaidi. Kuna maswali bado yapo hapo. Ni mwanzo mzuri kwenye kuujadili Muungano wetu. Hata mie nisingependa KABISA uvunjike, TUUBORESHE ili kila upande unufaike na kuridhika.

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 26, 2012

    Nakubaliana nawe Mheshimiwa Zitto .Z. Kabwe. Hiyo hasa ndio kiu yetu watanzania,siasa tuweke kando tuje kwenye uhalisia.Mungu ibariki Afrika ,Mungu ibariki Tanzania.

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 26, 2012

    Mimi pia ni mmoja wa hao wanaokerwa na Muungano....Kwanza kabisa napenda ieleweke wazi kuwa Siuchukii bali vijimambo tu :-

    Kama Tunajiita tumeungana kwa nini Zanzibar ina:-
    1. Rais Wake
    2. Bendera Na wimbo wao wa Taifa
    3. Bunge Lao

    Kwa Mtazamo wangu Kama tumeamua Kuwa Na Muungana Basi tuwe na serikali moja itakayofanya Maamuzi kwa maslahi ya pande zote bila upendeleo....Kama hilo haliwezekani basi kila upande ukae kwao na wawe na mamlaka kamili.....Marekebisho makubwa yanahitajika!!!!!!!!!

    Mama Maximus

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 26, 2012

    Zitto kusema ''vijana wa Tanzania wanataka Tanganyika yao '' ni unafiki ,mimi ni kijana na nataka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,kulete habari za Tanganyika ni kuturudisha miaka ya 1960 ...........hapo umenikera sana! mapendekezo yao yana logic kiasi flani ,tatizo lililopo ni kuwa kuna risk ya kuuwa kabisa Muungano wakijaribu kufanya re-structuring ndio maana we lazima tuwe very cautious in this!

    Mdau

    ReplyDelete
  8. AnonymousMay 26, 2012

    Tatizo kubwa kwa wazanzibari ni utaifa wao. Kwao uhuru wanaoutaka sio huu wa kujiamulia mambo ya kiserikali bali ni utaifa kutokana na utafiti uliofanyika. Serikali ya mfumo unaousema Mheshimiwa bado utakuwa na kigugumizi cha suala la utaifa ambalo wazanzibari ndio hoja yao kubwa. Katika mfumo wako zanzibar tayari ipo katika mfumo huo na kelele zao ziko kubwa zaidi katika mfumo huo kuliko Tanzania Bara.

    Kwa nini tusiuangalie mfumo wa EU, Mahakama yenye mamlaka kubwa moja, Bunge la mfano ulioueleza ni zuri zaidi na lissishie kwenye misingi ya mikoa tu bali litazame na ajenda muungano. Passport moja, sarafu moja, baraza la mawaziri, na uraisi unaorotate baina ya nchi mbili, nguvu ya serikali ikiwa chini ya Mawaziri wakuu.

    Ila katika masuala ya Mambo ya nje kila mmoja na lake, utaifa na tubakie na kila mmoja na utaifa wake. Wenzetu wameweza na union zao zipi katika mfumo huo na unaendelea kuimarika sisi kwa nini tushindwe tukiwa na nia.

    Kelele za wavunja muungano zinapata nguvu kwa kasoro kubwa ya utaifa hasa Zanzibar na sio chuki au kutothamini ukweli wa udugu uliokuwepo baina yetu, tatizo gani kuwa ndani ya mipaka yetu tukabakia raia wa nchi moja tanzania, nje ya mipaka yetu tukawa na utaifa wa nchi tunazotoka? Hasara gani ikiwa hasa ndio chanzo kikuu cha migogoro ni utaifa?

    Mimi ni mmoja wa unionist, nikiamini Zanzibar na Tanzania historical tumetoka mbali kabla hata ya uhuru wa tanganyika na zanzibar, tukiwa na aina ya mfumo wa nchi moja tokea zama za sultanate of zanzibar. Hivyo siamini kama muungano unaugumu kutunzika ila nchi iliyona historia ya kuwa taifa doogo kwa karne na karne halitowacha kuondoa hisia za kumezwa ikiwa utaifa wao haujawekwa kwenye meza na kujadiliwa kwa kina.

    Sote tunafaidika na muungano, na tumeona japokuwa una matatizo lukuki umeweza kudumu ka miaka 48, sababu nchi zenye muungano huu ziko stable na zinafanana zaidi kimaadili. Nazungumza hivi nikimaanisha hata hii jumia ya Afrika Mashariki sioni kama ni taasisi ya kudumu kutokana na nchi wanachama husuan Rwanda na burundi pamoja na sasa tetesi za kujoin South Sudan au hata Uganda, zote haziko stable kama tulivyo sisi. Hivyo ni jambo zuri kulindwa kwa kila hali tubakie kuwa ncho moja tukiwa ndani ya mipaka yetu na nje tujiwakilishe kwa nchi tuzitokazo.

