25 SERENGETI BOYS WAINGIA KAMBINI
Kikosi cha wachezaji 25 wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kimeingia kambini leo (Oktoba 21 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya raundi ya mwisho ya michuano ya Afrika kwa vijana.
 
Serengeti Boys ambayo iko chini ya Kocha Jakob Michelsen itacheza mechi hiyo ya raundi ya tatu na mshindi kati ya Congo Brazzaville na Zimbabwe ambapo tayari Congo Brazzaville imefanikiwa kupata ushindi wa ugenini wa mabao 2-1. Mechi ya marudiano itachezwa jijini Brazzaville kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.
 
Katika mechi hiyo ya raundi ya tatu, Serengeti Boys itaanzia nyumbani katika mchezo utakaofanyika Novemba 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, wakati mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye.
 
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liko katika mikakati ya kuhakikisha Serengeti Boys inapata mechi mbili za kirafiki za kimataifa kabla ya kumvaa mshindi kati ya Congo Brazzaville na Zimbabwe. Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika Machi mwakani nchini Morocco.
 
KAMATI YA LIGI YAIONYA AFRICAN LYON
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeipa onyo kali timu ya African Lyon kutokana na washabiki wake kuweka bango lililoandikwa ‘We believe in 0777’ kwenye mechi yake dhidi ya Azam iliyochezwa Oktoba 6 mwaka huu Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
 
Bango hilo ambalo si la mdhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom halitakiwi kuonekana tena kwenye mechi ambazo African Lyon inacheza vinginevyo Kamati ya Ligi itachukua hatua kali dhidi ya timu hiyo.
 
Kamati ya Ligi imezikumbusha timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kuzingatia kanuni zinazotawala ligi hiyo ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi.
 
PAMBANO LA YANGA, RUVU SHOOTING LAINGIZA MIL 47/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Ruvu Shooting lililochezwa jana (Oktoba 20 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa wenyeji Yanga kushinda mabao 3-2 limeingiza sh. 47,615,000.
 
Watazamaji 8,233 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000, na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 8,420,578.47 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 7,263,305.08.
 
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 203,000, waamuzi sh. 381,000, mwamuzi wa akiba sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.
 
Umeme sh. 300,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 3,500,000 wakati tiketi ni sh. 2,959,100. Gharama za mchezo sh. 2,806,859.49, uwanja sh. 2,806,859.49, Kamati ya Ligi sh. 2,806,859.49, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,684,115.69 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,122,743.80.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Million 8.4 za kitanzania ni 3000 british pounds, huu ni mshahara wa wiki wa mchezaji wa daraja la tatu la Uingereza, bongo ndio mgao wa timu nzima ya ligi kuu, duuuh kweli bongo tambarare. Ndio mnataka turudi huko wakati huku nje kuna opportunities for our kids kuliko hiyo nchi ya mafisadi, wanaocheza wanapata pesa ndogo waliokaa ofisini ndio wanakula panga.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...