Napenda kuwashukuru wadau kibao waliounga mkono wazo la kuwa na mada hii kila wiki ili kujipiga msasa na pia kujadiliana kuhusu hili na lile.
Mada yangu ya kwanza wiki iliyopita iligusia swali la ni kamera ipi iliyo bomba zaidi kuliko zimngine? Mie jibu la haraka haraka sikuwa nalo kwani ninavyofahamu mimi kamera bomba ni ile unayoweza kuimudu kuinunua, na pia lazima kwanza uainishe unataka kuitumia kwa shughuli gani kabla ya kujitosa dukani. Kutokana na ukimya nahisi somo lilieleweka. Asanteni sana kwa hilo.
Mada yangu ya leo ni simpo tu kama ile ya kwanza. Nayo ni je, mtu ufanyeje ama uitumie vipi kamera yake ili kuweza kupiga picha vizuri? Jibu hapa ni kama la wiki iliyopita. Tafadhali usikimbilie kukamata kamera na kuanza kubofya. Jipeleleze kwanza kabla ya kupiga hiyo picha. Namaanisha nini kwa kusema hivyo? Tulia nitajaribu kufafanua.
Unajua, aghalabu wadau wengi wanadhani kupata picha nzuri ni kwenda tu dukani na kununua bonge moja la kamera la bei mbaya, la automatic, na kuanza kufyatua kama hawana akili nzuri. Tatizo ni kwamba mwisho wa siku mdau anajikuta picha sio nzuri kama alivyotarajia.
Hakuna kitu muhimu katika kupata picha nzuri kama kujiandaa kisaikolojia. NDIO. KISAIKOLOJIA. Kujiandaa huko kuna mambo kadhaa ambayo napenda kuyaweka bayana kabla hujaanza kuhofu kwamba nataka kupoteza mtu hapa.
Ni kwamba, unapokamata kamera mkononi, kabla ya kuanza kubofya na kupiga picha, yafaa ujiulize maswali yafuatayo: Je, unaujua uwezo wa kamera yako? Je, ni nani unayetaka aione hiyo picha yako? Je, ni nini unachotaaka kionekane zaidi ya vingine? Ukiweza kuyajibu maswali hayo, amini usiamini, itakuwa vichekesho kama utashindwa kupata picha nzuri.
Tuanze na kuujua uwezo wa kamera yako.
Naam, kila unaponunua kamera kunakuwa na vijikaratasi ndani ya boksi lake vinavyokueleza kinagaubaga una kamera ya aina gani mkononi mwako, na ina uwezo gani. Usivibeze vikaratasi hivyo. Ni muhimu ile mbaya katika kujibu swali hilo. Acha uvivu, na wala usijifanye mjuaji. Soma kwa makini kila kilichomo humo kabla ya kukurupuka na kuanza kupiga picha. Hata kama maelezo katika vijikaratasi hivyo yatakuwa magumu kwako, jitahidi kwenda taratibu uyaelewe. Yaani, ukielewa japo nusu yake tu, utakuwa njia moja kuelekea kule uendako. Fanyia mazoezi hayo maelezo nawe hutakosea. Mradi kumbuka, acha uvivu na papara nawe utafanikiwa tu.
Juu ya nani unayetaka aione hiyo picha yako ama zako, nayo ina umuhimu wake pia. Hapa nazungumzia namna ya mpangilio wa taswira yako (composition) na ni nini unachotaka kusema kwa picha yako hiyo, na kwa nani.
Mfano; unachukua kamera na kuiweka jichoni. Kabla ya kubofya, jiulize (baada ya kujua uwezo wake – kwa kusoma maelezo kwenye vijikaratasi), hii picha ataiona nani? Na unataka kuonesha nini? Hapa namaanisha, unapopiga picha angalia kwa makini kwenye kitundu cha kuonea na kabla ya kubofya jiridhishe kwamba unachotaka kuonesha kinaonekana vyema kwa kupewa kipaumbele.
Mfano; ni hepi besdei ya kuzaliwa mtoto wako na ni siku ya kwanza nawe upo wodini kutaka kukamata kumbukumbu hiyo. Kumbuka, stelingi hapa ni kichanga na mama yake anafuatia. Hivyo lenga kamera yako zaidi kwa kichanga, mama akiwa pembeni kwa chati. Yaani kichanga kionekane kwa ukubwa mwili mzima kwa kuwa umbo lake ni dogo, na kwamba ni yeye mwenye kuenziwa siku hiyo. Usikurupuke na kuanza kupiga picha mama na kitanda kizima ambapo kichanga kitaonekana kiduchu dhidi ya mama na kitanda.
Vile vile, usisahau kujiuliza. Je, picha hii wakipelekewa wazazi ama wakwe na mashemeji, watachotaka kukiona ni nini hasa. Ni kitanda Walicholalia mama na mtoto ama kichanga kilichozaliwa, ambacho hata babu na bibi watakuwa na hamu kuona kafanana na nani…ama anaonekanaje? Hahahahaaaaaa….