    System ya sasa ni kwamba ndani ya Tanzania ni nchi mbili, nje ni nchi moja na ndio chanzo cha migogoro, katika mfumo ujao tuwe wamoja ndani ya mipaka yetu, nje kila mmoja na utaifa wake. Hivi tuseme muungano wa nchi za ulaya katika mfumo kama huo ni weaker kuliko huu wetu? au ndio matatizo zaidi kuliko wetu? Tukubali ugumu wa muungano huu ni hoja ya UTAIFA, na kama hakuna anekubali ukweli hebu na tuangalie marekebisho ya katiba ya zanzibar ya 2010, jee direction ya katiba ile haina lengo la kurejesha utaifa wao?

    Kama tatizo ni katika UN kukosa kukaa baina ya mabwana wa dunia (USA na UK) basi kwani lazima tubadili jina? Zanzibar wako tayari kukaa karibu na kina Zimbabwe huko mbali kabisa. mfano mdogo ni UK, Itali, Ujarumani, Ufaransa nk zote zinajiwakilisha kama nchi tafauti huku EU ikiwa inawajoin force zao kwanini sisi tushindwe?

    ReplyDelete
  9. AnonymousMay 26, 2012

    Wengi wamesema rais awe mmoja(DITTO),mtu mmoja kasema kupokezana urais kutoka kila upande kila baada ya vipindi kadhaa,nk(DITTO)..MUUNGANO UDUMU UDUMU MILELE.

    David V

    ReplyDelete
  10. AnonymousMay 26, 2012

    wacheni kutusemea wazanzibari kama nyie maunionist kaunganeni na congo na burundi tuacheni na Zanzibar yetu tunasema tena muungano wa kutawaliwa kama huu hatuutaki tunataka Zanzibar yetu thyen kama nyie maunionist tuje na muungano kama wa EU otherwise tubaki kama Malaysia na singapore na ujirani mwema hizo za zito sisi tunaona ni siasa za watanganyika dhidi ya kuimeza Zanzibar hana tofauti na nyerere

    ReplyDelete
  11. AnonymousMay 26, 2012

    zanzibar wanavyotaka na ilivyo hasa wanataka wawe nchi tafauti huu muungano hasa hatuutaki tena

    na tunataka tuwe na kila kituchetu hapa ndani kwetu na nje ya nchi iwe tuna balozi zetu iwe sisi na tanganyika mtu akitaka kuingia nchi nyengine aombe visa sio akuripuke tu kuingia nchi nyengine tumechoka na huu muungano uliopo sasa hivi na HATUTAKI HASA KUUNGANA NA TANGANYIKA

    NA nikwanini tuwe tunangangania huu muungano wakati hauna faida kwa pande zote mbili, ila ni bugudha tu

    jengine hakuna wacha zanzibar iwe huru kwa kila kitu na hapo tanganyika tuwe na balozi tu wa zanzibar na nyinyi watanganyika muwe na balozi tu zanzibar jengine hakuna

    hapo ndio kila pande itakuwa na amani na utulivu ndani ya roho zao sio sasa hivi chochote kitakachofanywa basi tatizo halijatatuliwa ila nikuongeza matatizo tu

    ReplyDelete
  12. AnonymousMay 26, 2012

    watanganyika tulio zanzibar hatuishi kwa amani kutokana na suala la muungano je wazanzibar waliopo tanganyika nao wanaishi kama ss huku kwao wakituona tu watanganyika tunapita wanasema muungano hatuutaki kila mtu kwao ss mwisho wa yote sisi tuliopo zanzibar itafikia kupigwa na kuvamiwa na hawa raia wazanzibar. tunaomba serikali iliangalie hili suala

    ReplyDelete
  13. AnonymousMay 26, 2012

    JAMANI WAACHENI HAO WAUNGUJA WAENDE ZAO MIMI BINAFSI SIWAPENDI, NA SIELEWI KWA NINI NA WAO NI WATANZANIA. NINAVYOSEMA HIVYO NI KWA SABABU ,WAO WAZANZIBARI KWANZA NI WABAGUZI NA KUJIFANYA WAO SIO WAAFRIKA ETI NA WAARABU KWANINI TUWANGÀNGANIE ? WAHATUONGEZEI LOLOTE ZAIDI YA MAJUNGU NA FITNA KAMA HAWANA AKILI NZURI . ACHA WAENDE ZAO WATAJIJU JINSI GANI WAO WATAKAVYO ISHI. tANZANIA SIO YA UISLAM TU HATA UKRISTO NA DINI ZINGINE ZINA HAKI LAKINI WAO NI UARABU KWENDA MBELE NA DHARAU KWA AWTU WÉNGINE WAO WANA JIONA KAMA NI WAARABU KUTOKA OMAN SASA ACHA WAAENDE ZAO HAWANA MPANGO WOWOTE ZAIDI YA KUTUPA HASARA ZA KUWASAIDIA KILA SIKU. WAACHE KWANZA SIO WAFANYA KAZI NA CHAKULA HAWANA KAMA WATAAGIZA CHAKULA KUTOKA UARABUNI ACHANA NAO SWAIN.
    MIMI KWA KWELI SIONI SABABU YA KUWA NA UMOJA NA HAWA WATU . ACHA WALE UROJO WAO NA UDEBWEDO

