Profesa Alexander Nyangero Songorwa (pichani kulia) ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori (Wildlife Division ) kuziba nafasi iliyokuwa wazi.
Kabla ya kuteuliwa Profesa Nyangoro alikuwa Profesa Mshiriki katika Usimamizi wa Wanyamapori, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro. Pia ndiye aliyekuwa  Mkuu wa Idara hiyo ya Usimamizi wa Wanyamapori SUA.
Wakati huohuo, Profesa Jafari Ramadhani Kidegheshon (chini) ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi, kuiongoza Sehemu ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori (Sustainable Utilisation of Wildlife Section). Kabla ya uteuzi huo Profesa Ramadhani alikuwa Profesa Mshiriki katika Usimamizi wa Wanyamapori katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro.
Uteuzi huo umetekelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna Tarishi kwa mamlaka aliyo nayo kwa mujibu wa  kifungu cha 6 (1) (b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002. Utekelezaji wa uteuzi huo ni kuanzia tarehe 24 Septemba 2012.

Mkurugenzi mpya wa wanyamapori, Profesa. Songorwa, ni msomi katika fani ya Wanyamapori. Anayo shahada ya kwanza (B.Sc.) ya Sayansi katika Zoolojia na Ekolojia ya Wanyamapori ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (mwaka 1987), Shahada ya uzamili (MSc) katika Mipango na Maendeleo Vijijini ya Chuo Kikuu cha Guelph, Ontario, Canada (1994) na shahada ya uzamivu (PhD) katika Uhifadhi Maliasili ya Chuo Kikuu cha Lincoln, New Zealand (1999).
Kabla ya kujiunga na SUA mwaka 2001, Prof. Songorwa alikuwa mwajiriwa wa Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzia mwaka 1982.
Akiwa Wizarani Profesa Songorwa alihudumu katka nafasi mbali mbali zikiwemo Askari Wanyamapori, Mkuu wa Kanda na Msaidizi wa Mkuu wa Mradi katika Pori la Akiba la Selous. Pia alihudumu kama Afisa Mwandamizi katika Mradi wa Uhifadhi Shirikishi wa Wanyamapori, Makao Makuu, Dar es salaam.
Naye Profesa Kideghesho siyo mgeni katika Idara ya Wanyamapori. Kabla ya kujiunga na na SUA mwaka 1999 Prof. Kideghesho alikuwa mwalimu katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka (CAWM-Mweka), Moshi kuanzia 1993.
Kitaaluma Prof. Kideghesho ana shahada ya kwaza (B.Sc.) katika Kilimo ya SUA (1993), Shahada ya Uzamili (MSc) katika Biolojia ya Uhifadhi ya Chuo Kikuu cha Kent, Uingereza (1996), na Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Norway kilichopo mjini Trondheim (2006). 

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

                                     22 Oktoba 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Hongera na Pole Mkurugenzi kazi mbele yako ni kubwa sana hasa ongezeko la vitendo vya ujangili hasa wa tembo, twiga na pundamilia. Watumishi wamekosa motisha, kwahiyo kazi kwako kuwapa ari na nguvu na waweze kujiamin ili wakusaidie vizuri. MaProfessor misisamo yenu thabiti mukiwa SUA tunaifahamu tunaamini ubabaishaji Wildlife Division sasa basi

    ReplyDelete
  2. Hongereni sana walimu wangu. Nimefurahi kuteuliwa kwenu kwani wote mna uzoefu na idara ya wanyapori na maliasili kwa ujumla. Tuko pamoja nanyi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...