Mwamgongo naingia, kwa beti chache si mia,
Jijini nimeingia, na kuiona kadhia,
Wambagala wanalia, usiku ukiwadia,
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.

Ni mbali sana Mbagala, au bongo zimelala?
Utingo wa dala dala, vipi awachune hela!;
Hamyaoni madhila, au ndio zenu mila?
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.

Wananchi wa jijini, nilidhani ni wajanja,
Wakuleta ukinzani, bei hizi kuzivunja,
Heri hata wa Kusini, ukimya wameuvunja;
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.

Ukenda Kariakoo, mida ile jioni;
Waweza kita kilio; kwa shida za magarini;
Watu washikana koo; kupanda kwa ushindani;
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.

Wadhibiti wa nauli, hivi nanyi hamjali?
Vijipesa vya ugali, vyote vifanywe nauli!;
Hii mbona ni kejeli; au hamna misuli?
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.

Ninakuomba Michuzi; uzitoe beti hizi;
Watu wafanyiwa wizi, tena kiuwazi wazi;
Dola fanyieni kazi, haya majitu majizi.
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.

Hapa ninamalizia, msije mkasinzia;
Wamagari 'mesikia; bei ziwe asilia;
Kususa nayo ni njia; Wambagala nawambia;
Nauli ya 'buku' moja kwa Mbagala si sawia.

Mwamgongo;(Bw)
Mwenyeji wa Tanga (safarini Dar)
13 Januari 2013

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Nyumbani ni nyumbani.Asante waTanzania kwa mapenzi na kuendelea kuni kumbusha nimetoka wapi. Shukurani wote kwa zawadi- Kahawa na Chai kutoka Bukoba, Kilimanjaro, Z'bar.Khanga zenye maneno ya kunipa moyo,spices,udi na dry fruits kutoka Dar,Tanga na Z.bar.Leo nina pokea zawadi kwa Mwamgongo ana nikubusha utamduni wetu.Maisha sita sahau.Asante WaTanzania.

    ReplyDelete
  2. Meseji nzuri wasomaji hapa globuni tumeilewa sasa kazi ipo kwa watendaji kwanza kuielewa kisha kuifanyia kazi.

    ReplyDelete
  3. Bongo Tambarale,

    Sumatra ipo hai mchana ikifika usiku kila Afisa kama hajafika nyumbani akiwa na familia yake atakuwa yupo Baa ya karibu na kwake akipata moja mbili!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...