    ReplyDelete
  14. AnonymousMay 26, 2012

    Muungano.. Muungano.. kweli wakoloni wametufikisha pabaya.. walitutawala na kutugawa. Ukweli ni kwamba sisi tulikuwa wamoja kabla ya kuja hawa mafedhuli wakoloni. Wakatugawa na kutuwekea mipaka walivyotaka wao. Hivi mmewahi kujiuliza kwani ramani ya Afrika ni rahisi kuichora kuliko ya Ulaya? Jibu mnalo wenyewe. Nikirudi kwenye swala la Muungano, kama jina lake lilivyo ni kitu kizuri sana. Tatizo ninaloliona mimi ni kuwa, kuna watu wanaamini kuwa nje ya muungano wao watapata fursa aidha za kutawala au kuwa na hali bora za maisha. Na hawa huongozwa na tamaa, uroho na wivu usio na maana( Kama wale walibia waliomtoa sadaka Gadafi kwa kutaka uhuru wa kuongea na kusikilizwa tu. Sasa wamepata uhuru walioutaka ila wameukosa ule wa amani)
    Mimi naona ni kweli kuwa kuna maeneo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho katika huu Muungano ambao mimi naamini ulikuwepo kabla ya kuja kwa wakoloni. Ila katika kufanya hayo marekebisho watu wasiongozwe na tamaa, huwa nakera sana kusikia kuwa madini, mafuta eti sio sehemu ya Muungano, huo ni upuuzi na tamaa tu. Kuondokana na upuuzi huo kila mmoja wetu afanye kazi kwa bidii na kuwajibika ipasavyo kwa kutunga sheria kali zitakazo wabana viongozi na yeyote asituchakachue. Tukizisimamia vizuri hizo sheria tutakuwa na amani na wala hatutakuwa na haja ya kulumbana kuhusu Muungano. Mwisho kwa kuwa wenye Muungano ni sisi wananchi wote basi si haula tukapewa nafasi ya kujadiliana jinsi ya kuudumisha huu Muungano.

    ReplyDelete
  15. Midladjy MaezMay 26, 2012

    ND. Zitto umeniibia mawazo yangu hapo juu kwenye vichwa isipokuwa mimi kwa vile nina uzoefu wa kuishi Zenji katika kipindi kigumu sana Novemba 1965 hadi Aprili 1974 kuna makovu yalitokea ya kijamii ambayo yanafanya upande mmoja usiwaamini sana upande wa pili...! Kwanza mauaji makubwa yaliyotokea siku za mapinduzi yalioongozwa na Watu wenye asili ya Bara na kwamba mfumo wa sasa wa utawala unadhibitiwa na watu wa Mrima! Pili mafanikio duni ya kiuchumi hayana mvuto kwa Wazanzibari labda kwa Wazanzibara ! Tehehehee..!.Sasa nikiunga mkono Mapendekezo yako lazima yale mambo ya utata yawemo katika mfumo mpya wa muundo wa Muungano ambapo isemwe kuwa Urais wa Muungano utakuwa wa zamu kila baada ya miaka mitano! Bila ya kuwemo hili nina uhakika siku zote Rais atatoka Bara! Mambo mengine yanazungumzika ikiwa nia njema ya kuendeleza muungano wetu adhimu ipo! Na tahadhari kwa wale wasioupenda muungano dunia yote inaelekea kuungana sasa nyie mnataka watoto na wajukuu wenu wakaishi wapi! Wengi wanashabikia kwenda kutembelea na kama hakuna budi kuishi Marekani , Canada au UK mnajua nchi zile ni dola za Muungano! Zitto kwa hili la Muungano umenikuna na utumie busara hizi hizi kuhakiklisha mnapigania kuimarishwa usafiri wa reli nchini! Najua unafahamu kwamba eneo la nchi yetu ilipo kijiografia tunapakana na nchi takriban 8..kama miundo mbinu ya reli yetu inakuwa imara na ya kuaminika basi ni mgodi tosha usiokwisha utakaokuza uchumi wa Tanzania kwa uhakika zaidi kuliko hii migodi yako unayoipigania kila siku..!! Mungu Ibariki Afrika , Mungu Ibariki Tanzania..!

    ReplyDelete
  16. AnonymousMay 26, 2012

    Hoja ya Zitto haina uzito wowote, naeleza hoja zenye mapungufu

    1. Si kweli kwamba watu wabara wanataka Tanganyika, kama anavyosema wengi wamezaliwa ndani ya Muungano, watatake tena Tanganyika ambayo hawaijui?. Kifupi ni kwamba sisi watu Wabara tunakerwa na manunguniko ya Wazanzibar, wanaona kama sisi ni wakoloni wao. Sisi watu wa bara hatuoni kama zanzibar wana msaada wowote kwetu na tungependa waruhusiwe waendelee na mambo yao na wawe ncu kamili kama wanavyolilia, tuna amini kwamba mtoto akililia wembe mpatie. Tunaona Zanzibar wanafaidi sana muungano, nchi ambayo ni sawa na wilaya ya Kibondo imejaza wabunge Dodoma, ina mwaziri, makamu wa raisi nk. inapewa umeme, ulinzi na ajira (polisi, uhamiaji, mambo ya nje n.k), wafanya biashara wao wamepata soko la watu mil. 40 free of charge na mengineyo. Tunasema Zenji waondoke sisi hatutajali tunaitwa Tanganyika, Azania, Tanzania ama jina lingine lolote.

