Hivi karibuni chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilielezea kile ilichoeleza kuwa ni kutishwa na wimbi la mauaji yanayotishia amani ya nchi kikidai kuwa jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake.

Madai hayo ya CHADEMA, pamoja na wanachama wengine na mashabiki wao, yalitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, ambaye alidai kuwa mauaji hayo yana mkono wa serikali ya CCM, ambayo kwa madai yao imeona wazi kuwa upepo wa kisiasa umekiendea vibaya na sasa kinataka kujiimarisha katika utawala kwa kuua watu wanaoipinga.

Akifungua kikao cha Baraza Kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam Aprili 29 mwaku huu mwenyekiti huyo alifafanua kuwa mbali na kuuawa kwa watu wanne kwa pamoja na juzi kifo cha mwenyekiti wao wa tawi huko Arumeru mkoani Arusha, jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo mwaka jana.

Mbowe katika maelezo yake alijaribu katika maeneo kadhaa kuihusisha CCM na au serikali yake katika matukio kadhaa yaliyowakabili baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema katika maeneo mbalimbali nchini likiwemo lile la Mbunge Highness Kiwia ambaye Suala lake bado Lipo mikononi mwa vyombo Vya dola likishughulikiwa.

Katika sehemu kubwa ya maelezo ya Ndg. Mbowe amejitahidi kuonesha kuwa mauaji yote yaliyoikabili na yatakayokuwa yakiikabili Chadema kupitia wafuasi wake yanafanyika kisiasa, Jambo ambalo ni la uzushi, kwani Halina ushahidi wa kisheria hata kimazingira, wa Moja kwa Moja unaoondosha ujinai au makosa hayo, na kuwa ni makosa yanayolenga muktadha wa kisiasa.

Huku akitaka kuuaminisha umma kuwa huo ndio ukweli, Ndg. Mbowe amesisitiza kuwa hilo lime kuwa likitekelezwa na CCM kwa lengo la kuwatisha wananchi kujiunga na chama hicho hoja ambayo haina msingi wowote wa kiutafiti.

Hivyo CCM kwa kutambua kuwa Suala la mauaji linabeba Kosa la jinai, na kwa kuwa Ndg. Mbowe ameshutumu Moja kwa Moja CCM na serikali yake kuihusisha na mauaji hayo, ni vema sasa nasi tukatoa msimamo wetu dhidi ya tuhuma, hiyo.

Kwanza, si busara hata kidogo kuihusisha CCM katika matukio hayo, kwani uchunguzi unaofanywa na vyombo vya dola umeshindwa mpaka sasa kuhusisha matukio hayo na siasa, badala ya kuyahusisha na makosa ya jinai ambayo hufanywa na watu kwa malengo tofauti na yale ambayo Ndg. Mbowe anataka kuwaaminisha watu.

Pili, CCM haijawai, haiwezi, na haitakuja fanya jambo lolote lenye lengo la kuvuruga Amani na Usalama wenye utulivu ndani ya taifa letu, hivyo uzushi na usingiziaji uliofanywa na Mtu Kama Ndg. Mbowe, si vema kuuacha kimya, badala yake nimetumia wasaa Huu muhimu Kujibu, na kutoa ufafanuzi ili Kuupa umma wa watanzania habari sahihi.

Ni aibu kwa Chama kama Chadema kujitahidi kwa nguvu zote kujaribu kuficha ukweli wa mauaji yanayotoa roho za watanzania wenzetu kwa kuyapa sura ya kisiasa. Hizi ni juhudi za makusudi za kutaka kuficha ukweli wa kinachotokea.

