Na Mwandishi Maalum Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba ( Mb) amesisitiza kwamba, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua wazi kwamba unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba vitendo hivyo vina madhara makubwa. 
Kwa kulitambua hilo, Waziri anasema serikali zote mbili ile ya Tanzania Bara na Visiwani, zimekuwa zikichukua hatua pamoja na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba unyanyasaji dhidi ya kundi hilo la jamii wakiwamo watu wenye ulemavu wa ngozi ( albino) unapunguzwa na hatimaye kutokomezwa. 
Waziri ameyasema hayo jana alhamisi, wakati alipokuwa akitoa mchango wake wakati wa majadiliano yaliyohusu ajenda ya utokomezaji na upunguzaji unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike. 
Mhe.Sophia Simba anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 57 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanawake ( CSW), ambao umeanza siku ya jumatatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York , Marekani. Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na tatizo la unyanyasaji kuainishwa katika Mpango wa Kitaifa wa Kupunguza Umaskini ambapo vitendo hivyo vinaelezwa kama kiashiria cha umaskini. 
Aidha akaeleza pia kwamba mipango mbalimbali ya utekelezaji katika ngazi ya kitaifa na kwa kushirikiana na sekta mtambuka imeundwa kwa pande zote mbili za Muungano. Vile vile akabainisha kwamba, taasisi za kisheria kama vile Chama cha Majaji wanawake, zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika kuwasaidia wanawake fursa ya kupata haki. 
Kama hiyo haitoshi, Waziri Sophia Simba amesema, kwa upande wa vyombo vya ulinzi na usalama kumeanzishwa pia mtandao wa Polisi wanawake lengo likiwa ni kuwawezesha na kuwapa nyenzo za kushughulikia kikamilifu matukio ya unyanyasaji wa kijinsia. 
 Pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali na wadau wengine, Waziri Sophia Simba hakusita pia kubainisha baadhi ya changamoto zinazokwamisha juhudi hizo. Amezitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja kutokuwapo kwa takwimu za uhakika kuhusu vitendo vya unyanyasaji, takwimu ambazo zingeweza kuchangia katika uaandaaji wa sera na mipango mbalimbali yenye kulenga kusukuma maendeleo ya wanawake. 
Akataja changamoto nyingine kuwa ni ile ya kubadili mtizamo wa jamii kuhusu suala zima la unyanyasaji wa jinsia na kwamba tatizo hilo linahitaji kuendelea kufanyiwa kazi.
 Mhe. Sophia Simba ( Mb) akichangia ajenda kuhusu Utokomezaji na Umalizaji wa Unyanyasaji dhidi ya  wanawake  na watoto wa kike wakati  wa mkutano wa 57 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake (CSW). Mkutano huu wa wiki mbili unaendelea hapa Umoja  wa Mataifa na  Mhe. Simba anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aliyeketi   nyuma ya Mhe. Waziri ni Naibu Mwakilishi wa Kudumu,  Balozi Ramadhan Mwinyi
 Mhe. Sophia Simba akishiriki majadiliano ya mada iliyohusu  umuhimu wa Takwimu  katika  kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia, Waziri alikuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika mjadala huo.  mjadala  ulikuwa umeandaliwa na   UNFPA,  ikiwa ni sehemu ya  mkutano wa 57 wa  CSW,kulia kwa Waziri ni   Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa  UNFPA, Bi Anne -Brigitte Albractsen
 Makatibu Wakuu,  Kijakazi Mtengwa ( Tanzania Bara) na  Fatma Gharib Bilal ( Zanzibar ) wakifuatilia majadiliano  kuhusu  utokomezaji na umalizaji  unyanyasaji dhidi ya  wanawake na watoto wa kike.
Kutokana na wingi wa washiriki wa  majadiliano   kuhusu umuhimu wa Takwimu katika kushughulikia unyanyasaji kuwa wengi  kupitia  uwezo wa ukumbi,     baadhi ya  washiriki    walilazimika kukaa chini kama inavyoonekana katika picha

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...