    2. Serikali moja yenye mawaziri wakuu wawili haitawezekana kamwe; jiulize nani atagharamia viongozi wa muungano akiwamo raisi? Huoni kama waziri mkuu wa bara atakuwa na nguvu kuliko Rais, umesahau ya Boris Yeltin na Gobachev?

    3. Umesahu kwamba ni kura ya maoni tu ndio itaondoa kelele zote hizi? Binafsi nasikia kichefuchefu mtu akiniita mtanganyika. Waaceheni zenji waondoke zao, tutaishi na malalamiko yao mpaka lini wakati hatupati chochote toka kwao.

    ReplyDelete
  17. AnonymousMay 26, 2012

    Mimi kinachonikera kuhusu hili suala la Muungano ni kelele na shutuma za wazanzibar kwa wananchi wa kawaida wa bara wakidhani tunafaidika nao, wamekuwa wakitoa maneno machafu kwa viongozi waasisi na hasa Mwalimu J.K Nyerere, wazanzibar wanahitaji elimu ya kutosha kwani wengi wao bado wana mawazo ya kwenye mabaraza ya kahawa, hawatoi hoja ila wanatoa lugha chafu, ni kweli muungano una matatizo na unahitaji marekebisho ila kwa jinsi ambavyo wazanzibari wanalichukulia suala hili na kudiriki hata kuanza kuwafanyia fujo baadhi ya wabara walioko zanzibar sio sahihi kabisa, Muungano unajadilika bila fujo.

    ReplyDelete
  18. AnonymousMay 26, 2012

    ni mjdala mzuri na hongera mh. Zitto kwa kufungua ukurasa huu wa majadiliano ya muungano wetu, mi nna ombi najua siko peke yangu tuko wengi sana,naomba mwenye ufahamu na uelewa mpana na thabiti juu ya huu muungano anijibu maswali yangu,:
    1. Nini dhumuni la hizi nchi mbili kuungana.
    2.na nini faida ipatayo kila nchi katika huu muungano.

    ReplyDelete
  19. AnonymousMay 26, 2012

    Kama M-bara mimi niliuamini sana muungano. Lakini baada ya kuona kina na upana wa manung'uniko ya Wazanzibari amabayo hayaishi nakubaliana na Mhe Zitto kwamba ni wakati wa kuachana nao. Kiwango cha matatizo yetu ya kimaendeleo ni kikikubwa na hakiruhusu kupoteza wakati kuwabembeleza Wazanzibari; tuachane ili kuwapa fursa ya kuanza ugomvi wao baina ya Wapemba na Waunguja!

    ReplyDelete
  20. AnonymousMay 26, 2012

    Ndugu yangu Zitto

    Naona katika huu mjadala ujikita sana katika upande wenu,nyinyi wanasiasa wa tanganyika munajifanya munajua sana kuliko sisi wazanzibari,hebu soma historia ya zanzibar.

    Kwa kuanza hapo hoja yako kuwa na rais mmoja eti kile kiti chenu katika umoja wa mataifa kilo close na wamarekani,ndio ambacho kinachokutoeni roho ? Unajua kwamba tulisha muandikia katibu wa umoja wa mataifa kumuuliza kuwa ana mkataba wowote wa muungano ? Jibu tulilo pewa kuwa hakuna ispokuwa kuna barua tu ya kuondolewa kiti chetu cha zanzibar na kubadilishwa jina kuitwa tanzania,barua hio imetoka upande wa tanganyika tu,na sio zanzibar.

    Sasa hujui kuwa huo ni wizi na udanganyifu ? Sisi tunachotaka wazanzibari kuwa huru kitaifa na kimataifa,tunataka bendera yetu ipepe ndani ya umoja wa mataifa na tanganyika yenu pale ipepee ndani ya umoja wa mataifa ndio tujadili suala la muungano.

    Hivi sasa pale umoja wa mataifa hakuna hata mzanzibari mmoja,ndani ya office ya waziri wa mambo ya njee hakuna mzanzibari hata mmojabalozi za tanzania vile,eti tunaita muungano ? Haya tukiacha hilo munapoomba misaada tunapewa kwa jina la tanzania kama jamhuri ya muungano,mukishapokea munatusahau na kujibambikizia nyie eti sio wa muungano ni tanganyika tu.

    Haya ndio munatupa 4.5 kutoka bank kuu,wakati tumetoa asilimia kumi na moja,masuala ya mikopo na misaada sisi wazanzibari hatupaswi kupokea 4.5 kwani kule inakotoka tupewa kama nchi mbili huru zilizo unganga,kimataifa haijali udogo wala ukubwa wa nchi wala population.

