Wakati Hospitali ya Igogwe baadae leo itakaribisha wageni kwenye chakula cha hisani kuichangia hospitali hiyo kwa shughuli za kuiendeleza hospitali na kusheherekea Jubilei yake ya dhahabu (miaka 50 ya kuasisiwa), Malenga wa Rungwe Daudi Lugano Kilindu amejitosa uwanjani kuhimiza uchangiaji huu kwa shairi maalum liitwalo Wapendwa Tusonge Mbele.
Shairi hilo litaimbwa kwenye chakula hicho cha hisani leo hii pamoja na shairi lingine refu zaidi, la beti 13, lililotungwa kwa kugha ya Kiswahili na beti tatu za mwisho zikiwa za Kiingereza.
Wadau  wa Michuzi Blog wanakaribishwa kulisoma na kuitikia ujumbe wa Wapendwa Tusonge Mbele. Akaunti maalum za Hospitali ya Igogwe kwa ajili ya michango ya Jubilei ni:

1.   Aliyeshika maisha, ndiye Mungu wa mbinguni,
Aliyetukutanisha tuliopo kanisani,
Leo atatuwezesha  tuchangie mapauni,
Wapendwa tusonge mbele, tung’ang’anie kutoa.

2.   Nianze na wale pale walengwa nambari wani,
Katua na timu ile kututia kampani,
Pole na safari pole, ni Igogwe karibuni,
Wapendwa tusonge mbele, tung’ang’anie kutoa.

3.   Hongera ziwashukie, mwaliko kuitikia,
Twaomba tusaidie, kwa mawazo na rupia,
‘Sipitali tuchangie, malengo kuyafikia,
Wapendwa tusonge mbele, tung’ang’anie kutoa.

4.   Ona mnavyopendeza, mavazi yamelemeta,
Sura zenu zaangaza, kwa lishe mmetakata,
Bila shaka mmejaza, mfukoni zinaita,
Wapendwa tusonge mbele, tung’ang’anie kutoa.

5.   Ni vyema tukitambua, kutoa si utajiri,
Yataka kua na nia na moyo wa ujasiri,
Tung’ang’anie kutoa, nawapeni hiyo siri,
Wapendwa tusonge mbele, tung’ang’anie kutoa.

6.   Sisi ndiyo wafadhili, kamwe tusijilegeze,
Tujitoe kila hali, shetani asitupumbaze,
Ulaya wako chakari, nao tusiwaumize,
Wapendwa tusonge mbele, tung’ang’anie kutoa.

7.   Tunavyo vingi jamani, ng’ombe, mbuzi na mikeka,
Miti, chai, kuku, kuni, mashamba vyatuzunguka,
Miwa, ndizi na majani, watoto wamefurika,
Wapendwa tusonge mbele, tung’ang’anie kutoa.

8.   Usiseme ni kidogo, wenzangu watanicheka,
Usitoe kwa kinyongo, bali moyo kupondeka,
Ikamilike mipango, tutoe bila kuchoka,
Wapendwa tusonge mbele, tung’ang’anie kutoa.
                              
©Daudi Lugano Kilindu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Asante kubwa Daudi wewe una meremeta.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...