Tumia mbinu hizi rahisi hata kwa taswira zinginezo. Mfano; unapotaka kupiga picha nyumba yako mpya wakaione nduguzo na wazazi, kuna haja gani nyumba ionekane kiduchu wakati picha inatawaliwa na sehemu ya mbele? Hapo, kumbuka, stelingi ni nyumba kama ilivyo, na sio bustani ama vichaka mbele ya nyumba. Kama unataka kuonesha bustani na mazingira yanayozunguka nyumba, yafanye hayo kuwa ndio stelingi wa picha yako, huku nyumba ikiwa kwa nyuma. Hapo utaeleweka.
Na kama unapiga picha ya familia, kuna haja gani vikorokoro vingine kama meza, viti na dirisha kule nyuma viwe vikubwa kuliko nyuso za wanafamilia? Wewe hapa unataka kuonesha wanafamilia, kwa nini mimeza na miviti iwe mbele? Jipeleleze kabla ya kubofya mdau!
Kwa leo naomba niishie hapa kwa kushajihisha kwamba unapotaka kupata picha nzuri zingatia yale maswali mawili kwanza kabla ya kubofya, huku ukimkumbuka kwamba picha ina uwezo wa kueleza maneno 1000. Tatizo linakuja kama unataka kuyaeleza hayo maneno 1000 kwa mpigo. Kila mara tafuta eneo kuu na lipe kipaumbele, kama mifano hiyo ya kichanga na nyumba. Pia usiwe na papara na acha uvivu – soma yote yaliyo katika vijikaratasi vya maelezo. Kama hujaelewa uliza wazoefu.
-ANKAL
swadakta!!!
ReplyDeleteankal unalala saa ngapi?maana mi ndo naingia kukitanda mda huu
ReplyDeleteAsante sana kwa muhtasari huu mzuri.
ReplyDeleteItabidi mwisho wa siku, utuandikie kitabu kwa ajili ya hao ambao hawajaweza kukupata huku kwenye blog.
Ramadhan Kareem
Ahsante Ankal kwa somo la leo, Mungu akupe nguvu katika kazi yako na akulipe kwa nia yako njema ya kutufahamisha lile unalolifahamu. Huu ni uzalendo halisi, sio fotokopi kama ule wa majukwaani.
ReplyDeleteAhsante sana, na hongera zako.
Nimekupata vilivyo ANKAL, Shukran sana......kweli wewe ni PROFESHENO wa haya masuala ya photography!!!! Please keep up the good darasa....tuko wengi ambao tulikuwa hatuyaelewi haya.
ReplyDeletewelldone ankle, unasema maneno kama mwalimu una uwezo mkubwa wa kusomesha. kweli mfano wa kichanga na nyumba umenikosha kweli, mapori na vitanda havina sababu ya kuonyeshwa kwenye taswira ya picha. tunafutilia kwa karibu somo lako la upigaji picha nzuri. Mwisho wa siku utatwambia wapi kamera bomba zinapatikana hapa Dar. Nakutakia kila la kheri. Mdau uliyekutana naye sabasaba 2012.
ReplyDeleteSawasawa mwalimu, tuko pamoja...
ReplyDeleteAnkal Mjanja sana!
ReplyDeleteUpo kama 'Banker' kila kitu unafanya kwa tija!
Yaani unatupiga bao kwa kuvuna THAWWABU za Mwezi wa Ramadhani kwa kutoa Darasa la kupiga picha?
Inshallah Mungu akulipe kwa hilo.
Ankal ndio upo katika kuvuta Swaummu nini?
ReplyDeleteDarsa nyingi!!!
Hongera sana ankal...misupu kwa darasa la bule kabisa
ReplyDeleteANKAL NA MM NAKUPA KAZI NYINGINE KUANZIA LEO
1 kuhusu kamara yako mm naita kamera ya ukombozi
2 ufanye safari ya kila mkoa na ukifika ingia vijijini
3 piga picha shule zote ili tubaini matatizo ya hizo shule kama vile madawati ubora wa hizo shule
4 piga picha hospitali na zahanati zote ili tubaini matatizo yote.
5 ninapo sema vijijini nina maana kuanzia kijiji kata tarafa na wilaya nzima.
6 baada ya kumaliza huko tutaingia kwenye miji na kimkoa kwa ujumla
7 hii kazi nakupa ww ankal na team yako nzima ya blog ya ukombozi na mkimaliza kazi ya kupiga picha hizo shule au hospitali mtuwekee hapahapa ili tuzione kisha ss wadau tutoe michango yetu ya mawazo kwa viongozi wote wa mkoa husika
8 juzi juzi tu nimesikia shule iko ndani ya mkoa wa DAR tena manzese lakini haina madawati sasa huku ni kutaniana yani haingii akilini kabisa.
9 ndio maana nataka tulifanye kama janga la kimkoa na kitaifa kwa ujumla.
10 nakuaminia ANKAL pamoja na team yako nzima
nawatakia kazi njema
ni mm mkeleketwa wa maendeleo. naitwa MZAZI nipo uk leicester....ankal kabla ya kuifanya hii kazi nakuomba uitoe hii mada kwa wadau tuone kama wataikubali au la...aksanteni sana na mungu akupeni maisha marefu.
Ndio mzee Muhidin issa Michuzi nakumbukuka ulitupiga picha moja zamani Gerezani Kids miaka ya 80's na kocha wetu alikuwa Hemedii Kionzo plz kama utakuwa unayo kwenye kumbukumbu zako tuwekee on ur blog or Gerezani facebooker group, mwananchi mkereketwa Gerezani damu
ReplyDelete