Ni aibu kwa chama kama Chadema kujaribu kutumia mauaji mabaya kama haya kutafuta mtaji wa kisiasa. Huku ni kuonyesha jinsi gani wamefilisika kisiasa mpaka wanafikia mahali pa kuamini kuwa wanaweza kutumia chochote kama mtaji wa kisiasa, vikiwemo vifo vya watanzania wenzetu. Huku si kufilisika tu ila kwakweli ni unyama unaotakiwa kulaaniwa na kila muungwana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 21 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 08, 2012

    Unajua mtu ukishajijengea sifa au historia fulani basi utashahabishwa nayo kwa kila jambo lenye mtizamo wa namna hiyo.

    Historia huhukumu, na pia humtambulisha muungwana na asiye muungwana. Nyie kijani na njano mna historia mbaya kuhusiana na mauaji, hivyo you deserve to be scrutinized with an equally deserving criticism.

    M.M.

    ReplyDelete
  2. Kwanza napenda niseme kuwa mimi ni m-Tanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Nina mawili matatu ya kusema.

    Nilitegemea aliyeandika taarifa hii angejitambulisha kikamilifu. Anavyoongelea suala la uungwana, napenda kumweleza kuwa kujitambulisha ingeonyesha uungwana na kutuheshimu sisi wasomaji. Kinyume chake, huyu Freeman Mbowe anayetajwa hakutumia uficho au uzembe huu wa kutojitambulisha.

    Kama ni suala la kufilisika kisiasa, mimi kama mfuasi wa Mwalimu Nyerere ninapenda kukumbushia kuwa miaka ya mwisho ya uhai wake, Mwalimu Nyerere aliilalamikia CCM kwa kufilisika kisiasa, na alifanya hivyo tena na tena, katika hotuba na maandishi yake, kama vile kitabu kiitwacho "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania."

    Nikirudi kwenye suala la haya mauaji, ninapenda kusema kuwa tangu yalipoanza na hadi sasa, nilitegemea CCM na serikali yake wawe mstari wa mbele kukemea na kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kulinda amani nchini. Kama kweli ujumbe huu tunaosoma hapa umetoka CCM, nashangaa kwa nini CCM itoe tamko wakati huu, baada ya watu wengi kupoteza uhai.

    Kama ni suala la kutumia jambo hili kisiasa, CCM inatumia fursa hii kujaribu kuiponda CHADEMA. Kwa miezi yote hii CCM na serikali yake haikutoa tamko la aina hii, ila sasa, kwa vile kuna fursa ya kuiponda CHADEMA ndio tunasikia tamko. Je, huku si kutumia suala husika kama mtaji wa siasa?

    Wajibu wa kwanza wa CCM na serikali yake katika hali iliyojitokeza ilikuwa ni kuungana na wa-Tanzania kulaani mauaji yale na si kungojea hadi sasa kwenye mwanya wa kujipatia umaarufu kisiasa kwa kuiponda CHADEMA.

    Kwamba CCM haijawahi na haitawezi kuhujumu amani na utulivu nchini si kweli. Kwa sera zake za kuruhusu rasilimali za nchi ziporwe na wananchi kudhulumiwa katika nchi yao, CCM inahujumu amani na utulivu nchini. Kwa sera zake za kukumbatia ufisadi, CCM inahujumu amani na utulivu nchini. CCM inapaswa kujua kuwa amani na utulivu unaosemekana uko Tanzania umetokana na sera nzuri za TANU ambazo CCM inazihujumu.

    Napenda kurudia kwamba mimi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Nikiangalia mtiririko na mazingira ya mauaji ya hao makada na mashabiki wa CHADEMA, inaniwia vigumu kuamini kuwa hayahusiani na siasa. Mwaka huu nilipokuwa Tanzania, nilikutana na mama mmoja ambaye anasema kuwa mwanae, ambaye alikuwa mwana CCM, aliuawa katika misukosuko ya siasa za CCM. Sasa kuambiwa kuwa CCM ni safi kiasi kwamba haina madudu kama hayo naona ni vigumu kwangu kuamini.

