Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika makabidhiano hayo. Kutoka kushoto ni Bibi Magdalena Rweyemamu, Bw. Francis Kitauli, Bw. Edwin Rweyemamu anayeteta jambo na Bw. Ludovick Utouh, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Bw. Salhina Mkumba na Bw. Athanas Pius.
=====
Na Mwandishi Maalum
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekabidhiwa rasmi Ujumbe wa Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa ( UNBOA)
Makabidhiano hayo yamefanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa mkutano wa 66 wa Bodi ya Wakaguzi ya UM.
Katika hafla hiyo Afrika ya Kusini ndiyo iliyoikabidhi Tanzania kijiti hicho. Makabidhiano ambayo yalishuhudiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Ombeni Sefue ambaye ameiwakilisha Serikali katika makabidhiano hayo.
Afrika ya Kusini imekuwa mjumbe wa Bodi kwa miaka 12 na Tanzania itamaliza ngwe yake mwaka 2018
Aidha hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Bi Suzan Malcora ambaye ni Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (Chief de Cabinet). Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki Moon.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyowashirikisha pia wajumbe wengine wa bodi ambao ni Bw. Dong Dasheng akimwakilishi Mkaguzi Mkuu kutoka Uchina na Bw. Amyas Morse Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka Uingereza. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu , Bw. Ludovick Utouh amewahakikisha wajumbe wenzie pamoja na sekretariati ya Umoja wa Mataifa kwamba Ofisi yake imejipanga vema kulibeba jukumu hilo.
“ Hafla hii ya leo inahitimisha rasmi mchakato mrefu wa makabidhiano ya jukumu hili, mchakato ulioanza tangu uteuzi wangu ulipofanyika mwezi Novemba mwaka jana. Ni mchakato unaofungua ukurasa wa kubadilishana mawazo, uzoefu na utaalamu. Kwa niaba ya Nchi yangu, Ofisi yangu na mimi mwenyewe binafsi naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa wajumbe wa Bodi ya UM na Kamati ya Operesheni za Ukaguzi” akasema Bw. Otouh.
Akabainisha kwamba Tanzania inachukua jukumu hilo la kuwa mjumbe wa UNBOA katika kipindi muhimu, kipindi ambacho UM unapita katika mageuzi makubwa ya kubadili mifumo yake ya kiutendaji ikiwamo kutoka utumiaji wa mfumo ujulikanao kama UNSAS kwenda mfumo wa IPSAS.
“ Tunaingia katika bodi hii katika kipindi ambacho UM inapitia mageuzi makubwa yakiwamo yale ya kutoka ukaguzi uliokuwa ukifanyika kila baada ya miaka miwili na kuingia katika ukaguzi wa kila mwaka”. Akasisitiza Otuoh
Na kuongeza. “ Matokeo ya mageuzi haya maana yake ni kuongezeka kwa ukubwa wa kazi kwa upande wa wakaguzi, ogezeko ambalo litatupasa si tu kufanya kazi kwa umakini mkubwa lakini pia kutekeleza majukumu mengi na katika muda mfupi”.
Na kwa sababu hiyo, akasema, kwa kutambua uzito na unyeti wa kazi kubwa iliyombele, ndiyo maana baada ya kuteuliwa kwake yeye na maafisa wake walianza jukumu la kujianda kwa kila hali ili waweze kulitekeleza jukumu hilo kwa ukamilifu na weledi mkubwa.
Akatumia fursa hiyo kuishukuru Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Afrika ya Kusini kwa namna ambavyo imetoa ushiriano mkubwa na wa karibu sana, kuanzia siku ile Ofisi ya NAOT ilipopitishwa kwa kauli moja na Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa kushika wadhifa huo.
Aidha akasema ingawa Afrika ya Kusini imemaliza ujumbe wake, Tanzania itaendelea kushirikiana nayo kwa karibu hasa kwa kuzingatia kwamba kukabidhiwa kwa jukumu hilo hakuhitimishi mchakato mzima wa kuendelea kubadilishana uzoefu na utaalamu.
Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza kwa niaba ya serikali, pamoja na kuwashukuru wajumbe wa bodi ya UNBOA na sekretarieti yake. Amesema Serikali inauchukulia ujumbe huo kwa uzito wa aina yake.
“Nimefurahi sana kuwapo hapa na kuiwakilisha serikali, ninapenda ninawakikishie kwamba, serikali yangu inalipa jambo hilo uzito wa kipekee sana. Heshima na mchango wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa unafamika na sasa tunapoingia katika jukumu hili ni dhahiri kwamba tunataka kufanya kazi nzuri hata katika maeneo mengine na uwezo huo tunao” akasisitiza.
Naye Naibu Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu kutoka Afrika ya Kusini Bw. Thembekile Makwetu akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, amemhakikisha Bw. Utouh na ofisi yake ushirikiano wa karibu na usiotereka. Huku wajumbe wengine wa Bodi nao wakielezea kutoa ushirikiano kwa Tanzani na kuikaribisha kwa moyo mkunjufu.
Kwa upande wake, Bi Susan Malcora akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, yeye amesema anaikaribisha Tanzania katika ujumbe wa bodi hiyo kwa mikono miwili na kusisitiza kwamba ujumbe wa Tanzania katika Bodi hiyo utasaidi sana katika kusukuma mbele ajenda ya uwajibikaji na udhibiti wa fedha na mali zinazomilikiwa na Umoja wa Mataifa.
Akasema Umoja wa Mataifa, unatambua umuhimu na mchango mkubwa wa Bodi hiyo na kuongeza kwamba itafanya kazi kwa karibu wa wajumbe wa bodi ili kuhakikisha kwamba mageuzi yanayoendelea hivi sasa ndani ya UM yanafanyika kwa ukamilifu na kwamba watazingatia ushauri na maelekezo watakayopewa na Bodi.


UN wanatuchukulia Mzee Ludovick Utouh sasa Mafisadi wetu hapa Tanzania watakaguliwa mahesabu ya kifedha na kulipuliwa na nani?
ReplyDeleteHabari hii poa sana na nampongeza sana mh. Ludovick Utouh kwa ufanisi wake.Ila swali langu gazeti la leo la mwananchi limeorodhesha majina ya vigogo waliopatiwa viwanja wilaya ya Ilala /Dar na jina lake likiwamo,pia wabunge kibao na majina ya vigogo wengine na ndugu zao.Je mh. Utouh umepita huko wilayani.Je wananchi wa kawaida waliotoa shs30,000 na kunyimwa viwanja hii imekaaje?Je walal hoi na mwananchi wa kawaida tuende wapi ili tupate haki yetú ,kama ofisi zote bila ya kuwa na jina na fedha ,hupati huduma yoyote.Bro michuzi naomba unirushie hii comment hewani.Big up mdau ughaibuni ,big Joe
ReplyDeleteBwana Utouh, Kazi nzuri uliyoanza huku hujamaliza. Hongera lakini Tz tunakuhitaji zaidi kutokana na MABAKA UCHUMI kuzidi hasa kwa mrengo wa rasilimali ya Gesi na Petroli.
ReplyDeleteNadhani umepatiwa kazi ya UN Kimkakati upishe MIBAKA ipite. Nakuombea Mungu urudi mapema kuimarisha yale mazuri uliyo anza kwa sababu huku yatanyambuliwa.
Uto awepo asiwepo, kuibiwa mtaibiwa tu.
ReplyDelete