JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII




UFAFANUZI WA TAARIFA MBALIMBALI ZILIZOTOLEWA KWENYE VYOMBO VYA HABARI DHIDI YA DAWA BANDIA YA KUPUNGUZA MAKALI YA UKIMWI YENYE JINA LA BIASHARA TT-VIR 30 TOLEO NAMBA 0C.01.85.
Tarehe 9 Mei, 2013, Mhe. Dkt. Hussein A. Mwinyi (Mb) Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, katika kuhitimisha hoja ya bajeti ya Wizara alitolea ufafanuzi suala la dawa bandia ya ARV kufuatia hoja zilizokuwa zimetolewa na Mhe. Zarina S. Madabida (Mb) kuhusu kuhusika kwa kiwanda cha dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) katika sakata la dawa bandia ya ARV.

Baada ya ufafanuzi huo wa Mhe. Waziri kutolewa, kumekuwa na taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari zinazoleta mkanganyiko kwa wananchi kuhusu suala hili.

Ili kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza, Wizara inapenda kutoa ufafanuzi  kuhusu tamko lililotolewa na Mhe. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.  Aidha, kama ilivyoelezwa katika taarifa mbalimbali za umma zilizokwisha kutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na  TFDA  kuhusiana na suala hili, bado inasisitizwa kwamba kampuni ya TPI Ltd iliiuzia Bohari  ya Dawa (MSD) dawa bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na. 0C.01.85, kwa mujibu wa nyaraka zilizopo.

Tunapenda kusisitiza kwamba, Mhe. Waziri katika hotuba yake hakukanusha kuwa kampuni ya TPI Ltd iliiuzia MSD dawa bandia bali alieleza kwamba uchunguzi wa awali katika kiwanda cha kampuni hiyo haukuonesha dawa hiyo ilizalishwa na TPI Ltd  bali vifungashio ni vya TPI Ltd na nyaraka zinaonesha TPI Ltd kuiuzia MSD dawa hizo bandia. Aidha, alieleza kuwa vyombo vya usalama bado vinaendelea kulichunguza suala hilo ili kubaini chanzo na wahusika wakuu wa dawa hizo bandia.

Kwa kuzingatia unyeti wa suala hili, Wizara inatoa wito kwa vyombo vya habari kusubiri hatma ya uchunguzi unaofanywa na vyombo vya usalama na kuepuka kutoa taarifa ambazo zinaweza kupotosha umma na jitihada kubwa za Serikali katika kupambana na dawa bandia nchini.

N. Mwamwaja
MSEMAJI
16 Mei, 2013.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 16, 2013

    Kama ulitengeneza au kampuni iliuza hakuna tofauti muhimu dawa ni feki cha kuchunguza dawa imedhuru na kusababisha vifo vya watu wangapi. Kila dawa ni lazima katika boxi na karatasi ya maelezo yake inaandikwa imetengenezwa na kampuni gani sasa nini kinachunguzwa?

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 16, 2013

    Mimi mafno ninaitwa KALULU GENDAGENDA.

    Pana tuhuma za kukutwa mbuzi wa wizi ktk Gunia lenye jina langu HUKU IKITHIBITISHWA AMETOKEA MIKONONI MWANGU bado huyo mbuzi itakuwa mimi sihusiki naye ama hakuna uhakika kama mimi huyo mbuzi ninammiliki?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...