    Sote tunasikia mara kwa mara jinsi baadhi ya hao wanaoitwa viongozi wa CCM wanavyolalamika kuwa wanatishiwa maisha yao. Sitaki kuwataja majina, kwani malalamiko yao sio siri.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 09, 2012

    kwa hio we mchangiaji wa 1 unataka kusema maalbino wote tz ni chadema? kweli hio hoja haina msingi yaani kuua wanachama wa chama fulani ili kuwatisha wananchi basi watawaua wengi maana hao chadema c kidogo. kama kweli Mbowe kasema hivo hana sera huyo.

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 09, 2012

    Nimependa sana uchambuzi wa mtu huyu aliyetoa maoni ambaye hana chama chochote. Ni kweli kabisa nami niliposoma habari hii hadi mwisho nimejiuliza aliyeandika ni nani mbona hajitambulishi? jamani ccm mkae mkijua wananchi kwa sasa tumeelimika vya kutosha hivo kupindisham maneno mnajidanganya wenyewe tu.
    Kashfa za kufanya mauaji hata ndani ya chama chenu mnazisema tu kwa baadhi ya wanachama wenu kutishiwa kuuliwa na kama Dr. Mwakyembe alishalalamika kuwa polisi hawafuatinlii suala lake kimakini sasa nani anamuwinda kama si ninyi wenyewe? Amani haimaanishi kutokuwa na vita nchini tu. Ukikosa ada ya mtoto huna amani, ukikosa chakula huna amani, afya bora huwezi kuwa na amani haya mambo yenu ya kusema kila siku eti nchi ilikombolewa 1961 wadanganyeni wa enzi hizo hivi sasa ukombozi wa karne hii si hilo tu ni mengi mno ambayo serikali yenu haijakamilisha na hamtoweza kwa namna mnavokwenda.
    Wenu
    Mtanzania asiyeridhishwa na utendaji wa serikali ya CCM

    ReplyDelete
  5. NINAUNGA MKONO HOJA YA PROF MBELE

    ReplyDelete
  6. NINAUNGA MKONO HOJA YA PROF MBELE

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 09, 2012

    Asante sana prof kwa kuwaambia ukweli..tatizo lao CCM wanatuona watanzania wenzao kama hatuna akili vile..waache kujitetea pamoja na serikali yao kwa maelezo ambayo hata mtoto wa primary anajua ni uongo..fanyeni kazi kwa vitendo,maneno mengi

    ReplyDelete
  8. AnonymousMay 09, 2012

    Taarifa imetoka CCM utambulisho huo unatosha kuwa imetoka wapi, ingekua imeandikwa na mtu binafsi ingekua na ulazima wa kujibiwa, kwa hiyo kama mtu anahitaji kujibu hoja ajibu hoja kulingana na taarifa kuijibu ccm, kutaka lazima kujua aliyeandika ili tuanze kumtathmini badala ya hija iliyoko mezani huko pia ni kufilisika kimawazo.

    ReplyDelete
  9. AnonymousMay 09, 2012

    Well said Mbele, u deserve to be called Mtanzania! Wana-CCM si Watanzania tena, wako kwenye ulimwengu wao tofauti.

    ReplyDelete
  10. mimi swali langu ni rahisi tu..... kwanin mauaji haya yanatokea kwa makada wa CHADEMA tu na kwanin Jeshi la polisi,CCM na serikali yake havionyeshi kuwajibika kutokana mauaji haya? hivi wew uliyeandika makala hii una reference yeyote ya makada wa CCM waliouwawa kwa kuchinjwa au kujeruhiwa kwa kukatwa katwa mapanga kisha serikali ikaonyeshwa kutokubadilika? mauaji ni kitu kingine kabisa,mazingira haya yana mpa hata mwendawazimu mashaka kuwa ni ya kisiasa na si hivyo tu bali yanafania kupangangwa na kufanikishwa na chama tawala na serikali yenye ushawishi na nguvu za kidola. uliandika makala hii umejificha kwa kujua kwamba unakana kwa makusudi kitu unachokijua ukidhani kwamba ndo utakuwa umewaondolea uchungu wahanga wa mauaji na kuwahadaa watanzania kwamba maujai haya si ya kisiasa. Ni tabia ya kawaida ya CCM kuita kila tuhuma inayoelekezwa kwao kuwa ni la kizushi na lisilo na mashiko.
    ushauri wangu ni kwamba, fanyen utafiti wa hizi tuhuma kwanza kuona ukweli wake uko wapi sio kukaa kwenye computer yako na kuandika huu ni uzushi wakati undani wa suala hili unaujua. Chonde chonde,serikali tunaiomba ifanye wajibu wake wa kulinda wananchi wake.sisi kama wananchi,tunahitaji amani na siasa za kujengea wananchi imani na nchi yao na ushawishi wa kimaendeleo.

