Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO katika kikao chake cha 36 kinachoendelea (tarehe 24 June hadi 6 Julai 2012) katika jiji la Saint Petersburg nchini Russia imelikubali ombi la Tanzania la kuurekebisha mpaka wa Pori la Akiba la Selous, ambalo ni Eneo la Urithi wa Dunia, ili kuruhusu uchimbaji wa Madini ya Urani. Eneo linalohusika ni asilimia 0.8 ya eneo la Pori la Akiba la Selous

Kwa mara ya kwanza ombi hilo lilipelekwa kwa Kamati hiyo ya Urithi wa Dunia ya UNESCO mwezi Januari 2011 ambapo lilijadiliwa katika Kikao chake cha 35 ambacho kilihamishia mjadala huo katika Kikao cha 36 kinachoendelea.

Uamuzi huo ulifanyika ili kuruhusu Tathmini ya Athari ya Mazingira (EIA) kukamilishwa na kutoa muda kwa wataalam wa IUCN kufika eneo linalihusika ili kuliona na kuhakiki taarifa ya tathmini hiyo.

Pori la Akiba la Selous ambalo lina ukubwa wa Kilomita za Mraba 50,000 ni mojawapo ya hifadhi kubwa duniani zenye viumbe mbalimbali. Ni eneo maarufu kwa nyanda kubwa za tambarare zenye nyasi na misitu ya miombo pamoja na aina nyingi za wanyamapori.

Kufuatia kukubaliwa kwa ombi hilo la nchi yetu nachukua fursa hii kutoa shukrani kwa Kamati ya Urithi wa Dunia, IUCN, Kituo cha Urithi wa Dunia na taasisi mbalimbali, pamoja na watu binafsi ambao walichangia katika kulifanya ombi letu kukubaliwa.

Uamuzi uliotolewa na Kamati ya Urithi wa Dunia utatupatia uwezo na fursa nzuri ya kutimiza malengo yetu kiuchumi na kijamii kwa wananchi. Pia tutapata uwezo wa kulihifadhi na kuliendeleza vyema zaidi Pori la Akiba la Selous.

Mhe Khamis Suedi Kagasheki
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
4 Julai 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 04, 2012

    Mradi tusichonge mzinga

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 04, 2012

    Sasa mbona kule serengeti mmetunyima barabara mkidai wanyama watakufa? Tulishatoa mapendekezo kuwa barabara ya serengeti ichimbwe chini kwa chini hakutakuwa na athari kwa wanyama lakini hao UNESCO na Frankfurt wameng'ang'ania msimamo wao kwa vile wanajua Kenya watakosa maslahi (ambayo nao wanayo) kama barabara hiyo ikijengwa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...