Serikali imesema itachukua hatua kali za kisheria kwa atakayebainika kutumia vibaya simu za mikononi, na mitandao ya kijamii kuleta uchochezi au kwenda kinyume na maadili ya nchi.

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa lengo la kufanya hivyo ni kutaka kukomesha vitendo hivyo hatari vinavyoonekana kukua siku hadi siku.

“Hatua hizo zitachukuliwa dhidi ya kampuni au mtu yoyote atakayetoa kashafa na kuitukana serikali, viongozi wa serikali, dini, siasa na watu binafsi,” alisema na kuongeza kuwa vitendo hivyo vinakiuka sheria za nchi.

Alisema hatua hizo pia zitawakumba watu wote wanaojihusisha na uonyeshaji kwenye mitandao hiyo picha za ngono, unyanyasaji wa watoto na ukiukaji wa maadili na kutoa taarifa zenye lengo la kuvunja utulivu na amani.

“Matumizi mabaya haya ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kama za simu za mikononi, barua pepe, na mitandao ya kijamii yanafanywa na watu wachache kwa kusambaza taarifa zenye nia ya kuchafua taifa letu,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba teknolojia hiyo katika miaka ya karibuni imechangia kuleta maendeleo makubwa nchini, baadhi ya watu wanaitumia kwa mambo yasiyofaa.

Aliendelea kusema kuwa watu wengine wamekuwa wakiitumia kwa kufanya wizi, ujambazi,ubakaji, biashara ya madawa ya kulevya na ukahaba na kusambaza siri za watu binafsi bila idhini ya wahusika.

Alisema matumizi yasiyofaa yanafanywa na watu wachache yanaelekea kuharibu maadili ya watanzania na yanaweza kuhatarisha utulivu na usalama wa nchi kwa kutumia TEHAMA.

Aidha alisema pia hatua kali zitachukuliwa kwa wakala au kampuni ya simu yoyote itakayouza SIM kadi kwa mtu yeyote bila ya kuwa na kitambulisho kinachotambulika kisheria.

Alisema pia ni kosa la jinai kutoa taarifa za uwongo wakati wa usajili wa SIM kadi na serikali imejipanga kuzima sim kadi zote ambazo hazijasajiliwa kama inavyotakiwa kisheria.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. sheria ziwepo kwanza hatuna sheria za kutosha nchi nyingine zina sheria thabiti kama information gorvernance halafu ndo watu wabanwe.ni kweli watu wanazibukia matumizi ya technolojia bila ustaarabu kuliko hata wanaozitengeneza.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...