    Tumechoshwa a na siasa maji taka!

    ReplyDelete
  11. Mimi pia si mwanachama wa chama chochote cha siasa na hivyo sina sababu ya kupendelea upande wowote. Hata hivyo naungana na Profesa Mbele kwamba kitendo cha muandishi wa tamko la CCM kutojitambulisha kunanifanya mimi na wengine wengi kutilia mashaka ukweli wa tamko hilo.

    Kwa kawaida msemaji wa CCM ni Nape Nnauye ambae ndiye katibu mwenezi, itikadi na ushirikishaji umma na mara zote huwa anajitambulisha. Aidha naamini Katibu mkuu wa chama au mmoja wa wajumbe wa sekretarieti za chama hicho hangeona aibu wala woga kuandika jina lake au wadhifa kwenye tamko nyeti kama hili

    Pili tamko hili halielezi kwa nini CCM isihusishwe na mauaji hayo zaidi ya kusema kwamba kauli ya Mbowe ni uzushi na dalili za kufilisika kisiasa. Nilitegemea mtoa taarifa huyu angetumia muda wake mwingi kuelezea ushahidi au taarifa zilizotolewa na polisi kuhusiana na mauaji hayo na aghalabu kutaja majina ya watuhumiwa wa mauaji hayo waliokamatwa ili kuthibitisha kuwa hawana uhusiano wowote na CCM.

    Pia nilitumaini muandishi huyu angeeleza msimamo wa chama cha mapinduzi kuhusu suala hilo na hatua zitakazo chukuliwa dhidi ya Mbowe au mtu mwingine yeyote anaeaminika kuzusha habari hizo (kama ni uzushi).

    Zaidi ya yote CCM inapaswa kujua kuwa utaratibu wake wa kuwalinda na kuwatetea wanachama wake na kuwanyanyasa wapinzani umefanya wahuni, majambazi na wakorofi wengi kujipenyeza katika chama hicho. Matokeo yake ndiyo haya yaliyoanza kujionesha ambapo wahuni wanafanya mambo yanayoipaka matope CCM.

    ReplyDelete
  12. AnonymousMay 09, 2012

    Unajua Nape anayozungumza hayajui,kwavile hayuko humu yanakotokea.Unaposema mauaji haya hayana mkono wa ccm haieleweki kabisa,mie naamini makada wa ccm baada ya anguko hili la arumeru ndio wamekuawakitumia hata kukodi watu wanaofanya uharamia huu.Siku moja ukweli utakuwa wazi na sielewei huyu nape ataweka wapi sura yake naamini kama anakanusha hii damu iliyomwagika isiyo na hatia pamoja na machozi ya familia zilizoachwa yatima damu hiyo itakua juu yako Nape.
    Mungu ni mwaminifu sana na atayafunua yaliyofichwa juu yako nape nauye,ucwe kibaraka wakukumbatia mambo yaliyoko wazi.
    MWISHO.

