Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameambiwa juzi, Jumatano, Desemba 5, 2012, kuwa ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam-Lindi utakamilika katika miezi sita ijayo kuanzia sasa.
                    Rais Kikwete alipewa maelezo hayo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Mhandisi Gerson Hosea Malangalila Lwenge wakati aliposimama kukagua maendeleo ya ujenzi kwa akiwango cha lami wa kilomita 56 kati ya  Nyamwage, Mkoa wa Pwani na Somanga, Mkoa wa Lindi.
                    Rais Kikwete alisimama kukagua ujenzi wa Barabara hiyo wakati akirejea Dar es Salaam kutoka Lindi ambako alifanya ziara yenye mafanikio makubwa ya siku tatu kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi.
                    Akipewa maelezo ya ujenzi wa Barabara hiyo kwenye eneo la Somanga, Rais Kikwete aliambiwa kuwa kati ya kilomita hizo 56 tayari kilomita 30 zimeshatiwa lami. Barabara hiyo inajengwa na Kampuni ya MS Karafi.
                    Naibu Waziri huyo alimwambia Rais Kikwete: “Mjenzi anajenga kiasi cha mita 250 kila siku na kama hapakuwepo na kuharibika kwa lolote ama mvua isipokuwa nyingi kupita kiasi, basi ujenzi wa Barabara hii utakuwa umekamilika katika miezi sita ijayo kuanzia sasa.”
                    Naibu Waziri alimwambia Rais Kikwete kuwa ni kweli ulikuwepo ucheleweshaji kwa upande wa mjenzi, lakini sasa maendeleo ni mazuri. Barabara hiyo ilipangwa kukamilika Juni, mwaka jana, 2011.
                    “Kwa jumla ujenzi wa Barabara nzima umekamilika kwa asilimia 78, njia ya awali ambako lami itawekwa imekamilika kwa asilimia 98, madaraja madogo kiasi cha 55 tayari yamejengwa na vifaa vyote ikiwa ni pamoja na kokoto viko kwenye eneo la ujenzi.”
                    Barabara ya Dar es Salaam-Lindi ina urefu wa jumla ya kilomita 452 na kukamilika kwa kipande cha Nyamwage-Somanga una maana kuwa mtu yoyote anaweza kusafiri kwa lami tupu kutoka Mtwara hadi Kagera ama Mwanza ama Arusha ama Tunduma.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
07 Desemba, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. wakati umefika sasa hichi kipande kiishe, miaka nenda rudi mnatuambia kitaisha kitaisha. june 20013 ikifika mtatuambia june 2014 aaargh...inakera sana, wakati wa masika hapo tunalala sana.

    ReplyDelete
  2. ktk aya ya mwisho imesomeka kuwa ".....mtu yoyote anaweza kusafiri kwa lami tupu......."

    mimi ningependa isomeke angalau ....."mtu yeyote anaweza kusafiri kupitia barabara ya lami tupu......."

    jamani tujitahidi kutumia kiswahili chetu vizuri..Tanzania inasemekana ndio mwasisi wa kiswahili na mimi nakubaliana na hilo hivyo tuwe mfano kweli hususan kwa idara nyeti kama KURUGENZI YA MAWASILIANO IKULU

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...