Tarehe 25 Juni 2012 huko Geneva Dkt. Agnes L. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (Permanent Representative of Tanzania with WMO) alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu (Executive Council) ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization - WMO).
Uchaguzi huu umefanyika kwenye kikao kinachoendelea hivi sasa cha sitini na nne cha kamati hiyo kuu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani. Nafasi ambayo Dkt. Kijazi amechaguliwa kuijaza imeachwa wazi na Sudani na Dkt. Kijazi atakuwa mjumbe mpaka mwaka 2015 wakati uchaguzi utakapofanyika tena.
Kati ya nchi 189 ambazo ni wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani ni nchi 37 tu ambazo zina wajumbe katika kamati hiyo kuu.
Hii ni nafasi muhimu na adhimu kwa nchi yetu kwani italeta manufaa na misaada kwenye sekta ya hali ya hewa nchini na pia kuitangaza nchi yetu Kimataifa.
Dkt. Kijazi ana ujuzi wa kutosha katika masuala ya hali ya hewa kwani baada ya kumaliza kidato cha sita alisoma fani hiyo kuanzia ngazi ya cheti, diploma, shahada ya kwanza (BSc), shahada ya pili (MSc) na shahada ya tatu (PhD).
Aidha Dkt. Kijazi ni mwanamke wa kwanza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa hapa nchini na pia ni mwanamke wa kwanza katika kanda hii ya Afrika Mashariki kuwa na wadhifa huu na kuchaguliwa kwenye nafasi hii ya kimataifa.
Kwa kupata nafasi hii Tanzania na hasa Mamlaka ya Hali ya Hewa itafaidika kwa misaada itakayoiwezesha kuongeza uwezo wake hasa mitambo, vifaa na mafunzo. Taarifa za kuchaguliwa kwa Dkt Kijazi katika nafasi hii zilitufikia wakati Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (MAB) ikiwa inaendelea na kikao chake cha 29 kilichofanyika mjini Morogoro.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bwana Morrisson Mlaki alimpongeza Dkt. Kijazi na kusema kuchaguliwa kwake kunaonyesha kazi nzuri ambayo Mamlaka ya Hali ya Hewa inafanya katika kutekeleza majukumu ya kuiwakilisha nchi kimataifa katika masuala ya hali ya hewa.
Kwa mara ya mwisho Tanzania ilikuwa na nafasi hii kuanzia mwaka 1995 hadi 2007 ilipokuwa imeshikwa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Mohamed S. Mhita na ambaye pia alikuwa Rais wa Shirika hilo katika kanda ya Afrika. Tunampongeza Dr. Kijazi na kumtakia mafanikio katika kutekeleza majukumu hayo ya kimataifa.
Imetolewa na Monica Mutoni; Afisa habari Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Nilipoanza kusoma habari hii nilijua fika kuwa lazima neno "msaada" litakuwepo!
ReplyDeleteMtanzania akishika nafasi fulani katika kiwango cha kimataifa cha kwanza ni kusaka misaada. Kasumba chafu sana hii.
Achia hapo tu. Waziri toka eneo fulani iwe kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi kanda atafanya juu chini kupendelea kwake. Ndiyo maana hamana usawa katika kugawa raslimali za nchi. Wizi mtupu.
Watanzania wenzangu tubadilike. Misaada inatuponza na kuendelea kunyonywa!