    ReplyDelete
  13. AnonymousMay 09, 2012

    Uhuru na kazi ndio salamu ninazoanza nazo. Ndg msomaji uliyepita napenda kukujuza tu kuwa katika Chama cha Mapinduzi hakuna sera inayoruhusu raslimali za nchi kuporwa na hakuna Sera inayokumbatia Mafisadi. je ni watu wangapi wanaofikishwa kwenye vyombo vya dola wakishutumiwa na makosa ya ubadhilifu?

    amani na utulivu uliotaasisiwa na Tanu ni wajibu wa kila mtanzania kuuenzi na kuulinda na si kazi ya CCM tu; Chadema mmefanya kazi nzuri ya kutuamsha wananchi lakini katika kutuamsha mnaienzi amani? jibu ni hakuna. haya sasa kabla ya kuinyoshea vidole CCM basi jichunguzeni kwanza nafsi zenu. CCM inaongozwa kikatiba na ni wajibu wa CCM kuwachukulia hatua za kikatiba wale wote wanaokwenda kinyume na katiba ya Chama.

    mwana CCM

    ReplyDelete
  14. AnonymousMay 09, 2012

    Anonymous wa kwanza unasema ukijenga historia ya kitu basi unashabahiana nayo, je Chadema wenye historia ya ukabila na ukanda (to be precise uchaga) na ukristo je, "you deserve to be scrutinized with an equally deserving criticism?".

    ReplyDelete
  15. AnonymousMay 09, 2012

    Safi sana Prof. Mbele,

    Kwani umeeleza vizuri kiasi cha kueleweka.

    Ndugu zetu wanaendelea kupoteza maisha. CCM na serikali yake mmekaa kimya mwee! kama waliokufa ni kuku... Hizi damu zilizoko ardhini hakika haziwezi kufutika katu ninaamini zitaendelea kutulilia na kutuzunguka kwani zilikuwa zikipigania HAKI.

    Naona wenzenu Chadema wameliona hilo na kuamua kulikemea kwa ukali wa aina zote, ndipo naona baada ya matamshi hayo ya kila namna, cha kushangaza ndio polisi wanasema wamewakamata wauwaji woooooote tena kwa wakati mmoja???!!!! Duu! Kazi kweli kweli.

    Ni wazi chama chetu hiki kimepoteza dira na kushindwa kusoma alama za nyakati. Tuige mfano wa Ufarasa, midahalo ya wazi mara kwa mara.

    Mie kila mara hukumbusha kuwa hili ni bomu ambalo tunalitengeneza linaendelea kukua siku hadi siku, likisubiri mkannyagaji.

    PAMBANENI KWA AINA ZOTE LAKINI SI KUPOTEZA UHAI.

    ReplyDelete
  16. Tunazungumzia mauaji ya makada wa CHADEMA na sio maalbino wew ananymous. Usiwe kibaraka wa kuchumia tumbo lako tu na kusahau wenzako,ndo maana unaropoka ovyo. unadhihirisha tabia halis ya Chama chako za kujibu hoja nzito kwa kihoja chepesi kisicho hata na mashiko. huu ni wakati wa kuangalia maslahi ya taifa la Tanzania sio tumbo lako ndugu. usidhani kama utakuwa na amani kwa unapata milo mitatu kwa kufitini haki za wenzio wakati wengine wanateseka na mfumuko wa bei,miundo mbinu mibove,ukosefu wa ajira,matumizi makubwa ya sio na tija kwa serikal etc. Vua gamba Vaa Gwanda sasa. Shime,tujiangalie watanzania,tutajivunia lin rasilimali zetu!

    ReplyDelete
  17. AnonymousMay 09, 2012

    Anonymous wa kwanza unasema ukijenga historia ya kitu basi unashabahiana nayo, je Chadema wenye historia ya ukabila na ukanda (to be precise uchaga) na ukristo je, "you deserve to be scrutinized with an equally deserving criticism?".

    Huyu aliye uliza swali kwa mchangiaji wa kwanza ni mwenda wazimu kabisa. Kitu chochote kikubwa huanzaishwa na watu wachache (like minded people) haijalishi ni kabila au dini gani. Ulitaka CHADEMA ku advertise kuanzishwa kwa chama? Sasa mbona kina viongozi wa makabila na dini tofauti achilia mbali makada nawanachama?

