RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga (pichani) amesema Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo na Baraza la Taifa la Michezo (BMT), hazina nguvu ya kusimamia uchaguzi wa shirikisho hilo.

Tenga aliyasema hayo leo mara baada ya kikao cha kamati ya utendaji na kusema kuwa tangu katiba hiyo ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2004 nguvu ya Waziri wala BMT haipo tena na kudai kuwa TFF ina nguvu kamili kama vyama vingine na kina uhuru wake kamili wa kutoa na kusimamia maamuzi yake bila ya kuingiliwa.

"Nitamtafuta Waziri ili nikutane naye na nimueleze kabisa kuwa agizo alilolitoa alitekelezeki na tutamshauri madhara ya maamuzi yake, serikali kuandika barua ni kutuingilia moja kwa moja na madhara yake ni kufungiwa, na tukishafungiwa hata wadhamini watakaa pembeni, timu zetu pia hazitacheza mpira, kuna watu nasikia wanasema bora tufungiwe, nitahakikisha kwa hali yoyote ile hatufungiwi.

"Sheria za nchi zipo, lakini ziliridhia toka mwaka 2004 kufanya shughuli zetu wenyewe bila ya kuingiliwa kwa kuzingatia objective (wajibu) zetu ambazo ni kucheza mpira, kama tutafanya kinyume na hapo kama kucheza tenesi au kuvuta bangi hapo ndio tuulizwe inakuwaje objective yenu sio hiyo.

Kauli ya Tenga imekuja wiki moja baada ya Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Fennela Mukangara kupinga katiba ya TFF kwa madai kuwa imekiuka kanuni ya za sheria ya BMT, namba 11 (1) na kutaka itumike ya mwaka 2006.

"Natoa agizo kwa wasaidizi wa msajili wa vyama vyote nchi kufuta taratibu za usajjili kwa mujibu wa sheria na kanuni za BMT, sisi hatuitambui katiba iliyotumika katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka huu na sasa badala yake tunatambua ile ya mwaka 2006, hii ni batili na imekiuka kanuni na sheria za BMT,"alikaririwa akisema Dk Mukangara wiki iliyopita.

Pia kufuatia sakata la katiba hiyo kutotambuliwa na serikali Waziri Mukangara alitangaza pia kumsimamisha kazi msajili wa vyama vya michezo nchini Mercy Rwezaura aliyedaiwa kuipitisha katiba hiyo na tayari mchakato wa kumtafuta mwingine umeanza.

Lakini Tenga alisema: 'Kifungu alichotumia Waziri kuzuia katiba mpya kanuni zake zinaendelea kuzungumzia marekebisho, hatuwezi kuchukua vipande vidogo vidogo kwa jambo kubwa kama hili, katiba tuliipeleka kwa msajili na ikakaa kwa siku 14, baada ya siku hizo kupita akatupatia katiba yetu hatukujaza fomu sasa lilikuwa jukumu la nani kutupa fomu ya kujaza si ni msajili hajatupa sisi tufanyaje?"alihoji "Waziri anaposema hatukufuata taratibu kwa vile hatukujaza fomu sio haki, ametuadhibu kwa kosa ambalo si la kwetu, tunadhani jambo hili lingeangaliwa kwa kina, hata hivyo mwaka 2004 hakukuwa hata na muda wa kuandika muktasari mabadiliko yalifanyika pale pale ukumbini na uchaguzi ukafanyika.

"Tulishaachana na mambo yetu kuingiliwa na serikali wala BMT maelekezo ya Waziri nadhani amesahau kabisa kuwa tulishatoka huko siku nyingi,ni kweli kabisa uhalali wa marekebisho ya katiba yanatokana na mkutano mkuu peke yake na si mtu mwingine yoyote na BMT wala Waziri nafasi yao haipo tena, na anavyotutuma tuandike barua FIFA tuwambie ametuamuru kufuta katiba yetu, nasema wazi hatutafanya hivyo, sana sana tutawapa maelezo na kuwambia tutakutana naye na kuyamaliza"alisisitiza

"Marekebisho ya katiba yetu hatukufanya kwa siri tuliwaeleza kabisa hatuna fedha ya kuitisha mkutano mkuu mara mbili, kama mtakumbuka marekebisho haya yalikuwa wakati tumeshaomba wadau wakachangishana fedha kwa ajili ya kuisaidia timu yetu ya Serengeti alafu wiki moja baadae wadau hao wakuone unaitisha mkutano mkuu unaogarimu milioni 135 watakuelewa?

