Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Ludovick Utouh akisaini katika kitabu cha wageni, wakati alipoutembelea ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, na kuzungumza na maafisa wa Ubalozi
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Ludovick Utouh, akifafanua jambo wakati wa mazungumzo yake na Naibu Katibu Mkuu, Asha- Rose Migiro. Bw. Utouh akiongoza ujumbe wa watu watatu kutoka Ofisi yake alikuwa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa Ziara ya Kikazi ikiwa ni sehemu ya Maandalizi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kuingia kwenye Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa mataifa kuchukua nafasi inayoachwa wazi na Afrika ya Kusini. Tanzania inaingia kwenye Bodi hiyo mwezi Julai mwaka huu.
Bw. Otouh akiwa na Naibu Katibu Mkuu mara baada ya mazungumzo yao alipomtembelea Naibu Katibu Mkuu ofisini kwake
CAG akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, kutoka kushoto ni Mkuu wa Utawala Bw. Modest Mero, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Nje, Bw. Fransis Kitauli, CAG, Kaimu Balozi, Bibi Maura Mwingira, Bw. Salhina Makumba, Naibu Mkurugenzi ukaguzi wa nje , Bibi Salome Mollel, Mkurugenzi wa Utawala Ofisi ya Mdhibiti na Bw. Justin Kisoka afisa ubalozi anayehusika na Kamati ya Tano ya Bajeti na Utawala ya Umoja wa Mataifa
Naibu Katibu Mkuu na CAG akiwa katika picha ya pamoja na kutoka kushoto, Bw. Justin Kisoka afisa wa Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa anayehusika na Kamati ya Tano ya Masuala ya Bajeti na Utawala, Bw.Fransis Kitauli, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Nje, kulina kwa Naibu Katibu Mkuu ni, Bw. Salhina Mkumba Naibu Mkurugenzi ukaguzi wa nje na Balozi Tuvako Manongi msadizi wa Naibu Katibu Mkuu.
Na Mwandishi Maalum
New York
Ikiwa imebaki takribani miezi miwili kabla ya Tanzania kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( NAOT) kuingia rasmi katika Ujumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa ( UNBOA). Mkuu wa chombo hicho, Bw. Ludovick Utouh anasema yeye binafsi na ofisi yake amekwisha kujipanga vema kulikabili jukumu hilo.
Bw, Utoh ameyaeleza hayo siku ya alhamisi wiki hii wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Asha- Rose Migiro alipomtembelea ofisi kwake . Bw. Utouh yupo hapa Umoja wa Mataifa akifuatana na wasaidizi wake watatu kwa ziara ya kikazi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awali kujiunga na Bodi hiyo.
Katika mazungumzo hayo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali, amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu kwamba yeye binafsi anatambua ukubwa wa kazi inayomkabili mbele yake, na dhamana anayoibeba kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watanzania wote.
“ Tanzania tumeaminiwa, sifa zetu zinafahamika na ndiyo maana tukapendekezwa kuingia kwenye Bodi hii . Tumejianda na kujipanga, tutatumia uwezo wetu na maarifa yetu kulikabili jukumu hili na heshima hii tuliyopewa” akasisizia Bw. Utouh.
Akaeleza zaidi kwa kusema kwamba, yeye na wataalamu wake, na kwa kushirikiana na wajumbe wengine wa Bodi hiyo, watalitekeleza jukumu hilo kwa uwazi na siyo kuviziana.
“ Tumejipanga kuifanya kazi hii kwa misingi na taratibu zote zilizoweka , tutafanya ukaguzi kwa uwazi, tutajadiliana na wahusika, na siyo kuviziana lengo ni kuboresha utendaji wa chombo hiki muhimu” akasisitiza
Na kuongeza. “Jambo la msingi na muhimu ni lazima kuwepo mawasiliano mazuri pamoja na kuheshimiana na siyo kuviziana au kuumbuana. hapana, siyo ajenda yetu. Tutaangalia wapi kuna matatizo na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kurekebisha kasoro hizo”.
Akabainisha zaidi kwa kusema, ukaguzi wa kuviziana na kuumbuana umeshapitwa na wakati. “Ukaguzi wa kuviziana ni wa kizamani hata nyumbani ( Tanzania) hatufanyi aina hiyo, tumeendelea, tunafanya ukaguzi wa viwango, tunajadiliana , kuelekezana na siyo kuviziana au kukomoana tunataka kujenga na si kubomoa” akasisitiza
Akifafanua zaidi kuhusu maandalizi ambayo ofisi yake imekwisha kufanya, ili kuwajenga uwezo mpana wataalamu wake, ameyataja maandalizi hayo ni pamoja na kuwapatia mafunzo ya vitendo na mitihani maafisa wake, kufanya ziara za kikazi, kuhudhuria mikutano ya kimataifa inayohusiana na masuala ya ukaguzi wa hesabu ikiwamo ziara hii ya kikazi ambaye yeye na maafisa wake wameifanya hapa Umoja wa Mataifa.
