Rais Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wenzie wa Afrika wakiwa katika mdahalo wa taasisi ya kilimo ya GroAfrica kwenye jengo la Makao Makuu Mapya ya Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia leo.Mdahalo huo umefanyika kingoni mwa Mkutano wa Uchumi wa Kimataifa kwa Afrika.PICHA NA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa miradi mikubwa ya kilimo ya kibiashara nchini itatekelezwa kwa shabaha mbili kubwa - ambazo ni kuwatoa wakulima katika umasikini na kulinda miliki ya ardhi yao.

Aidha, Rais Kikwete ameambiwa kuwa Marekani inataka kuhakikisha kuwa Mradi wa Uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania – Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) unakuwa ni mfano unaong’ara wa uendelezaji kilimo katika Bara la Afrika.

Akizungumza na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Dkt. Rajiv Shah kwenye Hoteli ya Sheraton mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kikwete amesema kuwa shahaba kuu zaidi ya miradi kama SAGCOT ni kuwatoa wakulima wa Tanzania katika umasikini katika kipindi kifupi na kulinda miliki ya ardhi yao.

Rais Kikwete na Dkt. Shah wako mjini Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF), Kanda ya Afrika, ulioanza leo, Jumatano, Mei 9, 2012.

Rais Kikwete alikuwa anazungumzia hofu ya baadhi ya watu kuwa miradi mkubwa ya kilimo nchini itachukua ardhi ya wakulima wadogo ili iweze kufanikiwa. “Nia na madhumuni ya miradi mikubwa ya kilimo nchini siyo kuwapora wakulima wetu ardhi yao. Hasha. Nia yetu ni kuwasaidia ili wakue na watoke kwenye hali ya kilimo cha kujikimu na kuingia katika kilimo cha biashara.”

Rais amesema kuwa wakulima wakubwa watapewa ardhi tu pale ambako iko ardhi ya kutosha na hata baada ya kupewa ardhi watatakiwa kuwasaidia wakulima wadogo wanaokuwa wanaishi jirani na shamba la wakulima hao wakubwa.

“Tutawapa ardhi kubwa wakulima wakubwa pale ambako iko ardhi ya kutosha. Na hata baada ya kuwa tumepewa ardhi hiyo, wakulima hao wakubwa watatakiwa kuwasaidia na kushirikiana na wakulima wadogo. Hii ndiyo namna pekee ya kuwasaidia wakulima wetu kuondokana na umasikini,” amesema Rais Kikwete.

Naye Dkt. Shah amemwambia Rais Kikwete kuwa Marekani imedhamiria kuhakikisha kuwa SAGCOT unakuwa mfano wa miradi ya mfano na inayong’ara katika Afrika. USAID ni moja ya mashirika ya kimataifa ambayo inashirikiana na Serikali katika kuendeleza mradi huo.

Dkt. Shah pia amemweleza Rais Kikwete kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Nchi Tajiri na Zenye Viwanda (G-8) ambao umepangwa kufanyika Marekani kuanzia wiki ijayo. Rais Kikwete ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Bwana Meles Zenawi ni miongoni mwa viongozi wane wa Afrika walioalikwa na Rais Barack Obama wa Marekani kuhudhuria mkutano huo.

Katika mkutano mwingine, Mtendaji Mkuu wa Benki ya HSBC, Bwana Andrew Dell amemwambia Rais Kikwete kuwa benki yake iko tayari kuiwezesha Tanzania kukopa fedha nyingi ya ujenzi wa miundombinu kwa mpango wa Sovereign Bond badala ya kutumia fedha za kodi kujenga miundombinu ambayo inaweza kujengwa kwa urahisi na kwa kutumia fedha ya benki hiyo.

Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na wakurugenzi wa Kampuni ya MSP Steel and Power Limited ya India, Mabwana Manish Agrawal na Pranay Agranal ambao wanataka kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

Rais amewakaribisha wakurugenzi hao kuwekeza katika uchumi wa Tanzania akisisitiza kuwa Tanzania bado unahitaji wawezekezaji kwa wingi na katika sekta zote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 10, 2012

    Yametimia Afrika kurudi katika enzi za ukoloni....kama wanania njema kwanini wasiwasaidie wakulima wazawa kwa elimu labda na mitaji ili wakulima wazawa ndio waendeshe hii miradi mikubwa ya kilimo?kwa nini?Afrika kuwa shamba la dunia baada ya muda fulani

    ReplyDelete
  2. Matatizo ya Mbarali ni mfano hai kwamba wakulima wakubwa kutoka nje wanathaminiwa kuliko wakulima wadogo wenyeji. Na hakuna nchi yeyote duniani iliyoendelea katika kilimo kwa kuwaachia makampuni makubwa kutoka nje yaendeshe kilimo.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 10, 2012

    Hawa jamaa ni wajanja sana na wanajua chini ya hiyo ardhi kuna nini. Kilimo ni danganya toto tu. Wanajua chini ya hiyo ardhi kuna gesi, mafuta, uranium, dhahabu nk na sisi tumelala usingizi fofofo ...

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 10, 2012

    ndio tunavyotawaliwa hivyo. Huu ni ukoloni mambo leo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...