"Kiongozi mzuri ni yule anayesema kweli hali halisi ndio hiyo tulipeleka waraka zikafanyika kampeni za kuukataa, nikawaangukia na kuwaeleza hali halisi zikapigwa kura 35 walipinga, 70 walikubali sasa kuifuta katiba ina maana watu 70 wote hawana maana? Kiongozi ambaye hawezi kufanya maamuzi magumu inatia shaka.

"Hata hiyo katiba ya mwaka 2006 anayoitaka Waziri ndio tufanyie uchaguzi haina nafasi ya BMT kusimamia uchaguzi, na kuitumia katiba hiyo ni kuiondoa mikoa mipya kama ya Simiu, Geita,Katavi, Waziri ameshauriwa kwa sababu hakuwa kwenye mpira, na wanaomshauri sidhani kama wanajua masuala ya mpira wala hawaijui katiba ya TFF inasemaje na hawajaisoma ndio maana Waziri akatoa maamuzi kama yale.

"Mama tafadhali naomba achia huu mchakato uendelee kinyume chake ni kuingiza nchi kwenye moto, kwenye vurugu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 16 mpaka sasa

  1. tengaaaaaaaaaaaaaaaaa aibuuuuuuu kwakoooo kumbe watuuu wa kubebwa ni tatizooo ndio maanaaa kenya hakuna vitu maalum wala mkuu mkoa wote ni kuchaguliwa

    ReplyDelete
  2. tenga kufungiwa isiwe sababu ya nyie kufanya vituko.kama kweli unajali soka la nchi hii basi tekelezeni maagizo ya waziri.wewe unasema kosa la msajili kutowapa fomu kwani mlikuwa hamjui taratibu zikoje?wewe mbona uko makini kuhakikisha taratibu zinafutawa iweje serikali isiwe makini?.kama hamtaki kuingiliwa na serikali basi na mabakuli yenu msipelekeke huko.kwenye hela mnataka msaada wa serikali.kwa kweli mnatuboa kila uchaguzi lazima uwe na mizengwe.kweli dunia ya leo mnaweza mkaweka mtu agombee na kivuli.kwanini hamtakai na wenzenu waongoze kuna siri gani mnayoificha.na usikimbilie kujitetea kuwa mmewaita fifa kwani wao ndio nini hata kwenye chaguzi zao nao wanafix matokeo iweje washindwe kushirikiana na nyie.

    ReplyDelete
  3. Kama Serikali haitakiwi kuingilia shughuri za TFF, mbona walikubali Serikali kumlipa mshahara kocha Max maximo kwa nn TFF isikatae kuingiliwa na serikali.?

    ReplyDelete

  4. sasa nimeamini TFF au zamani iliitwa FAT ni sehemu tamu yenye neema na utajiri, kama ilivyokuwa enzi za rafiki yangu na mzee wangu Ndolanga hakutaka kutoka hapo aliitumia FIFA kumkingia kifua na hata Rage akutaka kung'oka FAT mpaka alipelekwa rumande kwa wizi, sasa huyu mchagga ndugu yangu Tenga ndo kabisaa kaonyesha tamaa ya fisi na sasa anataka kuacha mtandao wake, anataka kuweka kijana wake, lakini kwa mwendo huu hawezi kufanikiwa maana wadau tumeshituka, wewe Tenga hakutaka kuondoka kwa heshima sasa utaondoka kwa aibu, sijui kwa nini viongozi wa KiAfrica ni waroho wa pesa na madaraka kiasi hiki? Kwenye kila jambo , vyama vya siasa ni mali ya watu fulani wakitoka madarakani wanataka waache mtandao, mpira hivyo hivyo, NGOS ni mali za watu. Sasa mimi nawakilisha wadau wa mpira Tanzania nasema TEnga ondokaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa FAT siyo mali yako na huyo kibaraka wako hatumutaki kabisaaaaaaaaaaaaaaaaaaa wizi mtupu. Mtakavyote hukosa vyote nasikia unataka kugombea CAF lakini kwa mwendo huu unaweza kujiaribia , TENGA ONDOKA MARA MOJA. HUWEZI KUDHARAU WIZARA NA BALAZA LA MICHEZO, HII NI SERIKALI SASA TENGA UNALETA MAMBO YALE YALE YA NDOLANGA NA RAGE YA KUDHARAU SERIKALI HAKUNA KITU KAMA HICHO MAANA SERIKALI NI MDAU MKUBWA NA SAUTI YA WANANCHI SASA UNALETA UMAFIA WA FIFA WAKINA SEPPA BLATTER TUNAWAJUA NA WAJUMBE KIBAO WA FIFA NI MAFISADI NA WALA RUSHWA NA WENGINE WAMEFUKUZWA KWA RUSHWA. Michuzi husinibanie nina hasira na viongozi uchwara kama Tenga, wizi mtupu ondoka haraka tuachie nchi yetu na mpira wetu.

