Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akiwa na Msaidizi wake Mkuu wa Karibu, Naibu Katibu Mkuu, Asha-Rose Migiro pamoja na watendaji wengine wa Taasisi za Umoja wa Mataifa, wakati wa hafla ya uzinduzi wa tovuti itakayotumika kufuatilia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) pamoja na ahadi za fedha na kisera ambazo zimetolewa na zile ambazo hazijatolewa na nchi wanachama na taasisi mbalimbali. Tovuti hiyo inajulikana kama http://iif.un.org na inaweza kutumiwa na mtu yoyote na mahali popote alipo ulimwenguni.
Na Mwandishi Maalum
Wakati ikiwa imebakia takribani miaka mitatu kufikia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Millenia ( MDGs). Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amezindua mtandao utakaotumika kufuatilia ahadi zote zikiwamo za fedha na za kisera ambazo zimetolewa ili kuchagiza utekelezaji wa malengo hayo.
Akizindua mtandao huo siku ya Jumatano hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amesema kuanzia siku hiyo kuna chombo ambacho kinamuwezesha mtu yeyote popote alipo duniani kufutalia ahadi zote zilizotolewa ili kufanikisha upunguzaji wa umaskini kupitia utekelezaji wa MDGs.
“ Kuanzia leo hii, tunacho chombo ambacho ni rahisi kutumiwa na mtu yeyote na mahali popote alipo duniani, ni kama duka moja kubwa ambapo tunaweza kufuatilia ahadi zilizotolewa na nchi wanachama na taasisi mbalimbali kusaidia kufikia malengo ya maendeleo ya millenia” akasema Ban Ki Moon.
Uzinduzi wa tovuti hiyo ambayo kwa kimombo inajulikana kama Intergrated Implementation Framework (IIF), ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro, ambaye ndiye msimamizi na mfuatiliaji mkuu wa utekelezaji wa MDGs.
Akizungumzia zaidi kuhusu utekelezaji wa malengo nane ya MDGs, Katibu Mkuu amesema nchi nyingi zimepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa malengo hayo katika maeneo kama vile ya upunguzaji wa vifo vya watoto wachanga, elimu kwa wote kudhibiti maambukizi ya virusi vya ukimwi, kifua kikuu na malaria, na usambazaji wa maji safi na salama.
Akasema kwa hatua ambazo zimefikiwa na mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukabili umaskini uliokidhiri. na ingawa bado kunachangamoto nyingi, lakini ni dhahiri kwamba licha ya hali ngumu inazoikabili nchi nyingi kuna matumaini ya kupiga hatua na kufanya vizuri zaidi.
Lakini akaonya kwa kusema “ Tunaposhindwa kutekeleza ahadi zetu kwa ukamilifu wake, uwajibikaji wetu mbele ya macho ya watu tunaowahudumia unakuwa na walakini.
Na kuongeza kwamba ingawa ni ukweli pia kwamba tovuti hii haiwezi kuwa suluhu ya kutatua changamoto zinazotukabili. Lakini itasaidia kuainisha mapungufu yaliyopo, utoaji wa taarifa za asili ya ahadi zilizotolewa, kufuatilia utoaji wa ahadi hizo na kuainisha mapengo kati ya ahadi zilizokwisha kutolewa na ambazo hazijatolewa na zinazohitajika ili kufikia utekelezaji wa MDGs.
Akasisitiza kwamba IIF itasaidia sana katika kuongeza uwajibikaji na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa. Na akaelezea matumaini yake kwamba wadau wote zikiwamo nchi wanachama, taasisi za Umoja wa Mataifa, sekta binafsi na asasi za kiraia wataitumia kikamilifu tovuti hiyo.
Tovuti hiyo licha ya kutumiwa na nchi wanachama wa UM, pia itatumiwa na watunga serĂ¡, wasomi, watafiti na vyama vya kiraia katika kuunga mkono utekelezazi wa MDGs na kuibua majadiliano kuhusu kitakachofuata kuhusu ajenda nzima ya maendeleo baada ya 2015.
Aidha na kwa mujibu wa Ban Ki Moon, tovuti hiyo pia itasaidia ufuatiliaji wa ahadi zitakazotolewa katika mkutano wa Kimataifa wa maendeleo endelevu na mazingira maarufu kama RIO+20 utakaofanyika wiki mbili zijazo huko Rio de Janeiro nchini Brazil.
Tovuti hiyo ya IIF imefadhiliwa kupita michango ya hiari iliyotolewa na Serikali za Canada, Nigeria na Jamhuri ya Korea.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...