    ReplyDelete
  18. AnonymousMay 09, 2012

    Profesa Mbele acha ushabiki wako na uongo wako wakujidai huna chama, mnafiki chama unacho na dini unayo usitubabaishe hapa, Uliondoka nchini hapa kukimbia ukame wa maisha enzi hizo, unakaa Marekani unakula starehe zako kisha unakuja TZ na visenti vyako kuvuruga amani ya nchi. Aliendika maneno hayo wewe humjui? Nembo ya CCM ipo, kama jina halipo ujue itakuwa imeandikwa toka ofc za CCM sasa shida iko wapi?
    Wewe unajua, CDM wanajua na watu wengi tu wanajua, na mtu yoyote yule mwenye akili hawezi kufikiria chama imara, chenye busara kinaweza kujiingiza kwenye mauwaji ya watu ambao ingawa uhai wao ni muhimu kama mtu mwingine yoyote hawana significance kisiasa wala sio tishio kwa mwana siasa yoyote, sasa how cheap can you people be in your quest to gain power in this country, hivi CCM wange kuwa na umafia huo wangewaacha hao wanobwata bwata hovyo wakawauwe watu ambao hawana hatia wala significance yoyote ya kisiasa, mnataka tu kupotosha Umma. Wao ndio wako on record kuwaua political oponents wao………..yule mbunge alietaka kuwa-expose viongozi wao wa CDM kwa ubadhirifu wao wamali ya chama, hawakumuondoa kule Dodoma kwa ajali? Walimfukuzia nini Kafulilah kwenye chama? He was a threat, naangewa-expose for nepotism, na ukabila na uchafu wote, kamheshimu Zito tu, angeyabwaga yote.
    Kuhusu Mwl, mimi ningependa umuache Mwl apumzike kwa amani na sio wewe tu wote sie tumuache mwl apumzike, mwl alikuwa ni binadamu, hakuwa mtume wala hakutolewa nyongo, hakuwa malaika wala mtakatikatifu, tumuache Allah (SWT) amhukumu kwa amali zake, Amen, tusitumie kauli zake out of context, maana hayuko kujitetea kuwa in what context alisema maneno hayo. Mimi nimeshawahi kwa masikio yangu kumsikia Mwl akihojiwa na CNN maara baada ya kustaafu, aliulizwa je umeachia madaraka kwa vile ujamaa umeshindwa? Mwl akajibu kwa kingereza........ ujamaa umeshindwa kama vile ukatoliki ulivyoshindwa duniani, lakini hii haina maana kama mimi sio mkatoliki, lakini ukweli nikuwa ukatoliki umeporomoka.........haya yalikuwa maneno ya mwl mwenyewe.
    We ni msomi angalau unatufanya tuamini hivyo, mauji yametokea, ni kazi ya police na Mahakama kuamua muuaji ni nani, CDM ndio wa kwanza kuwanyooshea kidole CCM bila ya kuwa na ushahidi wowotena kabla uchunguzi haujakamilika, sasa ulitaka CCM wakae kimya, kwanza tunajuaje kama sio wao wenyewe kwa wenyewe wanauwana kwa nia hiyo ya kutaka siasa za kuhurumiwa, kwanza wao ndio wenye sera za kumwaga damu, au hujui? Au ndio nyie kina penda chongo? Acha hizo prof. kuwa mkweli, kwanza naona maprof wenzio washa kudharau hakuna hata anayekujibu prof mzima kutwa kuandika udaku kwenye mitandao. Nenda magogoni ukapeleke propanganda zako, angalau ni taasisi inayojulikana.

