Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi akipokea toka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Augustino Nanyaro, kabrasha la mada mbalimbali zitakazojadiliwa wakati wa Mkutano wa siku tatu wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza ulioanza leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza baada ya kufungua mkutano wao, jijini Dar es Salaam, leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Augustino Nanyaro, baada ya kufungua mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza, jijini Dar es Salaam, leo.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amewaagiza maofisa wa Jeshi la Magereza nchini kuhakikisha wafungwa waliopo magerezani wanapata mafunzo mbalimbali ili wamalizapo kutumikia vifungo vyao wasiyarudie tena makosa yaliyosabisha kufungwa.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Maaskofu (TEC) Kurasini, jijini Dar es Salaam, Dk Nchimbi alisema kwa mujibu wa ufuatiliaji wake, kati ya asilimia 30 hadi 35 ya wahalifu wanaokuwepo magerezani wanarudia makosa ya uhalifu wamalizapo vifungo vyao.

“Hali hii siyo nzuri na ni changamoto ya kitaifa kwani inaashiria tatizo la kijamii linalohitajika kufanyiwa kazi kwa pamoja baina ya vyombo vya Haki Jinai na jamii yenyewe, kwa utaratibu maalumu,” alisema Dk Nchimbi na kufafanua;

“Pia ufuatiliaji wangu unaonyesha kwamba, taaluma ya uendeshaji wa wahalifu inahitaji kuwepo kwa programu za urekebishaji wa wahalifu ambao wataalamu wanapompokea mhalifu gerezani hufanya utambuzi wa vyanzo na sababu za mtu kutenda makosa ya kihalifu na kisha kumwandalia utaratibu maalumu wa mafunzo ya aina mbalimbali kulingana na mahitaji yake ili atakapomaliza kifungo asihalifu tena.”

Kutokana na hali hiyo, Dk Nchimbi alitoa agizo kwa Kamishna Jenerali wa Magereza pamoja na wajumbe waliohudhuria mkutano huo, waandae mikakati madhubuti ya kutekeleza sayansi ya urekebishaji wa wahalifu katika eneo la programu za urekebishaji.

Hata hivyo, alisema licha agizo hilo kuwa zito lakini aliutaka uongozi wa jeshi hilo kujenga hoja kupitia andiko maalumu kwa kuainisha mahitaji ya kutekeleza azma yao, na kuwaahidi kuwaunga mkono na kusaidiana nao katika kuwajengea uwezo wa kutekeleza.

Alisema endapo hatua hiyo itafanikiwa kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza msongamano mkubwa wa wafungwa katika magereza mbalimbali nchini.

Aidha, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Fidelis Mboya alisema mkutano huo wa siku tatu, unahudhuriwa na zaidi ya Maofisa Magereza 60, wakiwema kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Wakuu wa Magereza wa Mikoa, Wakuu wa Vyuo, Mkuu wa Kikosi Maalumu pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwawani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 07, 2012

    Bongo tambarare sana-hata ukipata PhD YA MAGUMASHI BADO WATAKUITA dkt....

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...