    Nyinyi wanasiasa wa tanganyika munajifanya munajua sana kuongea na kuchambua mambo,njooni zanzibar basi katika ukumbi tufanye majadiliano kama nyinyi wana siasa kweli ?

    Sisi wazanzibari hatushungulishwi na siasa zenu,kama munautaka muungano nyinyi basi nendeni kaungani na kenya,uganda,kongo,sisi tumechoshwa sana,mumetumaliza kiuchumi na kijamiii,sisi tuliungana kwa imani safi,ila viongozi wenu walopita walijifanya mwamba sana,na akili nyingi kumbe kutwanga maji kununi.

    Jamuhuri ya watu wa zanzibar kwanza juu ya meza.

    Halafu ndio mulete masuala yenu ya muungano,ikiwa kile kiti cha umoja wa mataifa kimewatoa roho basi tafuteni chenu,kile kiti kimeharamiwa mwaka 1964 dec 10,kile ni cha wazanzibari na sio tanzania.

    Kwa kumalizia nyinyi watanganyika muna haki pia kama tutavunja muungano,ikiwa mutaendelea na jina lenu la tanzania au tanganyika,lakini naona tanganyika yenu hamuuipendi ila muna ji pretend tu.

    Peoples repulic of tanganyika pale kwenye meza

    Peoples republic of zanzibar pale kwenye meza .

    Ndio tutajadili muungano.

    Nakuomba Ankal maoni yangu yaweke,hizi sio jazba ni ukweli,hizi zama za democracy. please

    ReplyDelete
  21. AnonymousMay 26, 2012

    KUITISHWA KURA YA MAONI (REFERENDUM) NI KITU CHA KAWAIDA NA NDIO DEMOKRASIA YA UKWELI, UNASHIRIKISHA WANANCHI KWENYE MAAMUZI.IITISHWE HUKO ZANZIBAR WAAMUE, HALAFU NDIO TUANZIE HAPO KUJENGA NCHI. KAMA WAINGEREZA WAMERUHUSU REFERUNDUM HUKO SCOTLAND...HUKU KWETU CHA AJABU KIPI!!!

    ReplyDelete
  22. AnonymousMay 26, 2012

    Ndugu yangu Zitto

    Naona katika huu mjadala ujikita sana katika upande wenu,nyinyi wanasiasa wa tanganyika munajifanya munajua sana kuliko sisi wazanzibari,hebu soma historia ya zanzibar.

    Kwa kuanza hapo hoja yako kuwa na rais mmoja eti kile kiti chenu katika umoja wa mataifa kilo close na wamarekani,ndio ambacho kinachokutoeni roho ? Unajua kwamba tulisha muandikia katibu wa umoja wa mataifa kumuuliza kuwa ana mkataba wowote wa muungano ? Jibu tulilo pewa kuwa hakuna ispokuwa kuna barua tu ya kuondolewa kiti chetu cha zanzibar na kubadilishwa jina kuitwa tanzania,barua hio imetoka upande wa tanganyika tu,na sio zanzibar.

    Sasa hujui kuwa huo ni wizi na udanganyifu ? Sisi tunachotaka wazanzibari kuwa huru kitaifa na kimataifa,tunataka bendera yetu ipepe ndani ya umoja wa mataifa na tanganyika yenu pale ipepee ndani ya umoja wa mataifa ndio tujadili suala la muungano.

    Hivi sasa pale umoja wa mataifa hakuna hata mzanzibari mmoja,ndani ya office ya waziri wa mambo ya njee hakuna mzanzibari hata mmojabalozi za tanzania vile,eti tunaita muungano ? Haya tukiacha hilo munapoomba misaada tunapewa kwa jina la tanzania kama jamhuri ya muungano,mukishapokea munatusahau na kujibambikizia nyie eti sio wa muungano ni tanganyika tu.

    Haya ndio munatupa 4.5 kutoka bank kuu,wakati tumetoa asilimia kumi na moja,masuala ya mikopo na misaada sisi wazanzibari hatupaswi kupokea 4.5 kwani kule inakotoka tupewa kama nchi mbili huru zilizo unganga,kimataifa haijali udogo wala ukubwa wa nchi wala population.

    Nyinyi wanasiasa wa tanganyika munajifanya munajua sana kuongea na kuchambua mambo,njooni zanzibar basi katika ukumbi tufanye majadiliano kama nyinyi wana siasa kweli ?

    Sisi wazanzibari hatushungulishwi na siasa zenu,kama munautaka muungano nyinyi basi nendeni kaungani na kenya,uganda,kongo,sisi tumechoshwa sana,mumetumaliza kiuchumi na kijamiii,sisi tuliungana kwa imani safi,ila viongozi wenu walopita walijifanya mwamba sana,na akili nyingi kumbe kutwanga maji kununi.

    Jamuhuri ya watu wa zanzibar kwanza juu ya meza.

