Meneja Masoko na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Angela Mziray (kushoto),akimkabidhi sh. 500,000, Kaimu Mhariri Mkuu wa Jambo Leo, Julian Msacky, Dar es Salaam leo, kwa ajili ya rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Mhariri Mkuu wa gazeti hili marehemu Willy Edward, aliyefariki mkoani Morogoro ambaye mwili wake utaagwa viwanja vya Mnazi Mmoja leo na kisha kusafirishwa hadi nyumbani kwao Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara kwa mazishi. Wa pili kushoto ni Ofisa Mwandamizi wa NHIF, Luhende Singu na Ofisa wa Habari wa mfuko huo, Grace Michael. (PICHA NA DOTTO MWAIBALE)
Na Grace Michael
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepokea kwa masikito makubwa kifo cha Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo, Willy Edward Ogunde ambaye alikuwa ni miongoni mwa wadau muhimu wa Mfuko huo.
Willy Edward enzi za uhai wake alitoa kipaumbele katika kuuhabarisha umma kwa kutoa habari zinazohusiana na sekta ya Afya hususan za kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Mfuko utaendelea kukumbuka na kuenzi yote yaliyofanywa na Willy kupitia nafasi yake ya uhariri katika gazeti la Jambo Leo.
Marehemu kwa mara ya mwisho alihudhuria mkutano wa saba wa waandishi waandamizi na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika mjini Morogoro mkutano ambao hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwaelimisha juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mfuko.
Kutokana na hayo, wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wanaungana na tasnia ya habari, familia, ndugu na jamaa kuomboleza msiba wa mhariri huyo.
Akimzungumzia marehemu, Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), Athuman Rehan, alisema kuwa marehemu alikuwa ni mtu mtulivu na aliyependa kushirikiana na wenzake kwa hali na mali hivyo kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa tasnia ya habari.
Katika kufanikisha shughuli za msiba, Mfuko umetoa rambi rambi yake kupitia uongozi wa Jambo Leo. Mungu ailaze roho yake pema poponi amina.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...