JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALI 

TAARIFA KWA UMMA


UWEKEZAJI KWENYE MAENEO YA MALIAKALE UNARUHUSIWA



Wizara ya Maliasili na Utalii imefafanua kuwa kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008 (Kifungu cha 4.5 na 46), wananchi, taasisi mbalimbali, pamoja na wadau wengine wa uhifadhi wanaruhusiwa kumiliki, kulinda, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho kwa sababu za mafunzo, historia na utalii. Sera pia inaruhusu uwekezaji katika maeneo ya malikale ambao unalenga kuhifadhi na kutumia rasilimali za malikale kama vivutio vya utalii.

Ufafanuzi huu umetolewa kufuatia habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku kuhusu mwekezaji kumilikishwa isivyo halali eneo lenye magofu ya kihistoria la kisiwa cha Chole kilichopo wilayani Mafia ambayo sasa yanatumika kama sehemu ya hoteli ya kitalii.

Wizara kupitia Idara ya Mambo ya Kale inatambua kuwa magofu ya kihistoria katika kisiwa cha Chole ni Kumbukumbu za Urithi wa Utamaduni yenye umuhimu kitaifa na kimataifa na Magofu haya yanalindwa na Sheria ya Mambo ya Kale Na. 10 ya mwaka 1964 na marekebisho yake Na 22 ya mwaka 1979. Idara inawajibika kusimamia uhifadhi na uendelelezaji wake kulingana na kanuni na miongozo ya uhifadhi na uendelelezaji.

Wizara inasisitiza kuwa siyo maeneo yote ya urithi wa utamaduni yanasimamiwa na Idara ya Mambo ya Kale moja kwa mojaMaeneo ya urithi wa utamaduni yenye sifa za kitaifa ni mengi lakini 12 tu ndiyo yanayomilikiwa na Serikali Kuu na kuendelezwa na Idara ya Mambo ya KaleMaeneo yaliyo mengi yanamilikiwa na watu binafsi, taasisi za umma na binafsi na vijiji au wilaya. Kwa mfano, Magofu ya Chole, Mafia hayapo chini ya umiliki wa Idara ya Mambo ya Kale moja kwa moja bali yapo chini ya umiliki wa wilaya na serikali ya kijiji cha Chole.

Hivyo Wizara haijahusika kuimilikisha kampuni ya “Chole Mjini Conservation and Development Company Limited” eneo lenye magofu ya kihistoria la Chole wala kutoa kibali cha kujenga hoteli katika kijiji hicho.

Hata hivyo, kutokana na taratibu zilizopo Wizara ilihusika kutoa kibali cha ukarabati wa magofu hayo (Kumb. Na. EA. 270/297/01/33) baada ya mmiliki kutimiza masharti ya kuwasilisha taarifa zifuatazo:-

       Uhalali wa umiliki wa jengo au eneo;
       Taarifa ya kitalaamu inayoonyesha hali halisi ya jengo na mahitaji ya kufanyia ukarabati au mabadiliko ya matumizi;
       Michoro/ramani za jengo linavyoonekana sasa na ramani zinazoonyesha maboresho yatakayofanyika wakati ya ukarabati; na
       Albamu ya picha inayoonyesha hali ya jengo kwa sasa na maeneo ambayo yanahitaji kukarabatiwa au kuboreshwa.

Baada ya masharti kutimizwa Chole Mjini Conservation and Development Company Limited ilipata kibali cha ukarabati kilichoambatana na miongozo ya uhifadhi ambayo mwekezaji alitakiwa kuifuata, na kazi ya ukarabati ilifanyika chini ya usimimamizi wa Wizara. Wizara ilihusika ili kuhakikisha kuwa ukarabati unafanyika bila kubadilisha mwonekano wa majengo husika uliokuwepo hapo awali.

Wizara inawahamasisha watu binafsi, mashirika na asasi mbalimbali kuwekeza katika sekta ya malikale mradi taratibu za kisheria za kupata eneo husika na kulikarabati zifuatwe. Uwekezaji huo ni utekelezaji wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008 inayotaka Idara ya Mambo ya Kale kushirikikisha wadau katika kuendeleza maeneo ya malikale.

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
25/05/2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...