    ReplyDelete
  19. AnonymousMay 09, 2012

    Wewe mwana CCM pole sana mimi pia nina kadi yenu ila ni mwanachama mfu na najuta why niliichukua but soon will handle it to CHADEMA. Unaposema Chadema hawaenzi amani hivi ninyi CCMhaya mambo ya kuwa mnahubiri amani kwavile jeshi la polisi ni kama lenu tu maana mnapoharibu wala hawawakamati mnapotukana wala hamguswi ninyi malaika, CHADEMA wanastahili kufanya wafanyacho maana the police are not impartial mtetezi wao nani wanapoonewa? nakuambia hizi habari za kusema amani inayojengwa na mbinu za kuwatia hofu wananchi ili wasiweze kuongea wla kuhoji uchafu unaofanya nanyi but one day YES yanamwisho tu. Hii habari ya udini na ukanda mnaieneza ninyi wenyewe give me a break tukianza kufuatilia wanaopangwa ukuu wa mikoa na wilaya na wakurugenzai for the past ten years its a shame a shame!!!! ni wa dini gani utajua anayehubiri udini ni nani wengine wanapewa because there is no way as some of the potential staffs to be accomodated have no enough qualifications but the truth is "udini mmeanzisha wenyewe na unawatafuna" Asante sana Prof. kwa kuwaambia ukweli na mkae mkijua hizi shule za kata zitaleta mabaliko ya kweli maana walimu wanajua kuwafundisha watoto kuchanganua kati ya mbivu na mbichi

    ReplyDelete
  20. AnonymousMay 09, 2012

    Profesa Mbele ningependa kuungana na mtoa hoja hapa juu kuwa ni afadhali Mwalimu angeachwa na asiingizwe kwenye siasa chafu za hivi sasa, yeye hayupo kutetea haki yake, na huu uhuru wa kuongea ni wengi watasema jinsi walivyokandamizwa wao au wazazi wao, kisiasa, kiuchumi na maendeleo kwa ujumla kwa siasa na fikira za Mwl Nyerere. Maandishi yake, mawazo yake na maisha yake hayakuwa yakitakatifu wala ya kitume kwa hivyo hayakuwapendeza watu wote, hata hiyo Mitume waliotumwa na Mwenyenzi Mungu na vitabu vyao vitakatifu walivyokuja navyo havikupendwa wala kuaminiwa na watu wote na hatimaye kusulubiwa kwa mwana wa pekee wa Mungu, YESU KRISTO, itakuwa kitabu kilichoandikwa na binadamu? "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania." Ni vitabu vingapi vimeandikwa na wana falsafa na wasomi mbali mbali na hata watu wa kawaida wakitanzania kuhusu hatma ya watanzania baada ya Uhuru wa Tanganyika, siasa ya ujamaa, upendeleo wa kidini, ukandamizaji wa kisiasa, ambavyo vilipigwa marufuku na ni marufuku hapa Tanzania kuwa navyo, hilo ni kosa na ni kosa la kutiwa ndani bila hatia. Wewe Mbele unajua hili kama wewe kweli ni prof na mwandishi wa vitabu, na ni waungwana wengi tu wanaojua ukweli huu si lazima wajitaje, wewe unajitaja ili uonekane kleen, kumbe mnafiki mkubwa, wenzio wanakuvisha kilemba cha ukoka, ufute umande!
    Na Mwl lazima ilikuwa aseme kuwa viongozi wa CCM wamefilisika kisiasa, ni kweli, kwani nani aliyewafilisi? Mwimbo ulikuwa mmoja tu kidumu chama cha mapinduzi zidumu fikira za mwenyekiti, fikira zile sasa bado zimedumu kwenye fikra za watu wengine kama wewe kwa mfano, sasa kwa wengine wameendelea na utandawazi, mabadiliko ya kisiasa na ndio maana unaona watu kama kina Mbowe na wenzake wanaweza kusimama kwenye majukwa wakatabiri na kudhamiria kumwagika kwa damu, kujitenga kwa ukanda na hoja za wajumbe wakiislam kuwe wengi kwenye tume ya katiba (kwa hiyo udini), bila ya kuchukuliwa hatua yoyote, akina kalaga baho na ubwezi wenu mnapiga makofu tena. Sasa wanaona kimya wanawala wenyewe watu wao nyama huko Arusha wanajidai CCM imewauwa, na yule bibi wa miaka 75 aliekutwa akiwanga huko alikuwa kada wao?, si wawapeleke mahakamani basi kama Mtikila anavyofanya?
    Sasa watu mliofilisika kimawazo ndio hamkawii kutumia maandishi ya Mwalimu na kujidai kumuenzi, kama mnamuenzi mwachani apumzike wakati mchakato wa kumfanya mtakatifu unaendelea, msije mkaharibu.

