Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania-TRL unapenda, kupitia taarifa
hii, kukanusha taarifa zilizochapishwa katika majarida ya Kulikoni la tarehe
Aprili 26 – Mei 2 na Fahamu la tarehe 26, April, 2013 kuwa mchakato wa ununuzi
wa Vichwa 13 vya treni ulikuwa na utata.
Ukweli ni kwamba Zabuni ya ununuzi wa vichwa vya treni 13
ilitangazwa kwenye magazeti mbalimbali tarehe 9 na 10 Novemba, 2012. Kabla ya
siku ya kufungua zabuni hii ambayo ilikuwa ni tarehe 1 Februari, 2013, TRL
ilipokea barua kutoka PPRA iliyopokelewa tarehe 31 Januari, 2013 ambayo iliambatanisha
barua ya malalamiko kutoka kwa Kampuni moja ikilalamika kuwa TRL ilikuwa imekiuka
Sheria ya Manunuzi kwa kuweka vipengele kwenye zabuni ambavyo viliiengua
kampuni hiyo isiweze kushiriki kwenye zabuni.
Baada ya kupokea barua ya PPRA, TRL ilitathmini hoja ya
mlalamikaji kwa kupitia Sheria aliyoitaja pamoja na nyaraka mbalimbali
zilizokuwepo. Baada ya tathmini hii TRL ilbaini mambo yafuatayo:
a) Mlalamikaji hakuwa miongoni mwa
makampuni yaliyokuwa yamenunua nyaraka za zabuni.
b) Mlalamikaji alijikita kwenye suala la
aina tano tofauti za injini zilizopendekezwa na TRL kutumika kwenye vichwa
hivyo vya treni bila kuzingatia kuwa zabuni hii haikuwa ya ununuzi wa injini
bali vichwa vya treni. Katika zabuni hii TRL haikuweka masharti yoyote
yanayozuia kampuni yoyote duniani kutengeneza vichwa hivyo vya treni.
c) Katika barua yake ya malalamiko
alieleza kuwa kabla ya kuandika barua kwenda PPRA alikuwa ametuma barua
nyingine kwenda TRL akiomba aina ya injini inayotengezwa na kampuni
anayoiwakilisha itajwe kama moja ya injini ambazo zingeweza kufungwa kwenye
vichwa vya treni ambavyo vingenunuliwa na TRL. Hata hivyo barua aliyoitaja
haikuwa imepokelewa na TRL.
d) TRL ilijiridhisha kuwa haikuwa
imekiuka Sheria ya Manunuzi.
Baada ya tathmini hii TRL ilipeleka maelezo yake PPRA kwa
barua ya tarehe 4 Februari, 2013.
Ifahamike kwamba taratibu za Rufaa katika Sheria ya Manunuzi
ziko wazi. Kama mlalamikaji huyu angekuwa na nia ya kweli kutaka kupata haki
yake angefuata utaratibu wa Rufaa ambao umeainishwa katika Sheria hiyo hiyo ya
Manunuzi badala ya kutumia vyombo vya habari.
Uamuzi wa mlalamikaji kutofuata taratibu za kisheria na
kuamua kupeleka tuhuma kwenye vyombo vya habari unaonekana ni uamuzi wa
kupakana matope ambao hauna tija kwa mlalamikaji, TRL na jamii kwa ujumla.
Aidha tunatoa rai kwa vyombo vya habari kutokubali kuandika
habari kabla ya kuzifanyia utafiti kwani kwa kufanya hivyo jamii ya Watanzania
inapotoshwa kwa kiasi kikubwa sana.
-Mwisho-
Imetolewa na Afisi ya Uhusiano
kwa niaba ya Mkurugenzi
Mtendaji wa TRL,
Mhandisi Kipallo Aman Kisamfu
Dar es Salaam
Aprili 30, 2013
Asante kwa ufafanuzi.Lakini mbona kama hamna "CONF".Mnajitetea kwa woga woga...Lazima kuna KITU hapa
ReplyDeleteDavid V
Ulitaka iweje
ReplyDelete