Mwamgongo naingia, kwa beti chache si mia,
Jijini nimeingia, na kuiona kadhia,
Wambagala wanalia, usiku ukiwadia,
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.
Ni mbali sana Mbagala, au bongo zimelala?
Utingo wa dala dala, vipi awachune hela!;
Hamyaoni madhila, au ndio zenu mila?
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.
Wananchi wa jijini, nilidhani ni wajanja,
Wakuleta ukinzani, bei hizi kuzivunja,
Heri hata wa Kusini, ukimya wameuvunja;
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.
Ukenda Kariakoo, mida ile jioni;
Waweza kita kilio; kwa shida za magarini;
Watu washikana koo; kupanda kwa ushindani;
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.
Wadhibiti wa nauli, hivi nanyi hamjali?
Vijipesa vya ugali, vyote vifanywe nauli!;
Hii mbona ni kejeli; au hamna misuli?
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.
Ninakuomba Michuzi; uzitoe beti hizi;
Watu wafanyiwa wizi, tena kiuwazi wazi;
Dola fanyieni kazi, haya majitu majizi.
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.
Hapa ninamalizia, msije mkasinzia;
Wamagari 'mesikia; bei ziwe asilia;
Kususa nayo ni njia; Wambagala nawambia;
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.
Mwamgongo;(Bw)
Mwenyeji wa Tanga (safarini Dar)
13 Januari 2013


Nyumbani ni nyumbani.Asante waTanzania kwa mapenzi na kuendelea kuni kumbusha nimetoka wapi. Shukurani wote kwa zawadi- Kahawa na Chai kutoka Bukoba, Kilimanjaro, Z'bar.Khanga zenye maneno ya kunipa moyo,spices,udi na dry fruits kutoka Dar,Tanga na Z.bar.Leo nina pokea zawadi kwa Mwamgongo ana nikubusha utamduni wetu.Maisha sita sahau.Asante WaTanzania.
ReplyDeleteMeseji nzuri wasomaji hapa globuni tumeilewa sasa kazi ipo kwa watendaji kwanza kuielewa kisha kuifanyia kazi.
ReplyDeleteBongo Tambarale,
ReplyDeleteSumatra ipo hai mchana ikifika usiku kila Afisa kama hajafika nyumbani akiwa na familia yake atakuwa yupo Baa ya karibu na kwake akipata moja mbili!