    ReplyDelete
  21. AnonymousMay 10, 2012

    Mwalimu angeachwa na asiingizwe kwenye siasa za hivi sasa, yeye hayupo kutetea haki yake, na huu uhuru wa kuongea ni wengi watasema jinsi walivyokandamizwa wao au wazazi wao, kisiasa, kiuchumi na maendeleo kwa ujumla kwa siasa na fikira za Mwl Nyerere. Maandishi yake, mawazo yake na maisha yake hayakuwa yakitakatifu wala ya kitume kwa hivyo hayakuwapendeza watu wote, hata hiyo Mitume waliotumwa na Mwenyenzi Mungu na vitabu vyao vitakatifu walivyokuja navyo havikupendwa wala kuaminiwa na watu wote na hatimaye kusulubiwa kwa mwana wa pekee wa Mungu, YESU KRISTO, itakuwa kitabu kilichoandikwa na binadamu? "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania." Ni vitabu vingapi vimeandikwa na wana falsafa na wasomi mbali mbali na hata watu wa kawaida wakitanzania kuhusu hatma ya watanzania baada ya Uhuru wa Tanganyika, siasa ya ujamaa, upendeleo wa kidini, ukandamizaji wa kisiasa, ambavyo vilipigwa marufuku na ni marufuku hapa Tanzania kuwa navyo, hilo ni kosa na ni kosa la kutiwa ndani bila hatia. Wewe Mbele unajua hili kama wewe kweli ni prof na mwandishi wa vitabu na ni waungwana wengi tu wanaojua ukweli huu si lazima wajitaje, wewe unajitaja ili uonekane kleen, kumbe mnafiki mkubwa, wenzio wanakuvisha kilemba cha ukoka, ufute umande!
    Na Mwl lazima ilikuwa aseme kuwa viongozi wa CCM wamefilisika kisiasa, ni kweli, kwani nani aliyewafilisi? Mwimbo ulikuwa mmoja tu kidumu chama cha mapinduzi zidumu fikira za mwenyekiti, fikira zile sasa bado zimedumu kwenye fikra za watu wengine kama wewe kwa mfano, sasa kwa wengine wameendelea na utandawazi, mabadiliko ya kisiasa na ndio maana unaona watu kama kina Mbowe na wenzake wanaweza kusimama kwenye majukwa wakatabiri na kudhamiria kumwagika kwa damu, kujitenga kwa ukanda na hoja za wajumbe wakiislam kuwe wengi kwenye tume ya katiba (kwa hiyo udini), bila ya kuchukuliwa hatua yoyote, akina kalaga baho na ubwezi wenu mnapiga makofu tena. Sasa wanaona kimya wanawala wenyewe watu wao nyama huko Arusha wanajidai CCM imewauwa, na yule bibi wa miaka 75 aliekutwa akiwanga huko alikuwa kada wao?, si wawapeleke mahakamani basi kama Mtikila anavyofanya?
    Sasa watu mliofilisika kimawazo ndio hamkawii kutumia maandishi ya Mwalimu na kujidai kumuenzi, kama mnamuenzi mwachani apumzike wakati mchakato wa kumfanya mtakatifu unaendelea, msije mkaharibu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...