Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya jana, Jumanne, Julai 24, 2012, alipokea kwa mshtuko mkubwa, masikitiko na huzuni nyingi taarifa ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mheshimiwa John Evans Atta Mills, kilichotokea mchana wa jana.
Kufuatia taarifa hizo, Mheshimiwa Rais Kikwete, kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, Serikali yake na kwa niaba yake mwenyewe amemtumia salamu za rambirambi Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa John Dramani Mahama.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Mheshimiwa Mahama, Rais Kikwete amesema: “Tanzania imepokea kwa mshtuko mkubwa, masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mheshimiwa John Evans Atta Mills, kilichotokea mchana wa leo (jana)”.
“Kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, Serikali yangu na mimi mwenyewe, natuma salamu za rambirambi kwako na kupitia kwako kwa wananchi na familia ya marehemu. Tuko pamoja nanyi katika kipindi hiki cha majonzi kwani ni msiba wetu sote.
Mimi na Tanzania tumepoteza rafiki mkubwa na Afrika imepoteza kiongozi wa kutumainiwa. Daima tutamkumbuka Rais John Evans Atta Mills kwa msimamo wake thabiti wa kutetea maslahi ya Afrika na watu wake. Hakika tutaukosa mchango wake uliojaa busara na hoja zenye kina, mantiki na ushawishi mkubwa.
Rais Kikwete alimaliza kwa kusema: “Tunaungana nanyi katika wakati huu mgumu wa majonzi kumwomba Mwenyezi Mungu, awape nguvu, moyo wa subira na baraka zake ili muweze kuhimili kipindi hiki cha majonzi. Aidha, tunaungana nanyi kumuomba Mola ampe mapumziko mema marehemu Rais Profesa John Evans Atta Mills. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...