    Halafu ndio mulete masuala yenu ya muungano,ikiwa kile kiti cha umoja wa mataifa kimewatoa roho basi tafuteni chenu,kile kiti kimeharamiwa mwaka 1964 dec 10,kile ni cha wazanzibari na sio tanzania.

    Kwa kumalizia nyinyi watanganyika muna haki pia kama tutavunja muungano,ikiwa mutaendelea na jina lenu la tanzania au tanganyika,lakini naona tanganyika yenu hamuuipendi ila muna ji pretend tu.

    Peoples repulic of tanganyika pale kwenye meza

    Peoples republic of zanzibar pale kwenye meza .

    Ndio tutajadili muungano.

    Nakuomba Ankal maoni yangu yaweke,hizi sio jazba ni ukweli,hizi zama za democracy. please

    ReplyDelete
  23. AnonymousMay 26, 2012

    Wewe Mh. Zitto nakuona unaanza kuchanganyikiwa. Umeleta 'story' nyingi na majigambo ya kuwa umesoma uchumi na mengineyo. Hongera kwa kuwa mchumi ila nasi ni wachumi vile vile.
    Kutokana na mazungumzo yako, sioni kama kuna hoja ya msingi uliyoitoa na kwa hivyo sitokujibu sana zaidi ya kusema kwa ujumla tu.

    Wazanzibari hawataki tena muungano, wachachoshwa nao na wala musiwalazimishe kubakia kwenye muungano. Miaka 48 ni kipimo tosha cha kujua faida na hasara yake. Kama kweli mulikuwa na nia ya kuweka misingi mizuri ya kuungana basi mungeiweka kwa miaka hiyo. Lakini kila miaka ilivyokuwa inazidi ndio dhulma na ukandamizaji unaongezeka. Sasa itoshe kufahamu kuwa, hatutaki tena na hatuna haja ya muungano nanyi (tanganyika). Kama itaonekana kuna haja ya kuungana basi tukutane kwenye Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
    Kwa vile wewe umejinasibu ni mchumi, basi utapendelea zaidi shirikisho la Afrika ya mashariki ambalo ni la mkataba na si la katiba.
    Namalizia kwa kutaka uongozi wa blogi usifute mawazo yangu na napenda sana kuwasiliana na huyu muheshimiwa ili kuweka hoja mezani na kuijadili

    ReplyDelete
  24. AnonymousMay 26, 2012

    Zitto wananchi hawataki muungano. Why r so slow?? Why dont u get it? Muungano umeexpire haifai tena si kwa watanganyika ua wazanzibari. kinachotakiwa ni kuuvunja na nchi hizi mbili kuanza upya kama majirani wema.

    ReplyDelete
  25. AnonymousMay 26, 2012

    santorini,
    Watanganyika mpo machoooo au mmelala fofofo,kwani wachangiaji na mtoa madda hii nawaona kama bado mmelala na mnafaa muaamshwe.
    sijui asilimia ngapi wamezaliwa baada ya muungano,sijui wazanzibari waacheni wende kwao,sijuiwanaringa wanajiona waarabu,sijui wazanzibri tunawapa ulinzi,umeme na tunawalinda.
    Poleni sana wachangiaji na mtoa madda pia kwani nyote hamjui chochoteeeee kinachoendelea.

    Kwa kukuelimisheni angalia
    zanzinet.net majibu yenu yote yatapatikana hapo,
    Nakutakieni utazamaji mwema.

    ReplyDelete
  26. AnonymousMay 26, 2012

    MIMI NINGEPENDA KUTOA MAONI MACHACHE KUHUSU HUU MUUNGANO WA TANZANIA YETU NI WAZI KWA KILA MWENYE AKILI TIMAMU KUWA ULIUNDWA ZAMANI TENA KWA HARAKA HARAKA BILA KUFUATA KANUNI SHERIA WALA TARATIBU ZOZOTE ZA MAANA ZA ULIMWENGU WA SASA AU HATA ULIMWENGU HUO WA 1964.