    ReplyDelete
  5. Tenga,umevuruga TFF,umevuruga uchaguzi,unabeba lawama zote.Unatafuta Sympathy.

    Halafu timu yetu ya Taifa ya mpira wa miguu ina mchezo na Morocco ndani ya wiki 3,akili zote mmeziweka kwenye Uchaguzi

    David V

    ReplyDelete
  6. tenga umesema kweli.mi naona waziri ana ajenda ya siri na hao wanaotaka kuturudisha enzi za FAT.ni aibu kwa waziri mzimz kukurupukia maamuzi bila kufanya utafiti hata kidogo kidogo.

    ReplyDelete
  7. KICHWA CHA MWENDA WAZIMU ALLHAJI PROF DR aLI HASANI MWINYI HAKUNA HATA KOMBE LA AFRIKA- KOMBE LA DUNIA- NDOTO---WAZIRI WA UVUMBUZI TALANTA NA MICHZO 2015 Tanzania WORLD CUP URUSI 2018, KAZI NNDOLANGA TENGA TENGA NDOLANGA

    ReplyDelete
  8. TFF na Hao FIFA wote mafisadi. Mtasemaje serikari zisiingilie mambo yenu wakati mnaitegemea kufanikisha mambo yenu, Je FIFA wanaweza andaa kombe ladunia bila serikali? Je Simba na Yanga wanaweza cheza mpira bila polisi?

    FIFA yenyewe ni ufisadi mtupu, angalia kashfa ya mchakato wa kuwapata waandaaji wa kombe la dunia mwaka 2018 na 2022.

    Mbona Ulaya wanaweka sera ambazo ni lazima zifuatwe na vyama vya mipira ya miguu.

    Hivi huyu Tenga yeye anaona ni sawa Nyamlani awe mgombea pekee wa TFF kati ya Watanznia Mil 45? yeye ni nani? Mmekaa naye miaka 8 hapo nini cha maana amefanya? Si afadhali wakati wa akina Ngolanga tulikuwa ndani ya 100 bora duniani na kulikuwa na migogoro kibao na hakukuwa na mdhamini yeyote.

    Huyo Tenga ataje nchi yeyote duniani iliyoendelea kimpira bila kuishirikisha serikali. Manitaka tu wakati wa shida zenu, ikifika kwenye maslahi ya matumbo yenu mnawakataa.

    Kamwe mpira wa hapa Bongo hautakaa uendelee, maana Tenga ndio alionekana ni afadhali kuliko watu wengine kumbe naye hamna kitu, achilia mbali hili la katiba ambalo ni dogo tu, nini cha maana amefanya kwa miaka 8? misingi gani unajenga kwa miaka nane? Hizo ni propaganda tu za kushindwa kusaidia mpira wetu.

    Afadhali kuna utandawazi siku hizi, mpira wa hapa bongo wengine tuliacha kuufuatilia muda mrefu tu, mimi Simba lakini naumia zaidi Arsenal ikifungwa kuliko Simba.

    By no means we will achieve anything with the nature of leaders we have, revamp of the entire system is instantaneously obligatory and we need a small group of leaders with apparition and who can collaborate with the government to develop football from the proletariat.

    ReplyDelete
  9. Mpigeni mawe lakini Tenga hapa yupo sahihi kabisa kimaelezo kuhusu katiba. Msingi wa uendeshaji taasisi yoyte ni Katiba. Katiba ya TFF haimpi Waziri madaraka ya kuiingilia labda atumie mabavu.TFF ni taasisi inayojitegemea na siyo shirika la umma. kuipa misaada isiwe sababu ya kuiingilia kiutendaji. Taasisi nyingi tu zisizo za kiserikali zinapewa misaada au misamaha ya kodi mbona haziingiliwi kiutendaji au katiba zao?

    Kwenye hili Mheshimiwa Waziri kashauriwa vibaya, huo ndiyo ukweli. Hatua kama hizi zinaweza kuturudisha kwenye enzi za FAT ya Ndolanga, migogoro kila kukicha.

