Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara ya waziri wa maji Prof. Jumanne Maghembe mkoani humo. kushoto ni katibu tawala wa mkoa Alhaj Salum Chima.
waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe akihutubia wakati akijumuisha ziara yake mkoani Rukwa.
ma-DC wa Rukwa, Methew Sodoyeka wa Sumbawanga, Kulia, Moshi Chang'a wa Kalambo, na yule wa Nkasi wakifuatilia hotuba ya waziri Prof. Maghembe.
NA RAMADHANI JUMA,AFISA HABARI-SUMBAWANGA
MKUU wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya ameiomba serikali kuupatia kipaumbele maalum mkoa huo katika miradi ya maji kutokana na kukabiliwa na upungufu wa muda mrefu wa huduma hiyo.
Alitoa ombi hilo kwa waziri wa Maji Mh. Profesa Jumanne Maghembe wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya waziri huyo mkoa humo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Alisema kuwa, licha ya tatizo hilo kuwa kubwa na la muda mrefu, huenda upungufu huo wa huduma ya maji safi ukaongezeka mara dufu mara baada ya ujenzi wa barabara zinazounganisha mkoa huo na ule wa Mbeya na Katavi kukamilika kwa kiwango cha lami, hali itakayosababisha idadi ya watu kuongezeka kutoakana na shughuli za kiuchumi kushamiri.
Manyanya alipendekeza serikali kutekeleza miradi midogomidogo ya maji ya visima mkoani humo ili kuwaharakishia wakazi wake huduma hiyo muhimu.
Kwa upande wake, waziri Profesa Maghembe iliahidi kuwa, serikali itatekeleza miradi ya maji katika vijiji 10 vya kila wilaya ya Mkoa huo ambazo ni Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.
Alisema kuwa, utekelezaji wa mpango huo utaanza na vijiji vitatu katika kila wilaya na tayari shilingi bilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili awamu ya kwanza kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji ya Laela, Matai na kijiji cha Nankanga.
Waziri Maghembe pia aliitaka Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga inayohudumia wilaya mbili za Sumbawanga na Kalambo kwa sasa, kupendekeza kijiji kimoja cha Sumbawanga Vijijini ili kiungane na kijiji cha Ulumi ambacho alikipendekeza Waziri mwenyewe na kuwa vijiji viwili ambavyo vitaongezwa katika awamu hiyo ya kwanza ya kupatiwa maji.
Alishauri pia barabara ya Namanyere kuelekea ziwa Tanganyika kupandishwa daraja na kuwa ya Mkoa, ambapo ikikarabariwa itasadia katika kuhakikisha mazao ya ziwani yanauzwa upande wa Tanzania, kuliko ilivyo sasa ambapo samaki wengi wanasafirishwa katika jirani ya Congo.
Kwa upande wa utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya maji, Profesa Maghembe alishauri wakulima wapatiwe pampu ndogondogo kupitia miradi ya Kilimo ili waweze kuvuta maji kutoka katika vyanzo kama mito badala ya kulima katika vyanzo hivyo.
Alizitaka Halmashauri za Mkoa wa Rukwa kubaini na kuorodhesha vyanzo vyote vya maji vilivyopo katika maeneo yao na kuvifikisha wizarani kabla ya mwezi Septemba mwaka huu, ili vichapishwe katika gazeti la serikali na kuwekewa utaratibu wa kivilinda.
Aliwashauri viongozi wote wa Mkoa wa Rukwa kwa pamoja kuanzisha programu maalumu za upandaji wa miti ili kutunza mazingira, vinginevyo baada ya miaka 10 vyanzo vingi vya maji vitapotea na kubaki historia hali ambayo itatishia uhai wa wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...