Katika Mazungumzo hayo, Naibu Katibu Mkuu Asha- Rose Migiro alimpongeza Bw. Utouh, Ofisi yake na Serikali kwa ujumla kwa kupata fursa hiyo ya kuingia kwenye Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.
Akasema kuwa, Tanzania imekuwa mfano wa kuingwa katika Bara la Afrika katika eneo hilo la Ukaguzi wa mahesabu kiasi cha kutambuliwa na Umoja wa Mataifa.
Migiro akaeleza kuwa Umoja wa Mataifa utatoa ushirikiano wa karibu kwa wajumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya UM katika utekelezaji wa majukumu waliyopewa.
Akabainisha kwamba dunia hivi sasa inapita katika kipindi kigumu cha kuyumba kwa uchumi na kwamba kila senti inayopatikana inatakiwa kutumiwa kwa uangalifu..
“ Tunapita katika kipindi kigumu, hali ya uchumi ni ngumu na imewakwaza hata wachangiaji wakubwa wa UM, lakini hali ni mbaya pia hata kwa wachangiaji wadogo, na ndio maana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa akisisitiza sana kuwa na matumizi bora na sahihi kwa kila senti inayopatikana”.
Kwa sababu hiyo akasema, kwa Tanzania kujiunga katika Bodi hii, itasaidia sana katika kutoa ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha uwajibikaji na uwazi”. akasititiza Migiro.
Akiwa hapa Umoja wa Mataifa, Bw. Utouh na ujumbe wake pamoja na kukutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu pia amekutana na baadhi wa wakuu wa mashirika ya UM wakiwamo watendaji wa UNDP, UN-Women, Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu, wajumbe wa Kamati ya Tano inayohusika na masuala ya bajeti na utawala na wataalamu mbalimbali.
Wakati wa mazungumzo na watendaji hao, walielezea kufurahishwa kwao na hata kushangazwa na namna Bw. Utouh alivyoonyesha uelewa wa hali ya juu kuhusu masuala ya fedha na uhasibu wa UM lakini kubwa zaidi namna walivyojipanga kabla hata ya muda wa kuchukua ujumbe huo haujafika jambo lililoonyesha wazi kwamba Tanzania imejipanga na inajua nini inachotarajiwa kukifanya.
Akitoa tadhimini yake kuhusu ziara yake hiyo ya kikazi, Bw. Utouh anasema ingawa ratiba ilikuwa imebanana sana lakini katika muda mfupi amewezea kujifunza mambo mengi, na kupata picha ya hali halisi ya mambo jambo ambalo anasema limemweka yeye na wataalamu wake katika nafasi nzuri zaidi ya kiutendaji.
Mwishoni mwa mwaka jana, Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa lilipitisha uteuzi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa.
Tanzania inachukua nafasi inayoachwa wazi na Afrika ya Kusini mwezi Julai mwaka huu na itafanya kazi na wajumbe wengine wawili wa Bodi hiyo kutoka Uingereza na China. Tanzania itadumu kwenye bodi hiyo kwa kipindi cha miaka sita. Aidha Tanzania inakuwa nchi ya tatu kutoka Afrika baada ya Ghana na Afrika ya Kusini kuwa mjumbe wa Bodi ya Wahasibu ya Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya majukumu ya Bodi ya Wahasibu ya Umoja wa Mataifa ni kukagua vitabu vya hesabu za Makao Makuu ya UM, Mashirika na Asasi zote zilizochini ya UM, Misheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa na miradi mbalimbali inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa
Bodi hiyo hukutana mara mbili kwa mwaka katika miezi ya Juni na Novemba ingawa wanaweza kukutana wakati wowote pale wanapohitajika. Aidha wajumbe hao watatu watasaidiwa na wakurugenzi watatu kutoka nchi hizo. Makazi ya wakurugenzi hao na ofisi zao zakudumu zitakuwa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Mh. umeweka sana sana heshima yako na taifa kwa ujumla hongera sana.
ReplyDeleteTatizo ni serikali sidhani kama watawachulia hatua mafisadi waliotafuna fedha zetu kama mchwa!
Hivi UN hawakuona watanzania wengine wa kuwateua zaidi ya Migiro na Utuoh ambao ni Wakilimanjaro na Wakaskazini??
ReplyDeleteJamani tujifunze kufahamu mambo kabla ya kuchangia. Uteuzi wa CAG kukagua UN siyo 'as a person' ni institution yaani ni ofisi ya taifa ya ukaguzi Tanzania. So hata akistaafu atakayekuja ukaguzi utaendelea for 6 years.
ReplyDelete