    Hivi kweli, mfano, waziri wa michezo wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani au hata Brazil anaweza kuamuru au kuingilia katiba au uendeshaji wa vyama vya mpira kwenye nchi hizo?

    Hivi, kwa mfano, waziri yoyote mhusika anaweza kuamuru au kuingilia uendeshaji wa taasisi zisizo za kiserikali, mfano za kidini?

    Uendeshaji wa vyama vya mpira duniani unafanywa chini ya Usimamizi wa FIFA sawa na ilivyo kwa mfano kanisa katoliki popote duniani linaendeshwa chini ya usimamizi wa Vatican.

    Hakuna nchi yoyote duniani iliwahi kushindana na FIFA ikashinda.Matokeo ni kufungiwa mpaka unaposalimu amri mwenyewe. hiyo ndiyo hali halisi.Tujadili kwa hoja siyo hisia.

    Ni kweli Tenga kachemsha kwenye mchakato wa uchaguzi lakini Katiba iliyopo ya TFF inapaswa iwe ndiyo msingi pekee wa utatuzi wa mgogoro wa TFF na siyo amri ya Waziri ispokuwa tu kama waziri anayao mamlaka ya kisheria ya kuamuru au kuingilia na hapa ni muhimu kujua ni vifungu gani vya sheria vinampa waziri mamlaka hayo.

    Tujadili kwa hoja na siyo kwa hisia...

    ReplyDelete
  10. Hovyooo..serikali isiwaingilie kwani huo mpira mnaocheza mnawakilisha nchi gani...Tenga ondoka huna jipya kipindi ulichokuwa madarakani hakina tofauti na kina ndolanga/rage....kichwa cha mwendawazimu kwa kwenda mbele!!!!Mekuu ondokakaga ngosha!!

    ReplyDelete
  11. Tenga haufai uongozi ulibebwa sana nasikitika kusema hivyo ila ni aibu kubwa unataka kutuletea wstanzania. Tukifungiwa na wewe utaingia ktk historia kama wale waliotusababishia soka letu kuporomoka. Tumia busara tii agizo la serikali

    ReplyDelete
  12. Bora kufungiwa! Fagio la chuma lipite na Tenga awe wa kwanza kuondoka. Ala! Anataka kuonyesha ubabe kwa serikali?

    ReplyDelete
  13. Sheria za nchi zinataka kila kikundi au taasisi nje ya serikali ili kiweze kutambulika kinatakiwa KUSAJILIWA, na katika kusajiliwa Katiba ni kitu kimoja muhimu kuwapo. Sasa Waziri ameona Katiba ya TFF ina mapungufu na anataka irekebishwe ili iweze kupata usajili halali, TFF wasipotoshe umma kuwa Waziri kawaingilia, hapana bali sheria inawataka kuwa na Katiba tena iliyopatikana kwa mujibu wa taratibu ambazo TFF haikufuata. Sasa shida iko wapi? Ikiwa taratibu hazikufuatwa basi Katiba ya 2012 ni batili. Kwa maneno mengine Waziri amekataa KUISAJILI TFF. Period .

    ReplyDelete
  14. Tenga siamini amefikia hapa! Ajabu sana!

    ReplyDelete
  15. KWA HIYO BW TENGA MKO JUU YA SRRIKALI????????/

    ReplyDelete
  16. Nakubaliana na wadau wote waliosema kwamba serikali haiwezi kuingilia mambo ya TFF, ni kweli. Lakini Tenga anajua ilo na yeye amefanya maamuzi ya kimagumashi ndiyo maana namwona yeye kama amesababisha haya makosa na kama nchi ikifungiwa basi yeye atabeba lawama. Naelewa Waziri na Tenga wote wanaelewa sheria za FIFA, kwani wote wana washauri wao wanaozijua sheria na wanawashauri ipasavyo. (Nikiwa mmoja wapo wa Wadau wapenda michezo Bongo, nasema Tenga amekua mtu mzuri kwangu)lakini kwa ili naona nakubaliana na jamaa wote kwamba Tenga ndiyo tatizo. Haiwezekani ukawa na mgombea mmoja kwenye uchaguzi haionyeshi demokrasia Inatakiwa yeye anafanya kazi pamoja na serikali kuzuia migongano kati ya serikali na TFF, kwani mchezo unaitaji support toka kwa serikali na FIFA, yaani hiyo ndiyo busara ya uongozi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...