    SASA BAADA YA MIAKA YOTE HII KUNA USHAHIDI ULIO WAZI KUWA MUUNGANO UMETUSAIDIA KUCHANGIA DAMU NA KUTUWEKA KATIKA AMANI, KIMAENDELEO SIWEZI KUZUNGUMZIA KWA KUWA MIMI SIO MCHUMI.MIMI NINGEPENDA KUZUNGUMZIA KUHUSU RIDHAA YA WANANCHI WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR KWANI MUUNGANO HUU UMEWAHUSU WAO KULIKO MTU YOYOTE MWINGINE,WAKATI UMEFIKA KWA TANZANIA SERIKALI AU CHAMA CHA MAPINDUZI KWA SABABU MIMI SIJUI SERIKALI NI NANI NA CHAMA NI KINA NANI NAONA WOTE NI MBWA KWA JIBWA YAANI SIONI TOFAUTI KUACHA UKAIDI WA KITOTO NA KUVIHUSISHA VYAMA VYA UPINZANI NA WANANCHI WA PANDE ZOTE KUAMUA NI MUUNGANO UPI UTATUFAA KUANZIA SASA KUELEKEA KARNE ZINAZOFUATA ULE WAKATI WA CCM KUENDELEA KUHUBIRI UMUHIMU WA MUUNGANO TULIONAO HATA KIPOFU WANAONA KUWA UMEPITWA NA WAKATI LAKINI JAMBO LA KUSTAAJABISHA SANA BADO KUNA VIONGOZI WA JUU HASA ZANZIBAR AMBAO WAO WAKO TAYARI KUTOA VITISHO KWA MTU YEYOTE ASIETAKA MUUNGANO BASI AHAME SASA HAO NDIO WASIOJUA WALA KUSOMA UPEPO UNAVYOVUMA UPEPO ULIWASHINDA KUUSOMA MUBARAK,GHADAFI ABDULLA SALEH WA YEMEN NA YULE ALI SALEH WA TUNISIA NA SASA UNAMPA TABU UPEPO HUO HUO ASSAD WA SYRIA NDUGU ZETU WA KENYA ULIWASHINDA UPEPO HUO HUO BAADA YA KUUWANA WALIJUA KUUSOMA VIZURI NA SASA WANAENDESHA NCHI KWA RIDHAA YA WATU WOTE SIO RIDHAA YA UONGOZI WA CHAMA TAWALA SASA TANZANIA NA CCM MNATAKA MFANO GANI? AU MNAFIKIRI NGUVU ZA DOLA NDIO DAWA YA KILA MARADHI KAMA NI DAWA HAO WALIOSALIMU AMRI WALIKUWA NA DOLA PESA AU DOLA SILAHA? NI VEMA MKAJIULIZA NA KUFANYA MAGEUZI YANAYOTAKIWA NA WENYE NCHI WALIOWAAJIRI KAZI BADALA YA KUFIKIRI WATANZANIA WALIOUNDA MUUNGANO NDIO WATAKAOULINDA KWANZA NI BORA MUULEWE ZANZIBAR NA TANGANYIKA TAKWIMU ZILIZOPO NUSU NA ROBO YA WALIOKUWA WATU WAZIMA WAKATI MUUNGANO HUU ULIPOZALIWA WAMESHAFARIKI DUNIA WENGI YA WATANZANIA HIVI SASA NI VIJANA WALIZALIWA MIAKA 25 ILIYOPITA NA WALE WALIOZALIWA MARA BAADA YA MUUNGANO AMBAO MIMI NI MMOJA WAO NA MAWAZO YETU SISI WENGI NI MUUNGANO WA 1964 UFANYIWE UKARABATI WA KUANZIA MSINGI MPAKA ROOFING AU UVUNJWE HUO NDIO MSIMAMO KWA LUGHA YA KISWAHILI SAFI UMEFIKA MWAKATI WA KUAMUA KUSUKA AU KUNYOWA LAKINI HUU SIO WAKATI WA KUPAKA MAFUTA KIPARA KAMA KUNA WENYE MASIKIO MSIJE KUSEMA HAMKUAMBIWA.

    MUNGU IBARIKI AFRIKA.

    MDAU.

    MONGOLIA.

    ReplyDelete
  27. AnonymousMay 26, 2012

    bara hatuhitaji tena huu muungano hauna faida yoyote gharanma kubwa kwa faida gani?? tunawabeba sana Zanzibar,,,, sisi bara tutaendelea kuitwa jamhuri ya muungano wa Tanzania,, hawazidi hata kwa ukubwa wa wilaya ya bagamoyo lakini wabunge 29 Zanzibar pekee watu milion moja tu ,Dar es salaam ina watu milion 6 wabunge saba tu kwa kweli hii kali

    ReplyDelete
  28. AnonymousMay 26, 2012

    Suala kubwa hapa ni kwamba Wazanzibari hawataki muungano wa aina yoyote na Watanganyika.

    Sababu ni kwamba imeonyesha wazi kwamba tangu mwanzo Watanganyika hawakua na nia njema katika kuungana na Wazanzibari.Viongozi wa Tanganyika wakiongozwa na Nyerere nia yao ilikua ni kuitawala Zanzibar, kuifisidi kiuchumi, kuigharikisha, kuifanyia kila ufisadi na mwishoe kuifuta katika uso wa dunia. Tayari mmeshatuonyesha ubaya mlionao sasa hatuwaamini tena.

    Tunapenda uhusiano wa kijirani kati yetu uendelee lakini muungano wowote mtakaotaja sisi hatuwaamini kwamba mna nia njema na sisi.

    Muungano umetunyima maendeleo, uhuru wa kuamua mambo yetu ya kiuchumi na kisiasa, umetudumaza, afadhali wakati wa kutawaliwa na wageni kuliko sasa kutawaliwa wa Watanganyika.

    ReplyDelete
  29. AnonymousMay 26, 2012

    BLOG YA JAMII KWA HESHIMA NA TAHADHIMA NAOMBA HII TOPIC IPANDISHWE TENA 'FRONT PAGE'-MWANZO(MARA MOJA TU).INA COMMENTS NZURI SANA NYINGI HAZINA JAZIBA,NI ZA KISOMI ZAIDI.LABDA WAKUBWA WANAWEZA KUPATA MAWILI MATATU HUMU.BORA KUJADILI MUUNGANO KULIKO KUJADILI UDINI NA UKABILA.

    David V

    ReplyDelete
  30. ZITO kama wewe ni "unionist" nadhani Tanganyika kwa kule kwenu kigoma iko karibu sana na Burundi na mfanana kwa kila hali, kuanzia tamaduni, rangi na hata asili... kwanini usipigie debe na kutia nguvu muungane na Burundi, badala yake unalazimisha na kung'ang'ania kuungana na nchi (Zanzibar) iliyo mbali na msio fanana tamaduni wala asili! Hivi kunanini Zanzibar kwa watanganyika? Si washasema muwaache wapumuwe??? Hivi hamusikii au hamuelewi?!!
    HATWEBU MUUNGANO!

    ReplyDelete
  31. Sikuwahi kufikiria kama kuna suluhishi kama hili na kama hili nalo halitakuwa suluhisho basi tunaelekea katika yafuatayo:
    1.kuvunja kabisa muungano
    2.kulazimisha muundo wa sasa katika muungano
    3.maafa na hili Mungu aliepushe.
    Alichosema ZITTO ni kikubwa na kinaingia katika akili ya mtu yeyete mwenye kuutakia mstakabali mwema muungano huu tuliorithishwa na wazee wetu Mwalimu Nyerere na Abed Amani karume.

    ReplyDelete
  32. AnonymousMay 27, 2012

    Labda tujiulize, ninini kiini cha kera ya muungano? ni utaifa? ni mfumo wa uongoze uliopita wakati wake? utaifa? nani anayefaidika na huu muungano na kwanini? nani asiyefaidika na huu muungano na kwanini?

    Swali lingine, je kuna mahali pengine duniani changamoto hii iliwahi kutokea au ipo leo hivi?

    Hebu tuangalie mfano wa China. Chukua miaka kama kuminatano au miaka ishirini iliyopita wakati huo ukimuuliza mTaiwani, je wewe ni mchina? mTaiwanizi anakujibu haraka na kusema, hapana mimi ni mTaiwani na sio mChina. Wakati huo China iliposikia kelele ndani na nje ya nchi yao kuhusu uhusiano wake na Taiwani, viongozi wa China politely walisema, China (pamoja na Taiwani) ni moja na itakuwa moja. Hapakua na kulegalega au hofu yoyote, msimamo huu ulikua mmoja na uliokamilika. Hatimaye mataifa mengine yenye maslahi yao waliisaidia Taiwani na matakwa yao ya kutaka kumegeka kutoka “China bara”. Wale viongozi wa China wakarudia kwa ukakamuvu na madhubuti kwamba msimamo ni sawa, umekamilika na haubadiliki kwamba, China ni moja na itakuwa moja tu hakuna kuvunjika wala nini.

    Lakini hao viongozi wa China walijua kwamba kelele nyingi za waTaiwani zilikua za maana fulani hivi (na sio porojo), kwamba yale wanayodai wanayataka mfano, kuwa na utaifa wao, uhuru wao, kujiongoza wenyewe, uhuru zaidi wa kufanya mambo yao wenyewe kama Taifa pekee, n.k. yana msingi wa aina yake hivi. Lakini viongozi wa China walijua hii orotha ya matakwa ya waTaiwanizi ilikuwa sio mambo wanayoyataka waTaiwanizi, viongozi hao walijua permanent suluhisho ni moja tu ambayo itachukua muda fulani kumilika na itafanya pande zote zirithike kikamilifu .

    Sasa kama movement ndio viongozi waChina wakaamua kuendeleza kimbunga cha kuijenga na kuiendeleza nchi yao “China bara”, walijua maendeleo yakiwa ya juu kufikia kiwango cha kilaupande kunufaika VIZURI basi hiyo kera itabadilika kidogo kidogo mpaka suala zima la kera ya muungano kuwa replaced na narrative ya maendeleo.

    Leo mTaiwani aliyeko popote pale iwe Marekani, Canada, au la muulize, je wewe ni mchina? Atakujibu kwa moyo, ndio mimi ni mchina natokea Taiwani. Wataiwani sasa wanajivunia China yao, hata ipad inatengenezwa China na kampuni ya kiTaiwani iliyowekeza “China bara”. WaTaiwani na China bara wanaona na kunauhusiano wa damu pande zote. Sasa pande zote zinanufaika na maendeleo dhabiti. Labda tunaweza kusema miaka kumi ijayo ukimuulizi mChina au mTaiwanizi, Je wewe ni raia wa nchi gani, jibu litakuwa moja. Eee bwana achakutuletea maswali yako hapa sie waChina tu na wale waliokua wanachochea nchi uvungike…unajuatena historia ya China inaandikwa.

    ReplyDelete
  33. AnonymousMay 28, 2012

    Naona Zitto Kabwe anatumiwa na wamerekani.wanataka tusiungane na zanzibar ili waje kiulaini. Huyu ni mtumishi wa wakoloni

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...